WANAFUNZI WENYE UHITAJI WAENDELEA VIZURI NA MASOMO, WAISHUKURU JIJI.

Baadhi ya vifaa vya shule vilivyotolewa na wadau wa Maendeleo Jiji la Arusha kwa wanafunzi wahitaji wa kidato cha kwanza kutoka shule mbalimbali za Sekondari za Jijini Arusha.
Wanafunzi wakipokea msaada huo.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt John Pima

 

Na Zulfa Mfinanga, Arusha.


Wanafunzi waliopata msaada wa vifaa vya shule ikiwemo sare za shule wanaosoma katika shule mbalimbali za sekondari za Jiji la Arusha wamewashukuru wadau waliofanikisha msaada huo uliowasaidia kuanza masomo yao ya kidato cha kwanza mwaka huu.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti walipotembelewa na waandishi wa habari katika shule zao, wanafunzi wao wamesema awali baada ya matokeo mazuri ya darasa la saba na kisha  kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, walikata tamaa ya kuendelea na masomo yao kutokana na hali ya kiuchumi walizonazo katika familia zao.


Victor Faustine mwenye ulemavu wa kuongea na kusikia, mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Themi amesema msaada huo ni mkombozi mkubwa sana kwake kwani umemsaidia kuwepo shuleni hadi sasa kwa kuwa hakuwa na sare ya shule wala vifaa vya shule jambo ambalo lililopelekea kukata tamaa ya kusoma.


“Awali nilifurahi sana kusikia nimefaulu mtihani wa Taifa wa darasa la saba na baadaye  kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, lakini ndoto zangu zilianza kufifia kila nikiangalia familia yangu nauwezo tulionao, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuongoza Mkurugenzi pamoja na wadau kulete huu msaada, mimi nawaahidi kusoma kwa bidii” Alisem Victor ambaye alikuwa alitafsiriwa na mwalimu Agnes.


Kwa upande wa wanafunzi Neema Evarest na Verynice Aggrey wa shule ya sekondari Arusha Day licha ya kuwashukuru wadau hao kwa kuwawezesha kuendelea na msomo lakini pia msaada huo umewafanya kuona na wana thamani na kuahidi kuja kutoa msaada kwa wahitaji hapo baadaye kama walivyosaidiwa.


Ibrahim Swai na Shozmina Sudi wa shule ya sekondari Arusha (Arusha Sec) pamoja na Melia Didasi wa shule ya sekondari Themi wameahidi kujituma zaidi katika masomo yao ili kutowakatisha tamaa wadau pamoja na wazazi wao na kuhakikisha wanatimiza malengo yao.


Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. John Pima amewapongeza wanafunzi hao kwa kuendelea kufanya vizuri katika masomo yao na kusema kujituma katika masomo ikiwa ni pamoja kutunza mali za shule, kuipenda nchi yao pamoja na kuwatii na kuwapenda wazazi ni uzalendo ambao utawasaidia kutimiza malengo yao.


Dkt Pima amesema mwezi Januari mwaka huu halmashari ya jiji la Arusha kwa kushirikiana na baraza madiwani, ofisi ya Mkuu wa wilaya pamoja na wadau wa maendeleo kutoka Jiji hilo waliwapatia msaada wa vifaa vya shule pamoja na sare za shule wanafunzi 413  wenye uhitaji waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na kushindwa kuripoti shuleni kutokana na changamoto ya kiuchumi inayowakabili.


Amesema wanafunzi hao walisaidiwa sare pamoja na vifaa vya shule  vikiwemo suruali, sketi, mashati, soksi, viatu, kalamu, penseli, madaftari pamoja na taulo za kike ambapo Dkt Pima amesema msaada huo ulilenga kuhakikisha hakuna wanafunzi anashindwa kuanza masomo yake kwa sababu ya kukosa mahitaji.


“Tulifanya hivyo ili kuhakikisha kuwa azma ya Rais Samia inatimizwa ya kuinua sekta ya elimu Jiji la Arusha kwani alituletea shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 100 na madawati 5250, na vyote vimeshakamilika na kuanza kutumika, na sisi tukaona tuna wajibu wa kumuunga mkono Rais wetu kwa kuwasaidia watoto wenye mahitaji kama hawa” Alisema Dkt Pima.


Aidha amewataka wazazi na walezi ambao watoto wao wamepata msaada huo kuhakikisha kuwa wanajipanga kwa ajili ya mhula wa pili wa masomo ili watoto wasikae majumbani kwa kukosa vifaa vya shule wakisubiri msaada kama wa awali kwani ni wajibu wao kuhakikisha watoto wanaendelea na masoma hata wasipopata msaada wowote. 


“Naomba wazazi ambao watoto wao walisaidiwa mhula wa kwanza wajitahidi kwenye mhula wa pili kwani unaposhikwa nawe shikamana, wasisubiri kusaidia tu, kwani tulifanya hivyo ili kuwakwamua katika hali ngumu katika mhula wa kwanza, kama akitokea mdau ni bahati nzuri lakini asipotokea bado mtoto anatakiwa aendelee na somo yake, tunataka kila mmoja anawajibika kama mzazi au mlezi”


Aidha Dkt. Pima ameendelea kuwashukuru wadau hao na wengine wanaoendelea kujitokeza kwa ajili ya kutoa masaada kwa wanafunzi hao ili kuhakikisha wanaendelea na masomo yao na kwamba anatamani kuona ndani ya Jiji la Arusha kila mwananfunzi mwenye sifa ya kusoma anapata elimu ili kujenga Taifa linalojitambua.


“Nawaomba wale ambao wanaguswa na jambo hili wafike ofisi ya Mkurugenzi akiwa na chochote alichonacho, sisi tunapokea kuanzia rula, kompasi na kuendelea, mwananchi yeyote ajisikie kuleta chochote alichonacho ambacho kitabadilisha maisha ya mtoto na kuleta upendo na furaha kwa watoto hao” Alisema Dkt Pima.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post