WANANCHI WAISHUKURU TPA KWA MSAADA WA VITANDA VYA WAJAWAZITO ZAHANATI YA NDANDALO

Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Manga Gassayah(kushoto) akikabidhi sehemu ya vitanda vitando vya kujifungulia wajawazito kwa Mganga Mkuu wa wilaya ya Kyela, Dk Saumu Kumbisaga kwaajili ya zahanati ya Ndandalo. Mamlaka ya usimamizi wa Bandari( TPA) imekabidhi msaada vitanda na mashuka 200 wenye thamani ya Shilingi milioni 10 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Bandari nchini. (Picha na Joachim Nyambo)


 

Na Joachim Nyambo, Kyela.

 

NDEREMO na vifijo vimetawala katika viunga vya Zahanati mpya ya Ndandalo iliyopo wilayani Kyela Mkoani Mbeya baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari( TPA) kukabidhi msaada wa vitanda vitano vya kujifungulia wajawazito na mashuka 200.

 

Mwanamke Sophia Mwangupile aliyewahi kujifungua mtoto njiani akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Kyela ni miongoni mwa wakazi wa Kata ya Ndandalo wilayani hapa ambao wameipongeza TPA kwa msaada huo uliogharimu jumla ya Shilingi milioni 10 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya TPA mwaka huu.

 

Baadhi ya wakazi wa Kata ya Ndandalo walioshuhudia kutolewa kwa msaada huo walisema uwepo wa vitanda vya kujifungulia kwenye zahanati hiyo mpya iliyozinduliwa hivi karibuni na Mbio za Mwenge wa Uhuru ikiwa imejengwa kwa Shilingi milioni 150 kunawaondoa kwenye mashaka ya kutembea umbali mrefu kuwapeleka wajawazito hadi Hospitali ya Wilaya kwaajili ya huduma za uzazi ikiwemo kujifungua.

 

Sophia maarufu kwa jina la Mama Lucy mkazi wa Mtaa wa Kalumbulu katika kata ya Ndandalo alisema alisema katika ujauzito wake wa pili alilazimika kujifungua akiwa njiani kuelekea hospitali ya wilaya kwakuwa kwenye eno lao hakukuwa na kituo chochote cha kutolea huduma hiyo.

 

 “Tunashukuru kwa  kutuleteo kituo hiki, awali tulikuwa tunasumbuka kutoka hapa  mpaka twende mjini. Umbali ni mkubwa na kama ni mjamzito wakati mwingine anajifungulia njiani..mimi mwenyewe nimewahi kujifungulia njiani.” Alisema Sophia.

 

“Tunaomba kuletewa kwa zahanati hii na wafanyakazi tuletewe wawe wengi na dawa zipatikane. Siyo watuletee ikawa ni jumba tu  hakuna madawa… watuletee dawa, wahudumu wawepo wa kutuhudumia. Tunashukuru watu wa bandari wamekuja kutuona..waendelee hivyo hivyo na wasichoke tu kwetu waende na kwingine hospitali ni nyingi zinazofunguliwa.” Aliongeza.

 

Mkazi mwingine, Benard  Mwakipesile alisema kutolewa kwa msaada huo kunawafanya wakazi wa Kata ya Ndandalo kuwa na tabasamu akisema kupata vifaa vya kujifungulia wajawazito si jambo dogo kwakuwa linakwenda kuwaondolea adha waliyokabiliana nayo kwa miaka mingi ya kufuata huduma hizo mbali.

 

Mwakipesile alisema mara kadhaa walikuwa wakishuhudia Hopitali ya Wilaya ya Kyela ikikabiliwa na msongamano wa wagonjwa wakiwemo wajawazito hatua iliyopelekea baadhi yao kujifungua wakiwa bado kwenye foleni au njiani wanapopelekwa.

 

Naye Sekela Nkanda alisema sasa wakazi hao wanajiona wako sehemu salama kwakuwa wamepunguziwa mwendo wa kuifikia hospitali ya wilaya hivyo watapata huduma stahiki karibu na mazingira wanayoishi.

“Ilikuwa ni vigumu hata wajawazito au akina mama waliojifungua kuhudhuria kliniki jambo ambalo ni hatari. N a hapa tunaomba huduma ya wazazi iwe kipaumbele kwakuwa tunapata shida sana kwa watoto na wajawazito.” Alisema Sekela.

 

Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela kupokea msaada huo, Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Saumu Kumbisaga alikiri kuwepo na msongamano wa watu wanaohitaji huduma kwenye hospitali ya wilaya na kuwa kuongezewa nguvu kwa zahanati kama ya Ndandalo kwa kupewa vifaa muhimu kunaleta unafuu.

 

Dk Kumbisaga alisema hospitali ya wilaya imekuwa ikipokea jumla ya wagonjwa 350 kwa siku na wajawazito ambao wamekuwa wakijifungua hospitalini hapo ni kati ya nane hadi 12.

 

Alisema kupokelewa kwa vitanda hivyo na uwepo wa miundombinu bora ikiwemo vyumba vya kujifungulia kunaufanya uongozi wa wilaya hiyo kuja na wazo na kuifanya zahanati hiyo kuwa miongoni mwa zile nne zinazopaswa kupandishwa hadhi na kuwa vituo vya Afya kwakuwa huduma za kibingwa pia zitatolewa.

 

Awali akikabidhi msaada huo, Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Manga Gassayah alisema jamii ya watanzania ndiyo wateja wakuu wa Bandari kwakuwa ndiyo wananchi wanaozitumia kusafirisha mizigo yao.

 

Gassayay alisema katika kuadhimisha wiki ya Bandari TPA wamekuwa na desturi ya kushiriki shughuli za kijamii ikiwemo kutoa misaada kwa maeneo yanayoonekana kuwa na uhitaji.

 

“Tumeamua kutoa vitanda hivi kama njia ya kumuunga mkono rais, Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuboresha huduma za Afya kwa kujenga Hospitali, vituo vya Afya na Zahanati kwa lengo la kuhakikisha afya ya watanzania iko salama.” Alisema Gassayah.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post