SMAUJATA SHINYANGA WAFANYA KONGAMANO LA KUPINGA UKATILI JAMII YAHIMIZWA KUTOA TAARIFA "PIGA SIMU 116"

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mwenyekiti wa kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bi. Nabila Kisendi ameiomba jamii kukemea vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ya videndo hivyo ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Ametoa ombo hilo katika kongamano la kupinga ukatili ambalo limefanyika katika uwanja wa zima moto Nguzonane na kwamba limeratibiwa na kampeni hiyo na kuhudhuriwa na viogozi wa serikali, dini, chama na wadau mbalimbali Mkoa wa Shinyanga.

Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bi. Nabila Kisendi jina maarufu Madam Kisendi amesisitiza wananchi wote wakiwemo watoto na wanawake kuungana kwa pamoja kupinga vitendo vya ukatili vinavyoendelea katika Mkoa wa Shinyanga ili kuendeleza amani Nchini.

Aidha Mwenyekiti Madam Kisendi ametaja malengo ya SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga kuwa ni pamoja na kuhakikisha wanatoa elimu ya kupinga ukatili kwenye jamii, Kuwatambua na kuwapongeza mashujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii, Kufikisha jumbe mbalimbali za Wizara na serikali kwa ujumla kwenye jamii kupitia njia za utoaji elimu, ushirikishwaji wa wananchi kupitia makongamano kama hili na Kujenga moyo wa uzalendo kwa watanzania, kujitoa katika mambo ambayo yanahitaji umoja wa kijamii ili kuleta matokeo ya haraka katika jamii zetu.

Madam Kisendi ametaja baadhi ya changamoto zinazokwamisha kufikia malengo ikiwemo ukosefu wa ofisi kwa ajili ya kutunza taarifa mbalimbali,ukosefu wa usafiri kwa ajili ya kufika sehemu kutoa elimu pamoja na Ushirikiano mdogo kwa viongozi ngazi za chini.

Amesema licha ya jitihada zinazo fanywa na serikali,taasisi binafsi na wadau mbalimbali wanatakiwa kutoa ushirikiano ili kufanikisha kutokomeza vitendo vya ukatili katika jamii kwa kutoa taarifa za viashiria vya matukio hayo.

 

Ametumia nafasi hiyo pia kumpongeza afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Shinyanga Bi. Lydia Kwesigabo pamoja na Afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Shinyanga Bwana Tedson Ngwale kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa majukumu.

Akizungumza mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, mtendaji talafa ya Shinyanga mjini Bwana Mathias Masalu amesema atahakikisha changamoto zinazoikwamisha SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga anazifikisha sehemu husika kwa ajili ya utekelezaji wake ikiwemo ukosefu wa ofisi pamoja na usafiri ili kuifikia jamii kwa uharaka.

Amesema kuwa SMAUJATA pamoja na wadau wengine wanatakiwa kuendelea kujituma kutekeleza majukumu yao licha ya changamoto hizo zinazowakabili.

Wakati huo huo Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Shinyanga Bi. Sophia Kang’ombe  pamoja na baadhi ya wadau waliohudhuria kongamano hilo wameisihi jamii kuacha vitendo vya ukatili.

Kampeni ya SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga imefanya kongamano la kupinga ukatili ambalo limeambatana na maandamano na kwamba limehudhuriwa na viongozi pamoja na wadau wakiwemo wanachuo na wanafunzi wa shule mbalimbali ikiwemo shule ya msingi Town, Mwenge pamoja na shule ya sekondari Ndala Manispaa ya Shinyanga.










This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post