WITO MAADHIMISHO SIKU YA WANAWAKE,WAZAZI WATAKIWA KUTENGA MUDA WA KUSIKILIZA WATOTO

Mkuu wa wilaya ya Arumeru Emmanuela Kaganda akikagua mabanda ya wajasiriamali katika viwanja vya Ngarenaro jijini Arusha

Na Egidia vedasto

Arusha

Wanawake wametakiwa kulinda na kudumisha tamaduni za Kiafrika, kutenga muda wa kukaa na watoto ili kunusuru kizazi  chetu na kuwa na watoto wenye maadili mema katika jamii watakaolitumikia Taifa kwa weledi.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wanawake yaliyofanyika katika viwanja vya Ngarenaro Jijini Arusha Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda amesema wanawake wasiige tamaduni za kigeni ambazo zinaharibu mawazo ya wengi, na kupelekea kukosekana kwa muda wa kuangalia watoto katika malezi na makuzi.

Aidha amesema wanawake kupewa nafasi mbalimbali za uongozi, fursa za kujiinulia uchumi pamoja na kushirikishwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo wanatakiwa kuwa chachu  na sio kuwa kikwazo cha jamii.

"Mwanamke wa sasa akishapata pesa utasikia sitaki kuolewa, sitaki kuzaa, jamani hayo sio maisha tuache kuiga tamaduni ambazo hazina maadili kwetu na badala yake tutumie nafasi hizo kuwa mfano bora wa kuigwa na wengi kwa kujenga familia na kushirikisha wenza katika maendeleo hayo" Kaganda amewaasa wanawake.

Kaganda amewataka wanawake kujifunza kwa mama zetu wa zamani jinsi walitenga muda kulea na kuzungumza na watoto ambapo matokeo yanaoonekana leo kwa kuzalisha viongozi bora na wenye maadili.

Wakati huo huo amewataka wanaume kuacha vitendo vya ukatili na unyanyasasji vinavyoacha makovu na majeraha makubwa katika mioyo ya wanawake na watoto badala yake wasaidiane na wenza wao kulea na kuzungumza na familia zao ili kujenga jamii bora.

"Inasikitisha sana, wanaume wanapiga wanawake, wanaua, jamani yatima wanaongezeka lakini pia tunatengeneza jamii yenye hasira kwa maumivu makali wanayopitia wakati  vitendo vya ukatili vikijitokeza" Kaganda amesema.

Mkurugenzi wa kituo cha Wanawake na Maendeleo ya Watoto (CWCD) Hindu Mbwengo akitoa hotuba yake leo katika maadhimisho ya siku ya wanawake jijini Arusha

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Wanawake na Maendeleo ya Watoto (CWCD) Hindu Mbwengo amesema wazazi wote wana jukumu la kuwa waangalizi katika makuzi ya watoto na si kuachiwa mwanamke peke yake.

Hindu ameeleza kuwa watoto wote wa kike na wakiume wapewe elimu ya kutambua dalili za viashiria vya ukatili na unyanyasaji na jinsi ya kutoa taarifa ili kukomesha vitendo hivyo.

"Kituo chetu tunajihusisha na utoaji elimu mashuleni  kwa watoto wa kike na kiume maana wamesahaulika katika kupewa elimu ya makuzi na jinsi ya kuwalinda dhidi ya vitendo vya unyanyasasji na ukatili ambavyo vimeshamiri kwa nyakati hizi" amesema Hindu.

Hata hivyo Baba wa zamu Daniel Sambu, kutoka kituo cha Wanawake na Maendeleo ya Watoto (CWCD)   amesema ni mhimu elimu iongezwe kwa watoto wa kiume kwani jamii ilisahau kuwapa elimu na ikawekeza elimu kwa watoto wa kike tu.

"Watoto wa kiume wameshambuliwa na vitendo vya unyanyasaji kwa kiasi kikubwa, inaumiza sana lakini inatubidi tuongeze kasi ya kutoa elimu ili na mtoto wa kiume ajitambue, kabla hajafanyiwa vitendo vya ukatili ajue dalili ambazo watu wenye malengo mabaya wanazitumia katika kushawishi kuwaingiza huko" amesema Sambu.

Mwenyekiti wa wanawake TANESCO Mkoa wa Arusha Tilda Mollel amesema suala la malezi na makuzi ya mtoto si la msichana wa kazi za nyumbani bali ni la wazazi wote kutenga muda kuwasikikiza na kuwafundisha watoto ili kuandaa kizazi chenye maadili mema na utiifu.

Baba wa zamu (Father on Duty) kutoka kituo cha Wanawake na Maendeleo ya Watoto (CWCD) katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani leo jijini Arusha

Mollel amesema, licha ya wanawake kuwa na majukumu mazito ya kujenga taifa, ni mhimu kubeba jukumu la uangalizi wa watoto kwani ndio taifa la kesho na ndio watakuwa walezi wa kesho.

"Nikiri sisi wanawake tuna majukumu mengi, wengine ofisini, wengine biashara lakini tujitahidi kadri tuwezavyo tutenge muda wa kuzungumza na watoto wetu ili tujue maendeleo yao, changamoto wanazokutana nazo na hata mambo mazuri watakayohitaji kutoka kwetu wazazi" amefafanua Mollel.

Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yalianza rasmi mwaka 1911 nchini Marekani baada wa wafanyakazi wa kazi za ndani kuandamana wakilalamika kutopewa haki za msingi kama huduma za bima ya afya, ujira mdogo, kubaguliwa  na kutopata muda wa kupumzika, sambamba na hayo maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu inayosema "Wekeza kwa Wanawake ili Kuharakisha Maendeleo yao na Taifa".

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post