KAMPUNI YA OBC YAHUSISHWA MGOGORO WA LOLIONDO

Kina Mama wa Kimaasai wakiwa wamepiga picha na bango linaloonyesha kutomtaka mwekezaji kampuni ya OBC, picha hii ilipigwa Septemba 15, 2011 katika tamasha la jinsia, kwenye viwanja vya TGNP Jijini Dar es salaam. Mwekezaji OBC amekuwa na mgogoro wa muda mrefu na wakazi wa eneo hilo ambao ni wamaasai jamii ya wafugaji. (Picha ya mtandao)

 Na Mwandishi Wetu, Loliondo

WANANCHI katika vijiji vinavyozunguka eneo la pori tengefu la Loliondo wamedai zoezi linalofanywa na Serikali la kumega ardhi yao kilometa za mraba 1500 linatokana na shinikizo la kampuni ya utalii ya Ortelo Business Cooperation (OBC) inayowekeza katika eneo hilo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema tangu mwaka 1992 wamekuwa na mgogoro mkubwa na kampuni hiyo ya kiarabu ya OBC kutokana na nia ya kampuni hiyo kutaka kuchukua eneo hilo kw aajili ya shughuli zake za uwindaji.


Kampuni ya Ortelo Business Cooperation Ltd (OBC), inamilikiwa na familia ya mfalme wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), imekuwa ikiwekeza Loliondo kwa zaidi ya miaka 30 sasa huku ikiendesha shughuli za uwindaji pamoja na utalii.


Mwenyekiti wa kijiji cha Arash, Kiaro Orminis anasema Serikali inachokifanya ni kutaka kuhalalisha eneo hilo kwa mwekezaji huyo ambaye kwa miaka mingi amekuwa akishindwa kufikia makubaliano na vijiji vinavyozunguka eneo hilo la uwekezaji na badala yake kumekuwepo na migogoro isiyoisha.


Onesmo Ole Ngurumwa, Mkurugenzi wa THRDC na ambaye pia ni mwananchi wa kijiji cha Ololosokwani anasema awali eneo lote la Loliondo lilijulikana kama pori tengefu la wanyamapori, lakini lilikuja kubadilishwa na sheria mpya ya wanyamapori iliyotungwa mwaka 2009 ambayo pia ilifuta sheria ya uhifadhi  wanyamapori ya mwaka 1974.


“Mabadiliko ya sheria ya Wanyamapori yalibadili hadhi ya mapori tengefu na kuondoa shughuli zote za kibinadamu kama ilivyokuwa awali. Sheria hii imepiga marufuku shughuli zote za kibinadamu katika maeneo ya mapori tengefu ambayo kimsingi yalikuwa yamepachikwa katika ardhi za Vijiji kwa kuwa lengo lake lilikuwa ni kusimamia rasilimali za wanyamapori na sio milki ya ardhi,”anasema Ole Ngurumwa na kuongeza:

 “ Bahati mbaya zoezi hili kwa upande wa Loliondo halikufanyika kama sheria ilivyoagiza, badala yake kumekuwemo na maneno mengi kuwa bado Loliondo nzima ni pori tengefu  kinyume na utaratibu wa sasa wa kisheria ambao hauruhusu pori tengefu  kuchangamana na shughuli za kibadamu,”. 


Hata hivyo anasema baada ya miaka ya 1990 makampuni binafsi kushamiri katika sekta ya  utalii wa uwindaji, kampuni ya Ortello Business Cooperation Ltd ilipewa eneo lote la Loliondo la Kilometa za mraba 4000 la vijiji vya Loliondo na Sale.


Anasema baada ya kampuni hiyo kupewa eneo hilo migogoro mingi ilizuka baina ya kampuni hiyo, wananchi na watumiaji wengine wa ardhi  ya vijiji kama makampuni mengine yanayofanya shughuli ya utalii  eneo hilo kabla ya kutungwa kwa sheria mpya ya wanyamapori ya 2009 iliyoondoa maeneo ya pori tengefu kuwepo kwenye ardhi ya vijiji.


Kwa upande wake Isaya Ole Naing’iria anasema baada ya kampuni hiyo ya OBC kushindwa kupokonya ardhi ya vijiji, ilikubali kukaa meza moja na vijiji vinavyozunguka eneo inalolitumia kufanyia shughuli zake na kuvilipa vijiji hivyo fedha kama sehemu ya kodi ya uwekezaji kutokana na matumizi ya eneo hilo.


“Hata hivyo wananchi tuliamua kuachana na mwekezaji huyu kutokana na mgogoro wa mara kwa mara wa malisho, alikuwa akizuia mifugo yetu isikaribie eneo la kunyweshea maji lakini pia eneo la malisho hasa wakati wa ukame na hivyo tukaamua kuachana nae. Miaka yote hii hakukubali kuondoka aliendelea kutumia eneo hili kwa mabavu huku akisaidiwa na askari,”anasema.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Ololosokwani Keri Dukunyi anasema wao kama vijiji hawaitaki kampuni ya OBC lakini inachoonekana ni Serikali kushinikiza mwekezaji huyo aendelee kuwepo kwenye eneo hilo kwa kuwa anaipatia fedha nyingi.


Anasema pamoja na kutoomtaka mwekezaji huyo, vijiji vilikuwa vikiendelea kupata pesa kutoka kwenye kampuni zingine za utalii ambazo zimekuwa zikifuata masharti ya vijiji hivyo hivyo serikali kupokonya eneo la kilometa za mraba 1500 ni kuwafanya kuwa maskini kwa kuwa hawatapata tena fedha hizo.


Hata hivyo pamoja na madai hayo ya wananchi, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa inatenga eneo hilo kwa ajili ya kulinda mazalia ya Wanyamapori, mapitio na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi kwa manufaa ya Wananchi wenyewe na Taifa kwa Ujumla.


Alama ambayo itatumika kama ukingo wa eneo ambalo ni sehemu ya kilometa 1500 zinazotengwa kwaajili ya uhifadhi

Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela akizungumza wakati wa kuaga mwili wa askari anayedaiwa kupigwa mshale katika zoezi hilo. Mwili huo wa Koplo Garlus Mwita ulisafirishwa kwenda Mara kwaajili ya Mazishi


Aidha Serikali imekanusha kuwaondoa wananchi hao kwa lengo la kumpatia mwekezaji yeyote eneo hilo bali zoezi hilo lina nia ya kuhakikisha usimamizi endelevu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ngorongoro na Pori Tengefu la Loliondo kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mkurugenzi wa OBC Issack Mollel alipotafutwa kuweza kuzungumzia kauli ya wananchi hao kuhusu kudaiwa kujihusisha na mgogoro huo hakuweza kupatikana na hata jitihada za kufika ofisini kwake zilizoko uzunguni Jijini Arusha kwaajili ya kuonana nae, ziligonga mwamba baada ya kukuta lango kuu la kuingilia ofisini kwake kufungwa na hakukuwa na mtu yoyote wa kufungua.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post