SIMBACHAWENE: MSD KUWENI WAZALENDO KATIKA UTOAJI HUDUMA.

Wajumbe wa Kamati Kuu Bohari ya Dawa (MSD) wakiwa na Mgeni Rasmi George Simbachawene (katikati) Jijini Arusha, Watatu kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Taifa Mavere Tukai na wa pili kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Tughe Mkoa Dar es salaam, Tughe Taifa na Mlezi wa Tawi la (MSD) Brendan Maro.

Na Egidia Vedasto, Arusha.

Watumishi wa Bohari ya Dawa ya Taifa (MSD) wametakiwa kuwa waaminifu na wazalendo katika utendaji kazi wao kwani ndio kiini cha mwananchi kuwa na afya bora.

Akizungumza katika kikao cha 23 cha Baraza la Wafanyakazi wa Bohari ya Dawa ya Taifa (MSD) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema watumishi wanatakiwa kuwatendea vizuri wananchi ili wasahau zile nyakati za nyuma ambazo huduma za MSD zilikuwa mbaya. 

Aidha amewasisitza kuagiza vitendea kazi bora vinavyosoma magonjwa na dawa vizuri ili wananchi wapate huduma wanayostahili.

"Hamuwezi kupata mafanikio kwa kuagiza vifaa vibovu wala dawa zilizoisha muda wa kutumika, mkumbuke itakuwa laana kwenu na kwa kizazi chenu chote, fikiria unasambaza dawa zilizoisha muda, watu wanapata kansa wewe unajivunia umefanya kazi, manunguniko ya wanadamu ni mabaya sana hayamuachagi mtu aishi kwa amani"

"Kumbukeni nyinyi ndio waagizaji, watunzaji na wasambaji, mkishawishiwa mkaagiza vifaa vibovu, huo ni usaliti na uhujumu uchumi, na sio uzalendo kabisa" amesisitiza Simbachawene.

Ameongeza kuwa, kwa sasa mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mkurugenzi Mkuu wa sasa, yanaonyesha utendaji kazi mzuri na kuhimiza  kama utaendelea kuwa mzuri 

basi Bohari ya Dawa ya Taifa itasambaza dawa na vitendea kazi katika makampuni ya Jumuiya ya SADC hatua ambayo itakuwa imefikia malengo makubwa.

"Niwakumbushe tena, tabia ya kuandika vikaratasi na kujifungia ofisini mkipitisha pesa kwa maslahi yenu haitafaa tena kwani sasa hivi serikali mtandao imejipanga sawasawa yaani hawacheki na mtu ukibainika jela inakuhusu" amesema Simbachawene".

Pia amewakumbusha MSD kuiga utaratibu wa kisasa wa kusafirisha dawa kwa kutumia magari yenye mfumo wa ulinzi kama yale ya kusafirisha sigara au  kusafirisha kwa ndege na hata kutumia treni ya kisasa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Taifa (MSD) Mavere Tukai amesema kwa sasa huduma zimeboreshwa na wananchi wataendelea kupata huduma bora.

Ameendelea kufafanua kwamba, wataendelea kufundishana utumishi bora, kusimamia malengo ya serikali na kufanya MSD kujiendesha  kibiashara.

"Kutokana na Baraza hili tumejipanga kuendeleza ukaguzi na usimamizi wa watumishi wa MSD, lakini pia atakayefanya vizuri atapewa motisha na atakayefanya vibaya ataadhibiwa" ameeleza Tukai.

Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam,  Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa na Mlezi wa Tawi la MSD Brendan Maro, amesema Baraza hili limesaidia kuboresha utendaji kazi kutokana na kubadilishana mawazo na ujuzi.

Washiriki katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Bohari ya Dawa Taifa (MSD)

Amefafanua kwamba katika baraza hili,  kumewekwa mikakati mizuri ya kiusalama, uwasilishaji wa bajeti ya taasisi na kukumbushana dhana ya ushirikishwaji mahali pa kazi.

Kikao hicho kilichodumu kwa siku tatu jijini Arusha kimejumuisha Wakurugenzi, wasimamizi na Wakuu wa vitengo kutoka kanda kumi za  Bohari  ya Dawa ya Taifa.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post