ZAIDI YA SHILINGI MILIONI MBILI ZAKUSANYWA KUJENGA CHOO KATIKA SHULE YA MSINGI KILOLELI, WANANCHI WAHAMASIKA

Na Stela Paul

Wananchi wa kijiji cha Kiloleli Kata ya Kiloleli katika halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga wamefanikiwa kuanzisha ujenzi wa choo chenye matundu 24 na chumba kimoja cha kujisitili wanafunzi wa kike katika Shule ya Msingi Kiloleli.

 

Wakizungumza na waandishi wa habari jana wananchi wa kijiji hicho wamesema wamefanikiwa kuazisha ujenzi huo baada ya kituo cha taarifa na maarifa kuibua changamoto zinazoikabili shule hiyo na kuwahamasisha katika zoezi la uchangiaji.

Mmoja kati ya wananchi wa kijiji hicho Martha Ngwelu amesema wameanzisha ujenzi huo kutokana na upungufu wa matundu ya choo unaosababisha wanafunzi kujisaidia katika mazingira yasiyo rafiki.

“Wanakituo cha taarifa na maarifa walitupa hamasa baada ya kuibua changamoto hii na kuchangia mifuko mitano ya saruji pamoja na shilingi 50,000 ndipo na sisi wananchi tukaanza zoezi la kuchangia maana tulikuwa tunasema tu kwenye mikutano ya hadhara lakini kuchangia hamna, kwahiyo tunaomba serikali itushike mkono ili kukamlisha ujenzi huu” amesema Ngwelu

Kwa upande wake Mwanakituo cha taarifa na Maarifa namba 9 kata ya Kiloleli Helena Makelele amesema wameibua changamoto ya upungufu wa matundu ya choo katika Shule hiyo na kuwashirikisha wananchi kupitia Bunge la jamii na wananchi wakahamasika katika uchangiaji.

 “Tulikuwa na Bunge la jamiii tukawashirikisha wananchi jinsi watoto wetu wanavyohangaika, wanajamii waliitikia nguvu ya wananchi ikaanza kuchimba mashimo, sisi kama wanakituo cha taarifa na maarifa tulitoa shilingi 50, 000 na mifuko mitano ya saruji. Wananchi walituunga mkono wakaanza kuchangishana, walianza na mchango wa shilingi 1,000 na badae wakatoa mchango wa shilingi 2,000 mpaka tumefikia hatua hii” amesema Helena.

 

Joseph Solea ni mwana kituo cha taarifa na maarifa katika kijiji cha Kiloleli ameeleza namna walivyoibua changamoto ya upungufu wa matundu ya choo katika shule ya msingi Kiloleli na kuchukua hatua ya kuwashirikisha wananchi ili kuchukua jitihada mbalimbali kwaajili ya ujenzi wa choo kipya.

“Tuliangalia changamoto zinazozikumba taasisi mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, tukabaini changamoto kubwa ni upungufu wa matundu ya choo katika shule hii kwa sababu watoto wanahangaika wakati mwingine wanakwenda kujisaidia huko chini, tuliwashirikisha wanajamii kupitia vikao mbalimbali kisha tukaanza ujenzi huu”amesema Joseph.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Kiloleli Mwalimu Juliana Petro amesema shule hiyo inajumla ya wanafunzi 997 ambapo changamoto ya upungufu wa matundu ya choo inachangia msongamano wa wanafunzi chooni hivyo kuchangia wanafunzi kupitwa na vipindi vya masomo darasani.

“wanafunzi wanapokwenda chooni wanakuwa wengi kwa sababu ya kusubiriana kwahiyo inachukua muda mrefu na wanachelewa kurudi darasani, kukamilika kwa ujenzi huu kutaleta unafuu na kupunguza mlundikano wa wanafunzi chooni japo matundu bado hayatoshi” amesema Mwalimu Juliana.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Kuhwema Mashara amesema kuanza kwa ujenzi huo imetokana na michango ilitokusanywa kutoka sehemu mbnalimbali ikiwemo kituo cha taarifa na maarifa, wananchi, serikali ya kijiji na Kamati ya maendeleo ya kata WARDC.

“walianza kituo cha taarifa na maarifa wakachangia, wananchi wakakubaliana tukachangia shilingi 2,000 tukanunua nondo na saruji na kujenga bampa ,WARDC ikanipa mifuko 30 ya saruji, kwenye serikali yetu ya kijiji nikatoa shilingi 600,000” amesema Mashara.

Mtendaji wa Kijiji hicho Nicholaus Mzirai amesema mpaka kufikia sasa wamefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Milioni 2,500,000 ambapo ujenzi umefikia kwenye hatua ya lenta.

“Kupitia vikao mbalimbali tulivyozungumza hapo awali na mpaka sasa jumla ya michango tuliyofanikiwa kukusanya ni shilingi milioni 2,500,000 na ujenzi umefikia kwenye hatua ya kupigwa lenta” amesema Mzirai.

Kuanza kwa ujenzi huo ni baada ya wanakituo cha taarifa na maarifa waliojengewa uwezo wa ulagabishi na Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP kuibua changamoto katika taasisi mbalimbali ikiwemo Shule ya Msingi Kiloleli na kuhamasisha wananchi kuanza kuchangia shughuli za maendeleo.

Muonekano wa choo cha zamani.Muonekano wa matundu ya choo ambayo yanajengwa na kituo cha Tarifa na Maarifa kutoka Kata ya Kiloleli wilayani Kishapu.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post