![]() |
Privanus Katinhila, Afisa Biashara Jiji la Arusha |
Na Zulfa Mfinanga,
Arusha.
Wafanyabiashara wa halmashauri ya Jiji la Arusha wametakiwa kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu za kufanya biashara ikiwa ni pamoja na kulipa kodi zilizowekwa na serikali kwa wakati ili kuepuka usumbufu kwa kuwa nia ya serikali ni kuhakikisha kuwa wanafanya biashara katika mazingira bora na salama.
Hayo yamesemwa na Afisa Biashara wa Halmashauri hiyo Privanus Katinhila alipokuwa akizungumza na wananchi wa jiji hilo kupitia vituo vya redio na Televisheni vilivyopo ndani ya Jiji hilo ambapo amesema suala la mapato ndiyo kipaumbele cha halmashauri kwa sasa hivyo ni wajibu wa kila mfanyabisahara na mtoa huduma kulipa kodi kulingana na biashara aliyonayo.
Alivitaja vyanzo vya mapato vilivyopo halmashauri ya Jiji la Arusha kuwa ni pamoja na leseni za biashara kwa maana ya biashara ndogo, ya kati na biashara kubwa, ushuru wa mazao, ushuru wa masoko, ushuru wa taka ngumu unaotokana na uchafuzi wa mazingira, ushuru wa madini, ushuru wa matangazo pamoja na ushuru wa standi kuu na standi ndogo ya mabasi.
Vyanzo vingine ni ushuru wa huduma yaani service levy kwa maana ya taasisi, mfanyabiashara na mtu binafsi ambao wanapaswa kulipa asilimia 0.3 ya mauzo yao ya mwezi, ushuru wa bodaboda pamoja na bajaji ambazo licha ya kuwa chini ya Mamlaka ya Udhibiti na Usafiri Ardhini(LATRA) lakini mapato yake hugawana na halmashauri.
“Lakini pia chanzo kingine cha mapato kinatokana na ushuru wa upimaji wa afya kwani watoa huduma za vyakula na vinywaji wanapaswa kupima afya zao kila baada ya miezi sita, hali kadhalika uuzaji wa vitabu kwa nyumba za kulala wageni ni miongoni mwa vyanzo vyetu vya mapato na vitabu hivyo vinapatikana Jiji ndiyo maana nimesema suala la mapato ni suala mtambuka kwa maana kwamba kila mtu anapaswa kulipa kodi” alisema Kantihila.
Aidha Katinhila amewatahadharisha wamiliki wote wa nyumba za kulala wageni ambazo hazijasajiliwa maarufu kama gesti bubu kujisalimisha haraka kwa mamlaka husika ili waweze kufanya biashara hizo kihalali kwani amesema wapo kwenye operesheni ya kukagua nyumba hizo usiku na mchana.
“Kuna watu wanaendesha gesti bubu huko mtaani, niwaambie tu kuwa sisi kwa kushirkiana na jeshi la polisi tunafanya operesheni usiku na mchana, wajue tu hata kufanya biashara hiyo bila kuwa na kibao cha kuonyesha hii ni nyumba ya kulala wageni ni kosa kisheria, wajisalimishe mapema wajue utaratibu ukoje lakini pia wamiliki wa nyumba hizo wanakumbushwa kulipa ushuru wa huduma ya asilimia 10 kwa mwezi ili wafanye biashara zao kwa uhuru” Alisisitiza.
Amesema operesheni wanazofanya hazina maana ya kumkomoa mtu bali siku zote serikali imeweka na itaendelea kuweka mazingira rafiki ya kufanya biashara kwa mtu yeyote atakayefuata utaratibu na sheria zilizopo.
Amesema ndiyo maana serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imewaondoa maeneo hatarishi wafanyabishara wadogo maarufu kama machinga na kuwajengea masoko mazuri, likiwemo soko la Ulezi, Machame Luxuary, Kiwanja Namba 68, pamoja na Soko la Mbauda, pamoja na kuwawekea miundombinu yote kama vile vyoo, maji, umeme na mitaro ya maji taka licha ya kuwa hawatozwi ushuru wowote.
Akizungumza jinsi ya kufungua biashara, Katinhila amesema ni lazima mhusika kuwa na Namba ya Mlipa kodi ya biashara(TIN Number) pamoja na Mtakaso wa Kodi yaani Tax Clearence ambazo zote hutolewa bure na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Baada ya kupata vitu hivyo utapewa maelekezo na TRA ya
nini cha kufanya, ndo baadaye utakuja kwetu kwa maana ya Halmashauri ukiwa na hivyo vitu ulivyopewa TRA utasema biashara yako ni ya aina gani ili ufanyiwe makadirio kwa mujibu wa sheria na kama kuna kitu hukielewi utaeleweshwa na wataalamu wetu na kisa utapatiwa leseni yako ndani ya siku moja au mbili”