MKUU WA WILAYA ARUSHA AZINDUA WIKI YA KERO

Mkuu wa wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa akizungumza na viongozi  pamoja na wananchi


Na Egidia Vedasto 

Arusha.

Wananchi wilaya ya Arusha wameendelea kumimika kueleza kero zao katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo katika wiki ya kero iliyozonduliwa leo tarehe 26 na itakayoendelea hadi siku ya Jumapili March 02 mwaka huu. 

Akizindua wiki ya kero Mkuu wa wilaya ya Arusha mjini Felician Mtahengerwa, amesema kusikiliza kero za wananchi utakuwa utaratibu wa kudumu ili kuhakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa.

Mkutano huo umehusisha watendaji na viongozi mbalimbali wa serikali kuanzia ngazi ya mtaa akiwemo Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Juma Hamsini, Katibu Tawala Wilaya, Mstahiki Meya Maximilian Iraghe pamoja na na baadhi ya madiwani.

"Viongozi wenzangu nawasihi tuwe tunawasikiliza wananchi kuanzia ngazi ya mtaa na msipowasikiliza watakuja ofisini kwangu nitawasikiliza, maana ninachokitaka wafanye shughuli zao wajipatie maendeleo na sio kuzunguka ofisini kueleza kero bila majibu ya kueleweka" Mkuu wa wilaya Mtahengerwa ameeleza.

Ameendelea kusema kuwa makundi mbalimbali ikiwemo wanawake na watu wenye ulemavu watapewa mtaji usio na masharti ili kupunguza umaskini na kujikimu mahitaji ya msingi.

Amesema pia wananchi wenye kero za ardhi  zitafanyiwa kazi kwani ofisi ya Mkuu wa wilaya imeandaa mawakili wawili watakaosaidia katika kesi hizo, sambamba na wazabuni wanaoidai halmashauri ya Jiji kulipwa madeni yao yote kabla ya Juni 31 mwaka huu ambapo wengine wameshaanza kulipwa.

Aidha amewataka viongozi wa ngazi za mtaa kuweka ulinzi katika mitaa yao dhidi ya watu wanaotupa taka ovyo kwani wanachafua mandhari ya Jiji hivyo utaratibu wa kuwatoza faini ya shilingi laki tatu hadi milioni kwa atakayebainika akitupa taka ovyo.

"Nawaagiza viongozi mliopo hapa kupambana na makundi ya wakabaji na vibaka katika mitaa kwani wanaleta hofu na kukosesha Jiji mapato kwani tunapata wageni lakini wakundi hayo yasipoondolewa tutakosa dola maana wageni watakuwa wanabaki kujifungia hotelini badala ya kuzunguka kununua vitu mbalimbali" Mkuu wa wilaya amesisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Juma Hamsini amesema halmashauri ya Jiji la Arusha inaongoza kwa vibali feki vya ujenzi kwa asilimia 85, vinavyoleta mkanganyiko kati ya wananchi na serikali. 

"Ni aibu kubwa na haitakubalika, nataka hili suala likomeshwe kwani  hili linahusishwa na ubadhilifu wa mali za umma na linachafua taswira ya Jiji letu" amesema Mkurugenzi Hamsini.

_wananchi wakisikiliza kwa makini hotuba kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa_

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post