CHADEMA YATANGAZA MAANDAMANO ARUSHA WIKI IJAYO.

Godbles Lema akiwa jukwaani na kina Mama wafanyabishara ndogo ndogo

Na Egidia Vedasto,

Arusha.

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kufanya maandamano yanayotarajiwa kufanyika tarehe 27 Februari 2024  mkoani Arusha ikiwa ni muendelezo wa maandamano yaliyofanyika Dar es salaam na Mwanza.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Soko Kuu mjini hapa, Mwenyekiti wa  Chadema  Kanda ya Kaskazini , Godbless Lema, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kudai haki zao kupitia maandamano.

"Nimekuja kuwalazimisha muandamane wababa, wamama, wafanyabiashara wakubwa na wadogo kwa sababu hali ni mbaya sana  kiuchumi kila mmoja wetu ni shahidi, maana vitu sokoni havishikiki". Amesema Lema

Aidha amewataka wananchi kuondoa hofu na woga juu ya maandamano ili kupigania haki zao za kupata katiba mpya na kukataa miswada ya Sheria iliyopelekwa Bungeni kusainiwa yenye lengo la kuminya uhuru wa chaguzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadae mwaka huu  na uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani  utakaofanyika Mwakani 2025.

"Arusha nisikilizeni,  kuweni kioo cha haki kwa niaba ya watanzania wengine kwa kuandamana ili kukataa mambo mabaya yanayoendelea nchini, yanayodidimiza uchumi wa wengi ikiwemo kukatika kwa umeme kila wakati na kupanda bei kwa bidhaa muhimu kama sukari na ikiwezekana  mlale katika vituo yatakapoanzia maandamano  ili asubuhi na mapema ya tarehe 27 mwezi huu muwahi barabarani" amesisitiza Lema

Lema amewahakikishia wananchi kuwa kutakuwa na ulinzi wa kutosha kutoka kwa jeshi la polisi na maandamano yataanzia ofisi za Mamlaka za Hifadhi za Taifa (TANAPA) zilizopo eneo la Majengo na mengine yataanzia Philips muda wa saa mbili kamili asubuhi.

"Nawambieni Mama zangu mama ntilie, wauza mitumba, dereva bodaboda na makundi mengine ya wafanyabiashara  jamani jitokezeni serikali itambue tumechoka na tunataka mabadiliko, tuiondoe serikali madarakani serikali ya Chama Cha  Mapinduzi (CCM), nawaambia ndugu zangu tufanye mabadiliko kwa kuichagua CHADEMA itakayotupa mwanga wa maisha."

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum  Mwalimu amesema maandamano hayo hayafungamani na dini, itikadi za vyama wala ukabila, bali ni ya kudai unafuu wa maisha kwa kila mtanzania.

Mwalimu ameongeza kuwa kila mmoja anatakiwa kuhakikishiwa haki ya uhuru,  na kupata mahitaji   yake  ya msingi ya kila siku kwani nchi ya Tanzania ina rasilimali za kutosha za kuhakikisha kila mwananchi anaishi maisha yasiyo ya mateso.

"Ndugu zangu tukikubali kuandamana naamini tutapata haki ya katiba mpya itakayoondoa sheria kandamizi, kwani hayo yanatuhusu sisi na vizazi vijavyo na ni kwa mustatakabali wa Taifa letu.

Mmoja wa waendesha bodaboda  Mkoani Arusha Abdul Salehe amesema wao kwa umoja wao watajitokeza kwa wingi kuandamana ili serikali iliyopo madarakani iwapatie nafuu ya maisha.

" Yaani siku hizi maisha yamezidi kuwa magumu maana vyakula vimepanda bei, umeme unakatika na petroli imepanda bei wakati huo huo marejesho kwa mabosi zetu yako pale pale, nakwambia ukweli maisha yamekuwa magumu mno kiasi kwamba hata mlo kwa familia zetu ni shida" ameeleza Salehe.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post