PJT-MMMAM YACHOCHEA UFUATILIAJI AFYA ZA WAJAWAZITO CHUNYA

Wadau waliohudhuria Kikao cha Tathmini ya Robo ya Tatu ya Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) mkoa wa Mbeya wakifuatilia mawasilisho ya utekelezaji kutoka kwa maafisa maendeleo ya jamii ya kila halmashauri za mkoa huo .(Picha na Joachim Nyambo)

 

Na Joachim Nyambo, Mbeya.

UFUATILIAJI kwa wajawazito kupata vipimo vya msingi ili kuwezesha kujifungua watoto walio na Afya bora ni miongoni mwa matokeo chanya yaliyoanza kujitokeza wilayani Chunya mkoani Mbeya baada ya kuanza kutekelezwa kwa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) mkoani hapa.

Kwa mkoani Mbeya PJT-MMMAM ilizinduliwa rasmi Agosti 19 mwaka jana ikiwa ni sehemu ya mikoa 10 ya awali iliyoanza utekelezaji wa programu hiyo nchini na tayari matokeo katika baadhi ya maeneo yameanza kuonekana kwenye vipengele vitano vya Malezi Jumuishi ikiwemo Afya bora,Lishe bora,Ujifunzaji wa Awali,Malezi yenye Muitikio na Ulinzi na Usalama wa mtoto.

Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Programu hiyo kwenye Kikao cha Mkoa cha Tathmnini ya Robo ya Tatu ya PJT-MMMAM, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Chunya, Nasra Mkupete alisema awamu hii kumeonekana kuwepo na msukumo mkubwa kwa wajawazito kupima afya zao.

Mkupete alisema wadau kwa kushirikiana na vituo vya kutolea huduma wamelivalia njuga suala la wajawazito kupima afya zao kwa kuhakikisha jamii inapewa elimu, ukusanyaji wa taarifa za wajawazito wanaopata vipimo na pia ufuatiliaji wa mahudhurio yao ya kliniki.

Alisema kwenye suala la vipimo vya afya za wajawazito linalenga kubaini uwemo wa magonjwa yanayoweza kusababisha mtoto kukosa afya bora anapozaliwa ambapo alibainisha vipimo vinavyopewa kipaumbele kuwa ni pamoja na VVU,Kaswende, uwingi wa damu na Malaria.

Alisema malengo ya mpango huo kwa robo ya tatu ya utekelezaji wa PJT-MMMAM ilikuwa kuwafikia wajawazito wapatao 5,581 katika kipindi cha kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu malengo aliyosema yamefikiwa kama ilivyopangwa.

Alisema kwa kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu wajawazito waliopima Kaswende  walikuwa 5,581, VVU 5,399, uwingi wa damu ni 5,581 huku akisema wataalamu wa afya walipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa jamii.

Afisa huyo alisema shughuli nyingine iliyofanyika katika kipindi hicho ni kufanya mafunzo rejea juu ya dalili za hatari kwa vituo vyote 37 vinavyotoa huduma ya Mama na Mtoto wilayani Chunya.

Alisema lengo ilikuwa kufikia vituo 37 na mafanikio ni kuwa tayari walifanikiwa kufanya mafunzo rejea kwa wataalamu wa vituo 15 na juhudi zinaendelea ili kuvifikia vituo vyote.

“Shughuli nyingine iliyofanyika ni kufuatilia watoto wote waliozaliwa katika kipindi cha kati ya Aprili na Juni kuona iwapo walipata chanjo. Mafanikio  ni kuwa hadi sasa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano wote wamepata chanjo.”

“Tulijiwekea pia mikakati ya kutoa elimu ya lishe bora na pia utoaji wa uji wa lishe kwa watoto wa awali, darasa la kwanza na darasa la pili. Lengo ilikuwa kuhakikisha wanafunzi wa awali,darasa la kwanza na la pili kutoka katika shule 79 kwa robo ya nne kwa ngazi ya halimashauri wamepatiwa uji wa lishe. Tumefanikiwa kufikia shule 61 sawa na asilimia 77.2” aliongeza.

Awali akifungua Kikao hicho, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Joel Mwakapala alisema serikali inatamani matokeo chanya ya programu hiyo yanaanza kuonekana kuanzia kwenye familia za watendaji wanaoitekeleza kwakuwa mapungufu ya uwekezaji kwenye malezi na makuzi ya watoto kuanzia umri wa miaka sifuri hadi nane yanaonekana pia kwao.

Mwakapala alisema kwa matokeo chanya kuanza kuonekana kwenye familia zao na watu wao wa karibu itadhihirisha pia kuwa wanatekeleza jambo ambalo na wao wenyewe wanalielewa na hivyo hata kile wanachokifundisha kwa watu wengine kiko sahihi.

Naye Afisa Mawasiliano na Ushirikiano wa Mtandao wa Maendeleo ya awali ya mtoto nchini(TECDEN), Andrew Nkunga  alisisitiza umuhimu wa wadau yakiwemo mashirika binafsi kushirikishwa kwenye utekelezaji wa programu hiyo kwakuwa mchango wao unahitajika.

PJT-MMMAM iliyozinduliwa kitaifa mwaka juzi inalenga kusaidia kuratibu kwa kutekeleza kwa vitendo sheria na sera mbalimbali zinazohusiana na MMMAM ikiwemo Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009, Sera Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na Sheria ya Watu wenye Ulemavu ya 2010 kwa lengo la kushughulikia  mahitaji ya ukuaji na maendeleo ya watoto wenye umri wa miaka 0-8 na kuahikisha kuwa “Watoto wote Tanzaniawapo kwenye mwelekeo sahihi wa kufikia ukuaji timilifu”.

Baadhi ya wakazi waliopo kwenye maeneo ya pembezoni wilayani Chunya hususani zinakofanyika shughuli za uchimbaji madini, kilimo cha tumbaku na ufugaji wanasema nguvu kubwa ya utekelezaji wa PJT-MMMAM inapaswa kuelekezwa kwenye maeneo hayo kutokana na uhitaji uliopo.

Daudi Sichone mkazi wa kijiji cha  Itumbi kilichopo kata ya Matundasi alisema bado elimu ya uzazi salama inahitajika kwa kiasi kikubwa kwenye maeneo ya machimbo kutokana na asilimia kubwa ya wanajamii waliopo huko kutotoa huduma stahiki kwa wajawazito na watoto wachanga hususani huduma za chanjo.

Naye Samuel Lugano mkazi wa kijiji cha Sipa katika Kata ya Kambi Katoto alisema wakazi wa maeneo hayo wameanza kuonekana kupata uelewa wa masuala ya kuzingatia kliniki kwa wajawazito na watoto wachanga baada ya serikali kujenga kituo cha Afya kwenye Kata yao.

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post