MILIONI MIA TATU KUJENGA KIVUKO KATI LONG'DONG NA LOLOVONO.

_Mbunge wa Arusha Mrisho Gambo (katikati) aliyevaa shati jeusi akiwa na viongozi wa chama cha Mapinduzi (CCM) wakiingia katika viwanja vya mkutano uliofanyika kata Sokoni (1) Leo Jijini Arusha_


Egidia Vedasto

Arusha

Wananchi wa kata ya Sokoni (1) wameipongeza serikali na juhudi za Mbunge wa Arusha Mrisho Gambo, kwa mpango wa kujenga kivuko ambacho kwa muda mrefu kimekuwa changamoto kubwa hasa kwa kipindi kama hiki ambacho mvua kubwa zinaendelea kunyesha.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wa Long'dong kata ya sokoni one Jijini Arusha, Gambo amesema tayari amefanya mazungumzo na TARURA na wameahidi kuanza kutekeleza ujenzi wa kivuko hicho mapema iwezekanavyo.

Aidha ameeleza kwamba, ataendelea kushirikiana na viongozi wengine wa serikali ngazi za kata na mitaa kutatua changamoto mbalimbali  ili wananchi wapate muda wa kufanya shughuli zao za maendeleo.

"Nitaendelea kusikiliza kero na kuzifanyia kazi kama ambavyo nimekuwa nikifanya katika mikutano yote niliyoifanya hapo awali lengo ni kuboresha miundombinu  na kurahisisha maendeleo ya wananchi" amesema GAMBO.

Kwa upande wake mkazi wa Mtaa Long'dong Norah Mollel amesema ujenzi wa kivuko utawarahisishia maisha, kuokoa pesa na muda tofauti na ilivyo sasa.

"Hiki kivuko ni muhimu mno kwa maisha yetu, ukiangalia wanafunzi wengi wa Long'dong wanavuka korongo kuelekea Lolovono ambako kuna shule nyingi ikiwemo Good Hope,  Barbra, Royal Vision na sokoni (1)

" Pia kuna vituo vya afya ikiwemo kituo cha Kanisa Katoliki na Maria Stoppers na kwa sasa ni shida kupata huduma hizo kwa urahisi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kupelekea korongo kujaa maji,  hivyo tunatumia muda mwingi kuzifuata huduma na tunatumia gharama kubwa" amefafanua Mollel.

Sambamba na hayo Gambo ameahidi kuwekwe matuta katika barabara ya Mnara wa voda unaounganisha barabara ya Sombetini na Morombo, ambapo wanafunzi wamekuwa wakigongwa wakati wakivuka kutokana na ukosefu wa matuta.

_Kulia ni Priscus Kway aliyejiunga na chama cha Mapinduzi (CCM) leo akitokea (CHADEMA)

Wakati huo huo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempokea mwanachama mpya kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Priscus Kway aliyekuwa mwenyekiti wa mtaa Sokoni one kupitia (CHADEMA) mwaka 2014-2019, baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mrisho Gambo.

"Nimeamua kuhamia (CCM) kwa maamuzi yangu bila kushawishiwa na mtu, kwa sababu nimeridhishwa na utendaji kazi wa Gambo kwa jitihada zake kubwa anazozifanya kutuletea maendeleo wana arusha, naahidi ushirikiano mkubwa kwa chama na  wanachama, najiamini siyumbishwagi uzuri wananchi wananitambua" ameeleza Kway.

_Gambo akizungumza jambo na Mtendaji wa TARURA, ni katika ukaguzi wa kivuko kinachotarajiwa kujengwa kati ya Long'dong na Lolovono katika kata ya Sokoni (1)

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post