Rais Samia aleta hospitali za kanda ndani ya Jiji la Arusha

Dkt John Pima Mkurugenzi wa Jiji la Arusha akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani

 *Zitakuwa katika kanda nne za Olmot, Kati, Moshono na Muriet

*Dkt Pima asema zitakuwa na huduma zote za kibingwa


Na Seif Mangwangi, Arusha


Ikiwa ni mwaka mmoja tangu Rais Samia Suluhu Hassan kuwa madarakani, Halmashauri ya Jiji la Arusha imeendelea kuboresha huduma za afya na hivi sasa imepanga kujenga hospitali za kanda.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt John Pima amesema Serikali ya Samia Suluhu Hassan imeamua kujenga hospitali katika  kanda nne ndani ya Jiji la Arusha ili kurahisisha zaidi huduma za afya.


Amesema katika maamuzi yaliyopitishwa na Baraza la madiwani wa jiji hilo hospitali hizo zitakuwa katika kanda ya  Murieti katika kata ya Murieti kanda ya Moshono  katika kata ya Moshono na kanda ya Olmot katika kata ya olmot na kanda ya kati. 


Dkt Pima amesema  kanda ya Murieti itatumia hospitali ya Muriet ambayo imeendelea kuboreshwa ambapo tayari Jiji limetenga Milioni 200 kwaajili ya kununulia jenereta la kisasa (Automatic generator), na kuboresha miundo yote muhimu ikiwemo majengo yatakayotumiwa kutolea huduma za kibingwa.


"Hospitali ya Murieti itakuwa sawa na hospitali ya Wilaya, tunataka iwe inatoa huduma za kibingwa ili mgonjwa akitoka pale anapelekwa hospitali ya rufaa Mount Meru moja kwa moja, na sio hospitali ya Wilaya," amesema.


Amesema hospitali nyingine ya kanda itajengwa katika kata ya Moshono na nyingine itakuwa katika kanda ya Olmot katika kata ya Olmot ambapo tayari Jiji limetenga Milioni 600 na ujenzi unatarajia kukamilika kabla ya Desemba mwaka huu 2022. 


"Hospitali hizi na zenyewe zitakuwa zikitoa huduma za kibingwa na zitakuwa zikishirikiana na hospitali ya Wilaya iliyopo Njiro ambayo ni maalum kwaajili ya utalii 'Medical Tourism', ambapo huduma zote za kibingwa zitakuwa zikitolewa hapo na wageni kutoka nchi mbalimbali wataruhusiwa kufika kupata matibabu ya kibingwa," Amesema na kuongeza,


"Kwa ujumla Rais Samia Suluhu Hassan amesaidia sana kuboresha huduma za Afya Jijini kwetu, kwa kweli tunajivuna sana kuwepo kwake madarakani, baada ya mwaka huu utaona tatizo la huduma za afya zitakuwa zimemalizwa kabisa hapa kwetu, na kila siku tunaendelea kuboresha huduma ili watu wasisafiri mbali kupata huduma," amesema.

Majengo ya hospitalini ya Wilaya ya arusha linavyoonekana kwa nje 


Amesema kanda ya kati itatumia hospitali ya Kaloleni ambayo imeboreshwa kwa kuwekewa vifaa vya kisasa na huduma zote za kibingwa zinapatikana katika hospitali hiyo ikiwemo madaktari.


Akizungumzia huduma za afya katika hospitali ya Kaloleni mtaalam wa mionzi Faris Shuma amesema kitengo chake kimeboreshwa kwa kununuliwa mashine  mpya ya kisasa yenye uwezo wa kupima magonjwa kama tezi dume, goita, moyo na umeme wa mwili.


"Hii mashine unaweza usiipate hospitali nyingi hapa nchini mara nyingi ni katika hospitali za Mkoa au rufaa, lakini hapa kwetu tunayo, inauwezo wa kupima tezi dume, inapima mgonjwa mwenye maradhi ya moyo, joto la mwili, goita, n.k,"amesema.

Faris Shuma mtaalam wa mionzi katika hospitali ya Kaloleni akionyesha waandishi wa habari ( hawapo pichani),mashine ya kisasa ya kutolea huduma hiyo


Amesema tangu mashine hiyo iliponunuliwa wagonjwa wengi wamekuwa wakifika hospitalini hapo kupata huduma na kwamba kwa siku za kawaida wagonjwa zaidi ya 7 hupatiwa huduma za mionzi.

 

Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha maabara katika hospitali hiyo ya kanda ya kati, Dkt Erasto Kyando amesema hospitali hiyo ina maabara ya kisasa ambapo huduma muhimu za kibingwa zimekuwa zikipatikana ikiwemo mashine ya upimaji wa figo na maini, mashine ya uchunguzi wa damu (full blood picture).Waandishi wa habari wakiwa katika hospitali ya Wilaya ya Arusha iliyopo Njiro wakipata maelezo ya huduma za meno zinazotolewa katika hospitali hiyo kupitia mashine ya kisasa 

1 Comments

This is received, thanks for your comments, will come back to you

  1. Asante kwa news la jiji letu la Arusha

    ReplyDelete
Previous Post Next Post