Na Mwandishi wetu, APC
Mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya 200 nchini yanayojihusisha na Masuala ya haki za binadamu, yamepongeza serikali ya awamu ya sita kwa kukubali mapendekezo 187 ya kuboresha haki za binadamu ikiwepo kufanyia marekebisho sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016.
Serikali imekubali mapendekezo hayo katika kikao cha mapitio ya hali ya haki za binadamu (UPR) cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binaadam kilichofanyika Geneva ambapo serikali iliwakilishwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria,George Simbachawene.
Akizungumza na mwananchi leo Aprili 6,2022, Mratibu wa mapitio ya hali ya haki za binadamu nchini,kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC) Wakili Leopold Mosha amesema idadi ya mapendekezo yalikubaliwa imeongeza mara dufu kutoka 108 ya kikao cha Novemba 2021 hadi 187 katika ripoti ya mwisho iliyotolewa mwezi Machi 2022.
"Tunaipongeza sana Serikali ya awamu ya sita kwa kukubali mapendekezo mengi na tunaamini machache ambayo yanafanyiwa kazi yatakubaliwa"amesema.
Amesema awali asasi za kiraia ambazo zilikuwa zinaongozwa na THRDC, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Save the Children ziliwasilisha ripoti kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu. Baadaye mwezi Septemba 2021, Serikali ya Tanzania ilipokea jumla ya mapendekezo 252 .
Mosha amesema katika mapendekezo yaliyokubaliwa na serikali 20 yamekubaliwa kwa sehemu na hivyo kufanya mapendekezo yaliyokataliwa kupunguza kutoka 132 hadi 65 tu.
Miongoni mwa mapendekezo yalikubaliwa ni kuboreshwa sheria ya huduma za habari (MSA) ya mwaka 2016 ili kuongeza uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.
Amesema mengine yaliyokubaliwa ni kuiboresha sheria ya ndoa ili kupunguza ndoa za utotoni, kuboresha sheria ya vyama vya siasa ili kutoa uhuru wa vyama kukusanyika na kushiriki siasa.
Amesema serikali pia imekubali kufanyia maboresho sheria zinazohusu haki za wanawake, wazee na sheria ya mtandao, kanuni za maudhui mtandaoni (EPOCA) na Sheria kuhusu dhamana na sheria kuwalinda Watetezi wa Haki za Binadamu.
Mratibu wa THRDC Onesmo Olengurumwa ambaye alishiriki mkutano wa Geneva amesema mwelekeo wa serikali ni mzuri katika kulinda na kutetea haki za binadamu.
Amesema sasa ni wajibu wa taasisi nyingine za serikali na asasi za kiraia kuendelea kushirikiana na serikali kutekeleza mapendekezo hayo.
Mratibu wa kitaifa wa Kituo cha Usuluhishi (CRC)Gladness Munuo amesema wanashukuru serikali kusikia kilio cha wadau na sasa kuna mafanikio makubwa katika kuondoa changamoto na haki za binaadam.
"Tunaona uhuru wa habari umeanza kuimarika,wanasiasa wanaofanya kazi kwa uhuru na tunashukuru serikali kukubali kuifanyia maboresho sheria ya ndoa"amesema.