*GAMBO AFIKISHA KILIO CHA UMEME KWA MAKONDA*

Aliyekuwa Mbunge wa Longido na Mwenyekiti wa CCM Mstaafu Michael Laizer akimkabidhi fimbo katibu wa Siasa na Uenezi Paul Makonda kama ishara ya kumsimika kuwa kiongozi mkubwa katika jamii ya wamasai Laigwanan

Na  Egidia Vedasto, 

Arusha.

Kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme linaloendelea nchi nzima, Mbunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo amemuangukia  Katibu wa siasa na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (CCM) Paul Makonda kutoa ufumbuzi wa tatizo hilo.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya stendi ya Kilombero iliyopo katikati ya jiji hilo, Gambo amesema anasimama upande wa wananchi kwa sababu  wananchi hawafanyi kazi sawasawa  kama ilivyokuwa hapo awali kwa kuwa tatizo hilo linarudisha nyuma maendeleo yao.

"Kwakweli suala hili linaumiza sana wananchi, hawafanyi biashara zao vizuri huku wakidaiwa kodi na kulipa mapato kama kawaida" amesema Gambo.

Akitoa ufafanuzi juu ya changamoto hiyo Makonda ameitaka wizara ya Nishati ya umeme kuzalisha  megawati za kutosha kulingana na mahitaji ya wananchi na kuongeza kwamba wizara itafute namna ya kuwaongezea wananchi units kama fidia kwa kipindi ambacho umeme umekatika mfululizo.

Amesisitiza kwamba taarifa za kukatika kwa umeme zitolewe ili wananchi wajue ratiba kamili ya upatikanaji wake jambo litakalisaidia kupanga shughuli zao kutokana na upatikamaji wa umeme.

"Lakini niseme pia, kusitokee baadhi ya maeneo kupata umeme usiku mara kwa mara kwa sababu hali hiyo haiwasaidii kwani shughuli za wananchi wengi hufanyika nyakati za mchana kwa hiyo ni lazima mzingatie mahitaji yao kwa wakati sahihi" alisema Makonda.

Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Paul Makonda akivalishwa shuka ikiwa ni vazi rasmi wanalovaa wazee wa Mila wa Jamii ya Kimaasai Mkoa wa Arusha akiwa katika ziara ya kikazi na kujitambulisha kwa wanachama wa CCM Mkoa wa Arusha

 

Baadhi ya wananchi wakizungumza na mwandishi wetu wamesema tatizo la kukatika kwa umeme limekuwa kero ya muda mrefu na kukatika bila taarifa jambo linalokatisha tamaa na kurudisha nyuma maendeleo yao.

Wananchi hao wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya umeme ili kuondoa shaka na kujenga imani kwa wananchi juu ya serikali yao ya Chama cha Mapinduzi.

"Kama kweli wanataka kutuaminisha juu ya haya yanayozungumzwa basi hili tatizo limalizike, kwa sababu linaendelea kututesa na hatujui ni lini litamalizika" alisema James Mbise aliyekuwa katika mkutano huo.

Kwa upande mwingine Makonda amezungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Maji Jumaa Aweso na kumtaka kutatua changamoto ya maji mkoani humo ikiwa ni pamoja na kukatika kwa maji baadhi ya maeneo wateja kupewa bili zinazokinzana na matumizi sahihi.

"Mbali na changamoto ya kukatika kwa maji na wateja kubambikiwa bili kubwa za maji lakini pia suala la maji chumvi liangaliwe ili kuepuka kuhatarisha afya za watumiaji" alisisitiza Makonda.

Akijibu changamoto hizo Waziri Aweso amesema zitafanyiwa kazi ikiwemo utaratibu wa kufunga mita za lipa kabla (prepaid meter) kwa kila mteja zoezi ambalo tayari zimeanza katika taasisi za serikali.

Aidha Waziri Aweso ametoa angalizo kwa wananchi pindi zoezi hilo litakapoanza kwa kuwauliza watumishi hao wa maji vitambulisho vyao vya kazi ili kuepuka matapeli.

"Niahidi kuwa wiki ijayo nitakuwa Arusha kwa ajili ya kushughulikia changamoto zote zilizobainishwa lengo likiwa kila mwananchi apate huduma hii ya msingi" alisema Aweso.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post