SMAUJATA MKOA WA SHINYANGA WAKUTANA NA KUZUNGUMZA NA ASKOFU SANGU WA KANISA KATOLIKI JIMBO LA SHINYANGA

Askofu wa Kanisa katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu akizungumza na viongozi wa kampeni ya kupinga ukatili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Askofu wa Kanisa katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu amesema jukumu la kulinda maadili ya jamii linahitaji ushirikiano wa dhati kuanzia hatua ya malezi na makuzi ya Mtoto  katika ngazi ya familia.

Ameyasema hayo  wakati akizungumza na Viongozi wa kampeini ya kupinga ukatili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga walipomtembelea jimboni kwa lengo la kumpongeza kutokana na juhudi zake katika mapambano ya kupinga ukatili.

Askofu Sangu amesisitiza kuhusu Msingi na umuhimu  wa Elimu ya ukatili  kuanzia  kwenye ngazi ya familia ili kujenga jamii yenye maadili mema.

“Sisi sote kwa pamoja tuendelee kushirikiana katika kujenga jamii yenye maadili mema  lakini hii Elimu ya ukatili dhidi ya binadamu lazima ishuke iende kwenye Familia, Familia ndiyo shule baadhi ya Familia watoto wanakua hawalelewi yaani Mama anamuacha mtoto kwenye kisenta anaenda kufanya kazi zake sasa yule mtoto analelewaje anafundishwa maadili ya namna gani kwa sababu mtoto kuanzia Mwaka mmoja hadi Miaka saba lazima awe karibu na wazazi kumbe tunapopeleka watoto kwenye Baby care asilimia 85 ya mtoto ni ya yule siyo yako tena mzazi ndiyo maana tabia mbalimbali sana zinaibuka”amesema Askofu Sangu

Amesema Kanisa litaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau wote katika juhudi za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kumshirikisha mwenyezi Mungu

Ametumia nafasi hiyo pia kuipongeza kampeni ya SMAUJATA kwa kuguswa kujitolea katika kupambana na ukatili wa kijinsia  huku akiwakumbusha kuendelea kumtanguliza Mungu

“Nimethamini wito wenu na kile mnachokifanya kwa ajili ya jamii sote tuko pamoja katika kupambana na hili janga kubwa la ukatili lakini ukatili umekuwa mbaya zaidi kwa sababu uko ndani ya Familia kama ni Shetani ameingia ndani kabisa kwenye chimbuko la maisha la ustawi wa jamii na kwa nini ukatili upo kwa sababu binadamu hathamini utu wa mtu mwenzake tunaposahau hii kwamba binadamu ameumbwa kwa sura ya mfano wa Mungu tunapotea kabisa maadili yanapotea”

“Kumbe kwenye kampeni hii tuko pamoja nawaalikieni katika Kanisa letu njooni kuna makongamano ya vijana njooni, semina za vijana njooni, vigangoni kwenye Parokiani njooni, Radio Faraja iko hapo tumieni Radio lakini tunawakaribisheni katika ngazi zote”.

“Kwahiyo basi tutaendelea kushirikiana lakini tukumbuke yote yanawezekana katika yule atutiaye nguvu  pamoja na kampeni yetu hii ya SMAUJATA tumtangulize zaidi Mungu pamoja na kufanya juhudi zetu zote za huku na huku tujue kwamba bila Mungu hatuwezi chochote kumbe tuikabidhi yote mkononi mwa Mungu”.amesema Askofu Sangu

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti idara ya Itifaki, uanachama na uenezi Bwana Solomon Najulwa amelipongeza Kanisa katoliki Jimbo la Shinyanga kwa juhudi zake mbalimbali za kupinga ukatili.

 “SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga inalipongeza sana Kanisa Katoliki lakini pia kwa usimamizi wako mzuri sana Baba Askogu Liberatus T.K Sangu kwa jinsi ambavyo Kanisa limeendelea kupinga ukatili katika mahubiri na makongamano mbalimbali ambapo sisi SMAUJATA huwa tunafuatilia sana tukijua kwamba Kanisa liko pamoja na SMAUJATA kwahiyo nirudie kwa kusema kwamba Baba Askofu Mungu akubariki sana wewe pamoja na uzao wako na Kanisa kwa ujumla mpate kubarikiwa siku zote”.amesema Najulwa

Kwa upande wake Katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana Daniel Kapaya naye ametumia nafasi hiyo kumpongeza na kumshukuru Askofu Sangu kwa kuendelea kutekeleza vema utume wake.

“Jambo la msingi kuja katika eneo hili Baba Askogu kwanza kabisa ni kukupongeza na kukushukuru kwa kufanya kazi kubwa sana ya kupinga ukatili umekuwa ukizungumza katika mahubiri yako ambayo tunayafuatilia sana lakini vile vile tunasikia katika vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na Radio Faraja unakemea sana vitendo vya ukatili”.amesema Kapaya

Viongozi wengine wa kampeni hiyo akiwemo Mwenyekiti wa idara ya Utamaduni, mila na destori Mwinjilisti Esther Emmanuel, Mwenyekiti wa idara ya uhitaji, maafa na makundi maalum Mhandisi Peter Mangula, Mwenyekiti idara ya jinsia Ispekta Alkwin Willa, pamoja na Mwenyekiti idara ya Elimu (Wanafunzi, Vyuo na Vyuo vikuu) Mwalimu leonard Mapolu wamepongeza huku wakiahidi kutekeleza majukumu yao kwa haki za usawa kwa lengo la kutokomeza ukatili wa kijinsia Mkoa wa Shinyanga.

Shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania (SMAUJATA) ni kampeni ya kupinga ukatili Nchini ambayo inatekeleza majukumu yake chini ya Wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum.

Kampeni hiyo ipo Mikoa yote na kwamba imeanzishwa na Mwenyekiti wa SMAUJATA Taifa Shujaa Sospeter Bulugu kwa kushirikiana na Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum Dkt. Dorothy Gwajima kwa lengo la kushirikiana na Serikali katika kupinga vitendo vyote vya ukatili Nchini.

Kwa niaba ya Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti idara ya Itifaki, uanachama na uenezi Bwana Solomon Najulwa amelipongeza Kanisa katoliki.

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post