TIC yakaribisha wawekezaji maonyesho ya Nane nane, wapo tayari kuwahudumia

Kutoka kushoto: Bi Olga Komeka (Afisa utumishi), Bw. Revocatus Rasheli (kaimu mkurugenzi wa uhamasishaji uwekezaji), Bw. Daudi Riganda (Meneja Kanda ya Kaskazi) na Bw. Godfrey Gowele wakitoa huduma katika banda la TIC katika viwanja vya Njiro Arusha

 Na Seif Mangwangi, Arusha


Kituo cha uwekezaji nchini (TIC), kimewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kufika kwenye banda la kituo hicho lililopo kwenye maonyesho ya kilimo nane nane katika kanda tofauti nchini ili kupata fursa ya taarifa za uwekezaji  hususani maeneo yaliyotengwa kwa uwekezaji.


Kaimu Mkurugenzi wa TIC,  Revocatus Rashel amesema hivi sasa kituo hicho kinatekeleza mpango mkakati wa miaka mitano ambao moja ya malengo yake ni kutoa fursa kwenye maeneo yenye masoko na yanayozalisha kwa wingi.


" Tumetengeneza utaratibu wa kuratibu taarifa za fursa zote zinazopatikana kwenye maeneo mbalimbali nchini na kuziweka kwenye tovuti na kukaribisha wawekezaji wengi zaidi, ikiwemo sekta ya madini, tunataka watu waje wanunue, kwa kuwaonyesha maeneo yanayopatikana na kwa ubora gani,"amesema na kuongeza:

" tunajua watanzania wengi wako huko pembezoni wakijishughulisha na kilimo, ufugaji, uvuvi, sekta ya misitu na tunachofanya ni kutangaza maeneo hayo ili wapate wawekezaji, tuweze kutengeneza ajira,"amesema.


Bw. Revocatus Rasheli (Kaimu mkurugenzi wa uhamasishaji uwekezaji) akifanya mahojiano na baadhi ya waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa TIC katika kuhamasisha uwekezaji kupitia maonesho mbalimbali


Amesema kituo hicho kimekuwa kikisaidia wajasiriamali wadogo kwa kuwajengea uwezo kwa kuwapatia mafunzo na baadae kuwaunganisha na taasisi zingine za kupata huduma mfano  kupata vibali vya taasisi ya ubora  TBS au mabenki ili wapate mikopo na  baadae kuwa wawekezaji wakubwa.


Amekaribisha watanzania wenye ardhi nzuri inayofaa kwa uwekezaji kufikisha taarifa zao katika kituo hicho ili waweze kusaidiwa kupatikana kwa uwekezaji na kufaidika na kituo hicho.


Kwa upande wake Meneja wa kituo hicho  kanda ya Kaskazini, Daudi Riganda amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja kituo hicho kimefanikiwa  kusajili miradi 30 ya uwekezaji huku sekta ya viwanda akitaja kuwa kinara dhidi ya sekta zingine.


Akizungumza na mwandishi wetu katika banda la Nane nane Njiro Jijini Arusha, Riganda asema kupitia miradi hiyo jumla ya  ajira 2661 zinatarajiwa kupatikana kupitia uwekezaji huo na kusaidia kupunguza tatizo la ajira nchini na kwamba sekta ya viwanda ndio iliyofanya vizuri zaidi.


Riganda amesema miradi hiyo ni sawa na  uwekezaji wa Dola za Marekani USD 135.38 mil, ambapo miradi hiyo imegawanyika kwa sekta ya viwanda miradi 14 utalii 9,  sekta ya kilimo 4 na miradi miwili ni kuhusu usafirishaji na miradi mmoja ni katika sekta ya kutoa huduma.


"Mkoa wa Arusha ndio unaoongoza kwa kupokea wawekezaji wengi zaidi nchini,jumla ya miradi 13 imetoka Arusha, ukifuatiwa na Mkoa wa Tanga kwa miradi 9 na mkoa wa manyara miradi 5 na  Mkoa wa Kilimanjaro miradi 3, uwekezaji sekta ya viwanda ndio inaonekana kukimbiliwa sana," amesema.


Amesema Mikoa ya kanda ya kaskazini imejaaliwa kuwa na sekta nyingi za uwekezaji nchini kuliko mikoa mingine huku akitaja sekta ya utalii kuwa kinara ambapo wawekezaji wanaweza kujenga hoteli pembezoni mwa hifadhi mbalimbali zinazopatikana kaskazini au kuanzisha kampuni za utalii.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post