Wakazi Kaloleni waishukuru serikali kuwapa elimu juu ya faida ya anwani za makazi, waomba elimu zaidi

 Na Seif Mangwangi,Arusha


Zoezi la kuandika anwani za makazi na majina ya mitaa limeendelea leo Februari 16,2022 katika mitaa mbalimbali katika kata ya Kaloleni ikiwa ni siku ya pili ya zoezi hilo Jijini humo, huku wananchi wakishukuru Serikali kuwapa elimu kuhusiana na faida ya zoezi hilo kwa uchache na kuomba kuelimishwa zaidi faida zake kiuchumi.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa APC Blog, wakazi hao wamesema sehemu kubwa ya makazi yao yalishawekwa namba lakini hawakuwahi kupewa elimu kuhusiana na faida za namba hizo hapo awali.


"Nyumba zetu zina namba kwa miaka kama minne iliyopita, lakini hatujui kwa undani faida zake ijapokuwa pia tunashukuru kwa elimu kidogo mliyotupatia, nafikiri mngetupatia elimu zaidi ya faida za namba hizi ingetusaidia sana ili tuweze kujiandaa na faida hizo hasa kiuchumi," anasema Jasmin Athuman mkazi wa kata ya Kaloleni, mtaa wa  stadium.


Ameiomba Serikali kuitisha vikao vya Mitaa na wao kuelimishwa kuhusiana na faida zake badala ya kuanza kuuliza maswali timu ya watu ambao wamekuwa wakipita kwenye mitaa yao kwaajili ya kuweka anwani hizo za makazi na kupata elimu kwa uchache kwa kuwa muda wa zoezi ni mdogo.


Hata hivyo kwa mujibu wa Afisa msimamizi wa zoezi hilo katika kata ya Kaloleni, Erinesta Moshi timu yake imebaini uwepo wa hitaji la wananchi kupewa elimu zaidi lakini hata hivyo wamekuwa wakijitahidi kuwaelimisha wananchi faida zake ijapokuwa kwa kutumia muda mchache.


Amesema kwa ujumla zoezi hilo limeendelea vizuri kwa siku ya pili na kwamba changamoto zilizojitokeza kwa siku ya kwanza zimeshapatiwa ufumbuzi. changamoto kubwa ilikuwa ni timu yake kurudia namba kwenye namba ambazo zikishawekwa mwanzo.


Awali akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt John Pima alisema ofisi yake imejipanga kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi wa Jiji la Arusha ikiwemo kupitia vipindi mbalimbali vya redio zilizopo Arusha.


Alisema yeye binafsi amekuwa akitumia redio za Arusha kutoa elimu kuhusiana na faida za zoezi hilo na wananchi ambao wamekuwa wakisikiliza vipindi kupitia redio hizo wamepokea kwa shauku kubwa zoezi hilo.


" Nimekuwa nikipokea maswali mengi sana kutoka kwa wananchi wanaosikiliza mahojiano yangu katika redio, hii inaonyesha ni namna gani wakazi wa Jiji la Arusha wamepokea vizuri zoezi hili,"Alisema Mkurugenzi Dkt Pima.


Zoezi la kuweka anuani za makazi katika jiji la Arusha lilizinduliwa rasmi jana Februari 14,2022 na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda ambaye katika hotuba yake aliwataka wasimamizi wa zoezi hilo kuifanya kazi hiyo kwa uadilifu wa hali ya juu kwa kuwa wameaminiwa.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post