Sintofahamu yaibuka AtoZ, ikianza kutiririsha maji bomba la Auwsa

 *Wananchi wasema maji ni salama na wanayatumia kulimia mbogamboga 

*Wahofia kuathirika na ukame, waomba uongozi uendelee kuyatiririshia mtoni

Sehemu ya mazao yanayonyeshewa maji yanayotiririka kutoka ndani ya kiwanda Cha AtoZ, Kisongo

Mfugaji akielekea kukata majani yaliyomea pembezoni mwa mto unaotiririsha maji yanayotoka ndani ya kiwanda Cha AtoZ baada ya kusafishwa na kuachiwa

Na Mwandishi Wetu, Arusha

SINTOFAHAMU imeibuka miongoni mwa wakazi ambao wanatumia maji yanayotiririka kutoka katika  kiwanda maarufu Cha  kutengeneza nguo na Chandarua chenye dawa ya kuua Mbu, cha A to Z  baada ya kiwanda hicho kukamilisha mtambo wa kusafisha maji machafu na hivyo kuanza kuyaingiza katika Bomba la maji taka la Mamlaka ya Maji Safi na Taka Arusha(Auwsa).


Wakazi hao ambao wengi wao wamekuwa wakitumia maji hayo kunyeshea mazao mbalimbali ikiwemo mahindi, maharagwe na mbogamboga wamedai endapo AtoZ itazuia maji hayo, wataathirika sana kwa kuwa wamekuwa wakitumia maji hayo kujipatia kipato na chakula kutokana na mazao wanayopanda.


Mzee ISSA Mtaro ni miongoni mwa wafaidikaji wa maji hayo ambaye anasema kwa zaidi ya miaka kumi amekuwa akitumia maji hayo, hivyo endapo yatazuiwa atakuwa ni miongoni mwa wahanga wakubwa.


Anasema pamoja na kwamba eneo la kisongo ni kame, kwa upande wake mwaka mzima amekuwa akiendesha kilimo Cha mazao mbalimbali kwa kutulia maji hayo kumwagilia mazao yake na kujipatia kipato Cha kuendesha familia na kuhudumia mahitaji mengine.


" Kwa kweli haya maji licha ya kulalamikiwa na baadhi ya watu, ambao wanadai ni machafu, Mimi yamekuwa msaada mkubwa kwangu, namwagilia mahindi, mboga mboga, kama mnavyoona hapa, Kuna ukame lakini mahindi na mbogamboga zote ni kijani, nawashangaa sana wanaolalamika eti maji ni machafu," anasema.


Kwa upande wake James Laizer , mkazi mwingine wa eneo linalozunguka kiwanda Cha AtoZ anasema maji yanayodaiwa kuwa machafu ni uongo kwa kuwa yeye ni mnufaikaji wa maji hayo ambayo pia amekuwa akitumia kumwagilia bustani yake ya majani nyumbani na migomba.


Anasema amekuwa akisikia Kuna watu wameathiriwa na Maji hayo lakini hajawahi kushuhudia watu hao na Wala yeye hajawahi athirika nayo jambo ambalo anahisi kuwa ni propaganda ambazo zimekuwa zikifanywa na watu wasiokuwa na mapenzi mema na kiwanda hicho.


Hata hivyo wananchi hao wanauomba uongozi wa kiwanda cha AtoZ kutoingiza maji yote kwenye mfumo wa Auwsa na kuruhusu sehemu ya maji kutiririka katika mkondo wa mto ili waendelee kufaidika na Maji hayo.


Akitoa taarifa kwa Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt Selemani Jaffo aliyetembelea kiwanda hicho machi3 mwaka huu, 2023, Meneja Usalama na Mazingira, Mhandisi Harrison Rwehumbiza alimweleza Waziri kuwa mtambo huo umeshakamilika kwa asilimia98 na kinachosubiriwa ni hatua ya Auwsa kufikisha Bomba lake na kuanza kupokea maji hayo.


Mbogamboga zinazolimwa kwa kutumia maji yanayotiririka kutoka ndani ya kiwanda Cha AtoZ

Amesema maji yanayotiririshwa kupitia mfumo huo ni salama kwa matumizi ya Binaadam kwaajili ya kunyeshea bustani na kwamba Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kupitia ofisi yake ya Kanda,  imethibitisha ubora wake na imekuwa ikichukua vipimo mara kwa mara ili Kuendelea kujiridhisha.


Waziri Dkt Selemani Jaffo alipongeza Menejimenti ya AtoZ kwa kuonyesha inajali afya za wakazi wanaozunguka kiwanda hicho baada ya kutii agizo la Serikali lililoagiza uongozi kujenga mtambo huo wa kuchakata maji machafu licha ya kuwa ni gharama kubwa.


Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt Selemani Jaffo ( mwenye suti ya blue nyeusi),  akisikiliza jambo kutoka kwa Meneja Usalama na Mazingira wa kiwanda Cha AtoZ Mhandisi Harrison Rwehumbiza, mara baada ya waziri Jaffo kutembelea kiwanda hicho kukagua mtambo wa kusafisha maji taka.

Waziri Jaffo alisema pamoja na kwamba Serikali imekuwa ikifaidika na wawekezaji, kwa kulipa Kodi kubwa na kutoa ajira kwa watanzania, lakini afya za wananchi ni jambo la kwanza kuangaliwa," Hongereni sana AtoZ, hili ndio Serikali tunalolitaka, uwekezaji uende sambamba na kujali afya za watu,".


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post