MBUNGE KUTUMIA 480 MILIONI KUJENGA OFISI ZA CCM

 

NA  VICTOR MAKINDA: IGUNGA

Mbunge wa jimbo la Igunga mkoani Tabora, Nicholas Ngassa, anatarajia kutumia kiasi cha Shilingi 480 Milioni, kwa ajili ujenzi wa ofisi za kata za Chama Cha Mapinduzi  (CCM) kwenye kata 16 za jimbo hilo.

 Ngassa aliyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi ramani ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) pamoja na matofali 1000 na mifuko ya sementi 100 wilayani Igunga jana.

“Moja ya ahadi niliyoitoa kwa wanachama wa  CCM jimbo la Iigunga wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ni kujenga ofisi za chama kwenye kata zote 16 jimbo la Igunga kwa fedha zangu binafsi.” Alisema.

 Ngassa aliongeza kusema kuwa mpango huo wa ujenzi wa ofisi hizo upo tayari na unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni huku matarajio yakiwa ni kukamilisha ujenzi huo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

 “ CCM ni chama kikongwe na ni chama kikubwa kinachoaminiwa, kupendwa na kutegemewa na mamilioni ya watanzania. Ni lazima kiwe na miundombinu wezeshi itakayo warahisishia watendaji wake kufanya kazi kwa ufanisi”. Alisema Ngassa.

 Ngasa alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa chama hicho kuendelea kujijenga kuanzia ngazi za chini, na kwa mapenzi makubwa aliyonayo kwa chama chake,  ameamua kutumia fedha zake binfsi zinazotokana na mshahara wake na vyanzo vyake  vingine vya mapato,  kuhakikisha kuwa kata zote za jimbo hilo zinakuwa na ofisi ambazo zitakuwa na sehemu ya  ukumbi wa mikutano na vyumba vitatu vya biashara.

“ Lengo sio kuwa tu na ofisi, bali ni kuwa na chanzo cha mapato cha uhakika kwa jumuiya za chama. Ofisi za kata ninazotarajia kuanza ujenzi wake hivi karibuni,  zitakuwa pia na vyumba vitatu vya biashara vitakavyotumika kwa shughuli za ujasiriamali ili pato litokanalo  liweze kusaidia ustawi wa jumuiya za chama ikiwa ni Jumuiya ya Vijana (UVCCM) Jumuiya ya Wazazi na Umoja wa wanawake (UWT).” Alisema Ngasa,

Katika hatua nyingine ya kuwawezesha watendaji wa  CCM  jimbo hilo kufanya kazi  kwa ufanisi, Ngassa alisema kuwa anatarajia kuwanunulia baiskeli makatibu wa matawi wote, pikikpiki kwa makatibu kata wote wa chama hicho jimboni Igunga.

“ Kazi ya makatibu wa Kata na matawi ni kubwa, natambua kuwa usafiri ni kikwazo kwao kuwafikia wanachama kwa haraka, moja ya mipango yangu ni kuwanunulia baiskeli na pikipiki ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi kuendana na kasi ya siasa za wakati huu”. Alisema.


Katibu wa CCM wa kata ya Mwamakona jimboni Igunga, Robert Madutu, alisema kuwa ujenzi wa ofisi hizo na vyombo vya usafiri  wanavyotarajiwa kupewa na Mbunge wao utawaongezea  ufanisi wa kazi ya uenezi wa chama hicho.

 Akizungumza kuhusu utekelezaji wa ahadi ya  Mbunge huyo  kwa ustawi wa chama, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Igunga, Mafunda Temanywa, alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi wilaya hiyo kimefarijika kuona kuwa kuna mwanachama mwenye moyo wa kujitolea katika kukijenga na kukiimarisha.

“Ninaamini kilichomsukuma mbunge wetu kujenga ofisi za chama ni uzalendo wake, dhamira yake na mapenzi yake mema kwa chama CCM, hivyo  ninatoa wito kwa wanachama wengine kuwa tayari kujitoa kwa hali na mali katika kukijenga CCM.”  Alisema Mafunda.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post