LOWASSA ATAKUMBUKWA KWA UZALENDO:RAIS Dkt SAMIA

 

Na Egdia Vedasto, Monduli

Viongozi wa vyama vya siasa wametakiwa kuwa wazalendo wa kweli, wastahimilivu na kutenda haki katika maisha Yao ya utendaji kazi pindi wanapopata madaraka.

Akitoa salam za rambirambi, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, nyumbani kwa Hayati Edward Lowassa Kijiji Cha Ngarashi wilayani Monduli Mkoani Arusha amesema Lowassa atakumbukwa kwa uthubutu wake aliokuwa nao katika kipindi chake chote Cha utendaji kazi.

"Amejitolea maisha yake yote kwa ujasiri na ushupavu  akihakikisha analeta mabadiliko katika nchi hii ikiwemo mchango wake mkubwa wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria pamoja na uanzilishi wa shule za kata ambazo zimeleta mageuzi makubwa kielimu," amesema Mheshimiwa Rais.

Amesema Taifa limepoteza  mwanamageuzi  na kipenzi cha wengi aliyefanya kazi kubwa na kuleta mabadiliko chanya ambayo yanamgusa kila mmoja  leo.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt Tulia Ackson amesema, ni mhimu viongozi wajifunze kuacha alama nzuri katika utendaji kazi wao pindi wanapopata  madaraka ya kuwatumikia wananchi

"Kama maandiko ya neno la Mungu yanasema siku za mwanadamu anayezaliwa na mwanamke ni chache na zinahesabika hivyo tujifunze kutenda mema na kutenda haki maana Mungu hadhihakiwi" amesema Dkt. Tulia.

Wakati huo huo Kiongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe amesema kwamba Lowassa atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika siasa za chama hicho alichodumu kwa miaka minne ambapo alisimama kugombea kiti Cha Urais mwaka 2015 kupitia Chama hicho.

"Huwezi kuiandika historia ya Hayati Lowassa ukakiacha Chama Cha Demokrasia na Maendeleo na kama mjumbe wa kamati kuu ya Chama, tutaukumbuka ukarimu wake na Kasi kubwa ya mabadiliko aliyoyaleta kwa kipindi hicho na kufanya wapatikane wabunge 115 na Madiwani 2000  wa viti vya udiwani katika uchaguzi wa mwaka 2015, niseme yeyote aliyefanya kazi na Lowassa aliishia kuwa rafiki yake" amesema Mbowe.

Maelfu ya watu na viongozi mbalimbali  kutoka sehemu mbalimbali za nchi na Magavana kutoka Kenya wamejitokeza kuupumzisha mwili wa Hayati Lowassa aliyefariki tarehe 10 February na kuzikwa Leo Kijijini kwake Ngarashi, Monduli Mkoani Arusha.

Hayati Lowassa ameacha Mjane Mama Regina  na watoto watano akiwemo Mbunge wa Monduli Fredrick Edward Lowassa.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post