Na Mwandishi Wetu,Arusha
Halmashauri ya Jiji la Arusha imetoa kiasi cha Milioni 81 kwa ajili ya kuwapa motisha walimu zaidi ya 200 ambao walifaulisha masomo yao kwa kipindi cha mwaka 2020 2021 ,pamoja na wanafunzi ambao walifanya vema
Akikabidhi fedha pamoja na zawadi kwa walimu hao mapema jana kwenye viwanja vya Ngarenaro mkurugenzi wa jiji la Arusha, Dkt Pima alisema kuwa wameamua kutoa motisha ili kuendelea kufuta ziro.
Alisema kuwa fedha hizo zina baraka ya baraza la madiwani na wao pia wame bariki kufanyika kwa zoezi hilo ambapo wamedai ni moja ya njia ya kuipandisha halmashauri kiufaulu
"Tuna walimu zaidi ya 200 hapa na hawa walimu wanaopata zawadi leo ni wale wa shule za sekondari,msingi,shule binafsi kwa upande wa msingi lakini na wanafunzi bora
Hawa walimu wamegaeanyika katika makundi makundi kuna ambao shule zao zilifanikiwa kufuta ziro kabisa ,kuna nyingine ambazo miaka ya nyuma zilikuwa zinaongoza kwa kuwa wamwisho ila sasa wamejitaidi na wametoka huko hivyo basi tumewapongeza kwa njia hiyo"aliongeza Dkt Pima
Aliwataka walimu ambao hawakuguswa na zoezi hilo la utoaji wa fedha pamoja na zawadi kuhakikisha kuwa wanafundisha kwa bidii sana masomo yao na kupata ufaulu wa daraja la juu ili waweze kupata zawadi na motisha kama hiyo kwa kipindi kijacho
Awali mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela alisema kuwa ualimu ni kazi nzuri sana na inatakiwa kueshimiwa sana ikiwa ni pamoja na kubuni namna ya kuendelea kuwapa motisha
Mongela alisema unapomuona kiongozi ambaye yupo imara basi jua ya kuwa mwalimu wake wa ngazi za chini alimsimamia vema katika ukuaji wake
"Nataka tu niwambie kuwa taifa hili linawategemea sana ninyi walimu hasa kwenye malezi na ukuaji wa watoto wetu nawapongeza sana Jiji kwa kubuni jambo hili ambalo limekuwa ni motisha nzuri"alisema
Aliwataka walimu hao kuendelea kuhubiri amani kwa wanafunzi,kwani Kama kila mwalimu atasimama ipasavyo kwenye suala hilo basi maadili yatakuwa mazuri
Naye Mbunge wa Arusha Mjini,Mrisho Gambo alisema kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya walimu na maslahi yao hivyo basi wanatakiwa wajitume
Alidai kuwa zawadi au motisha ambayo.na yeye ameipata katika hafla hiyo ambayo ni kiasi cha Milioni moja ielekezwe moja kwa moja kwenye choo cha walemavu katika shule ya sekondari Kaloleni.