MAPENDEKEZO YA MPANGO WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2024/2025 YAPITISHWA HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga  leo Alhamis Februari 8,2024 limepitisha mapendekezo ya mpango wa bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kiasi cha Shilingi Bilioni 40.5

Tamko hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe  Ngassa Mboje baada ya Madiwani kurithia kwa pamoja kwenye mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kupokea, kujadili na kupitisha rasimu ya mpango na bajeti 2024/2025 ambao umefanyika katika ukumbi wa makao makuu ya Halmashauri hiyo.

Pamoja na mambo mengine Mwenyekiti huyo ametamka rasmi kuridhia bajeti hiyo yenye jumla ya Bilioni 40.5 huku akisisitiza changamoto zilizopo kutatuliwa haraka ikiwemo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Mmetuonyesha nini tunatarajia kukifanya katika Mwaka wa Fedha unaokuja katika mapendekezo yenu wataalam wetu lakini sisi tumeridhia kwa pamoja na waheshimiwa Madiwani wajumbe wa Baraza maalum kupitisha bajeti yenye jumla ya Shilingi Bilioni 40.5 tunashukuru sana lakini kuna mambo ambayo tumeelekeza yafanyiwe kazi lakini kubwa sana ikiwa ni kiashiria cha hatali lile la Miezi sita (6) nusu Mwaka kuwa na asilimia 32 hiyo tuichukulie kama kiashiria cha hatali tunakwenda kumalizaje Mwaka wa Fedha unaoendelea sisi kama wawakilishi wa wananchi nia yetu ni kuhakikisha kwamba tunawahudumia wananchi wetu ambao wametuchagua katika yale ambayo wanayahitaji”.amesema Mhe. Mboje

Kutokana na hali ya ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Shinyanga ambapo kwa Miezi sita ya Mwaka huu wa Fedha 2023/2024 umefikia asilimia 32 mpaka sasa.

 Baadhi ya Madiwani kutoka kata mbalimbali za Halmashauri hiyo  wamemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kufikia malengo waliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kuongeza vyanzo vya mapato ambavyo vimesahaulika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Kisena Mabuba pamoja na mambo mengine ameahidi kushughulikia changamoto hiyo huku akiwaomba Madiwani kuendelea kusimamia mapato.

“Niombe sasa tuanze upya sisi tuwe kitu kimoja wakuu wa idara na watumishi wengine wote na waheshimiwa Madiwani tuzungumze sauti moja tunapomzungumzia mtu anatorosha ushuru tumzungumzie wote kwa sauti moja kama kuna mtu hawajibiki tumzungumzie wote kwa sauti moja hilo litatusaidia sana kila mmoja ajue mipaka yake na tupate kuisimamia tukifanya hivo mimi naomba niwatoe hofu tunatoka hapa tulipo, kuna watendaji mpaka wapigiwe simu mimi nimeshazungumza nao nimewaambia suala la mapato siyo suala la kubembelezana ni suala la wajibu kwa kila mtendaji”.amesema Mabuba

Akizungumza kwenye kikao hicho Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Shinyanga vijijini Edward Ngelela amemsihi Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kusimamia suala la mapato ya ndani huku akishauri kuundwa timu maalum kwa ajili ya kufuatilia suala hilo kwa watendaji wa kata ambapo pia amewaomba viongozi wa Halmashauri hiyo wakiwemo Madiwani wafanyabiashara kuwa mfano katika suala la kutoa ushuru.

Naye katibu tawala wa Wilaya ya Shinyanga amewakumbusha viongozi wa Halmashauri hiyo kuepukana na rushwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwenye mamlaka za kisheria kwa watu watakaobainika kujihusisha na rushwa.

Kaimu katibu tawala wa Mkoa wa Shinyanga Ibrahim Makana amelipongeza Baraza ma Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa kuridhia na kupitisha mapendekezo ya mpango wa bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kiasi cha Shilingi Bilioni 40.5.

 Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kupokea, kujadili na kupitisha rasimu ya mpango na bajeti 2024/2025 umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo wakuu wa idara na vitendo wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post