BARAZA LA MADIWANI LA HALMASHAURI YA WILAYA YA KISHAPU LIMEJADILI NA KUPITISHA MAPENDEKEZO YA BAJETI YA HALMASHAURI HIYO NA TARURA KWA MWAKA WA FEDHA 2024/2025

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. William Jijimya akizungumza kwenye Baraza hilo leo Februari 20,2024.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu limejadili na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Halmashauri hiyo ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 yenye jumla ya shilingi Bilioni 40 Milioni 821 na 3372.

Tamko hilo limetolewa leo Februari 20,2024 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. William Jijimya baada ya Madiwani kurithia kwa pamoja mapendekezo hayo.

Baraza hilo limepitisha mapendekezo ya bajeti  huku wakisisitizwa watendaji wa Halmashauri hiyo kuendelea kushirikiana na viongozi wengine wakiwemo Madiwani hasa katika suala la ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Wote kwa pamoja baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu tumejadili na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Halmashauri  ya Mwaka 2024/2025 yenye jumla ya shilingi Bilioni 40 Milioni 821 elfu 3372”.

“Kupitisha bajeti siyo suala tu la makaratasi twendeni tukashikane mashati kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato tusiruhusu chochote kitoke kwenye Halmashauri yetu bila kutoa ushuru tunaomba mkurugenzi kupitia wataalam wako tuonyesheni ushirikiano watendaji mtusikilize na siyo tu kutusikiliza nendeni mkatende kama ambavyo tumeshauri ili kuwaweka sawa wananchi wetu”.amesema Mwenyekiti Mhe. Jijimya

Pia Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu limepitisha mpango na mapendekezo ya bajeti ya matengenezo ya Barabara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 ambayo itatekelezwa na wakala wa Barabara za vijijini na mijini Tanzania (TARURA) Wilaya ya Kishapu.

Awali akisoma taarifa ya mapendekezo hayo kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Kishapu Mhandisi Hussein Shaweji amesema zaidi ya Bilioni mbili zitatumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo  matengenezo ya barabara kwa lengo la kuboresha miundombinu ya Barabara katika Wilaya ya Kishapu.

Wakati huo huo baadhi ya Madiwani wa kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wameitaka TARURA kutekeleza kwa vitendo bajeti hiyo ikiwa ni pamoja na kuyafikia maeneo korofi hasa kipindi hiki cha msimu wa mvua ili kuepusha usumbufu kwa wananchi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Emmanuel Jonhson ameahidi kusimamia mpango huo wa bajeti uliopendekezwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwemo suala la ukusanyaji wa mapato ya ndani.

“Niwashukuru kwa kujadili na kupitisha bajeti zetu zote mbili bajeti ya TARURA na bajeti ya Halmashauri niwaahidi kwamba yale mapendekezo tuliyokubaliana tutayasimamia, sisi mmetuachia kazi tunajukumu la kuhakikisha tunakusanya mapato ili kile kilichoidhinishwa kikatekelezwe kwa ukamilifu”.amesema Mkurugenzi Jonhson.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude amesisitiza viongozi wa serikali na wataalam mbalimbali kuendelea kushirikiana na Madiwani katika kubaini na kutatua changamoto za wananchi.

“Kinachotakiwa ni mawasiliano na kusikilizana na katika hili nisisitize watumishi wenzagu wote tukianza na mimi mwenyewe, Mkurugenzi, watendaji wa mamlaka za Serikali za mitaa lakini pia wezetu TARURA, RUWASA na wengine jamani tuwasikilize sana waheshimiwa Madiwani halafu tuwatimizie kwa sababu ndiyo hayo yanayotoka kwa wananchi”.amesema DC Mkude

Aidha Baraza hilo la Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu pamoja na viongozi wengine wa serikali akiwemo mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutatua kero za wananchi kupitia Fedha za miradi mbalimbali huku wakimpongeza Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake.

 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. William Jijimya akizungumza kwenye Baraza hilo leo Februari 20,2024.Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. William Jijimya akizungumza kwenye Baraza hilo leo Februari 20,2024.Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Emmanuel Jonhson akizungumza kwenye Baraza hilo leo Februari 20,2024.Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude akizungumza kwenye Baraza hilo leo Februari 20,2024.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu likiendelea leo Jumanne Februari 20,2024. 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post