KINACHOFANYIKA LOLIONDO NI UVUNJAJI WA SHERIA: Ole Ngurumwa

Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela akishiriki zoezi la kuweka alama katika eneo la Kilometa 1500 Loliondo

 

Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro

WAKILI MAARUFU nchini na Mkurugenzi wa Kituo cha utetezi wa Haki za binaadam (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema zoezi linaloendeshwa na Serikali kuweka mipaka kwenye eneo la ardhi ya vijiji vya tarafa za Sale na Loliondo Wilayani Ngorongoro ni uvunjaji wa sheria na ukiukwaji wa haki za binaadam.


Ole Ngurumwa ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ololosokwan amesema mtafaruku baina ya askari wanaosimamia zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika eneo la ardhi ya vijiji na wananchi wa maeneo hayo na kupelekea kuuawa kwa askari mmoja siyo takwa la kisheria.


Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo amekiri kuuawa kwa askari mmoja aliyekuwa kwenye zoezi la kusimamia kikosi kinachoweka alama katika eneo hilo kwa kupigwa mshale na wakazi wa eneo hilo.


Hata hivyo pamoja na vurugu hizo zilizopelekea kifo cha askari huyo ambaye hadi sasa jina na cheo chake hakijatambuliwa bado alisisitiza kuwa hali ni shwari na kwamba zoezi la kuweka alama katika eneo la kilometa za mraba 1500 linaendelea vizuri.


Wakili Olengurumwa amesema“ Kinachoonekana kwa sasa ni kuwa serikali inakwepa kuanzisha mchakato wowote wa kisheria kwa kuwashirikisha wananchi iwapo wanahitaji eneo hilo la kilometa za mraba 1,500. Wanatambua kuwa kuchukua hilo eneo la vijiji kwa utaratibu wanaotumia sasa wa kusema tunawagawia ardhi kilometa za mraba 2,500 kutoka kwenye kilometa za mraba 4000 hakutakuwa na gharama zozote za fidia.”


Anasema wanachosisitiza wananchi wa Loliondo ni kuondoa vikosi vilivyopo vya jeshi la polisi na kukaa kwenye meza ya majadiliano ili kutoa nafasi ya kutatua mgogoro huo na kutoa ushauri kwa Serikali chini ya uongozi wa Mama Samia kuhusu namna ya kuhifadhi maeneo ya Loliondo na kwamba michakato hiyo izingatie haki za binadamu na ushirikishwaji mpana wa wananchi ambao ni wakazi wa maeneo hayo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakiwa mafichoni, wakazi wa vijiji vinavyozunguka eneo hilo wamedai kuingiwa na hofu baada ya Serikali kupeleka askari katika eneo hilo na kuliendesha kwa nguvu bila ya wao kushirikishwa.


Wanasema idadi kubwa ya wananchi wamekimbia maboma yao na kukimbilia nchi jirani ya Kenya baada ya askari kuvamia kwenye makazi yao na kuwapiga huku wakipiga mabomu ya machozi.


Akitoa taarifa ya zoezi hilo kwa waandishi wa habari juzi akiwa Loliondo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella alisema kuwa zoezi hilo linaendelea vizuri bila tatizo lolote licha ya kutokea  mauaji ya askari mmoja yaliyofanywa na wananchi.


Alisema askari huyo aliuawa kwa kupigwa mshale katika zoezi hilo na kwamba jeshi la Polisi linaendelea kutafuta mtu aliyesababisha mauaji hayo.


Rc Mongela alisema nia ya Serikali ni njema  na haifanya jambo hilo kwaajili ya kuwaumiza wananchi bali inafanya kwaajili ya vizazi vijavyo kwa kuwa eneo la Loliondo ndio yalipo mazalia ya wanyamapori lakini ndio eneo lenye ekolojia inayotunza mazingira katika eneo la hifadhi ya Serengeti.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post