DC Arusha Ampongeza Mkurugenzi Dkt.Pima zoezi la Anwani za Makazi, asema ametekeleza ilani ya CCM kwa vitendo

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda akizungumza na watendaji wa mitaa na wenyeviti wa mitaa ya Jiji la Arusha, aliyekaa kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt John Pima

 Na Seif Mangwangi, Arusha

Mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda amempongeza Mkurugenzi wa Jiji hilo Dkt John Pima kwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM), kwa vitendo na kuwataka   watendaji wa Halmashauri ya Jiji hilo kufuata nyayo za Mkurugenzi wao.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la uwekaji wa anwani za makazi katika Halmashauri ya jiji la Arusha na mafunzo kwa watendaji wa mitaa na wenyeviti wa mitaa yote ya Jiji la Arusha, DC Mtanda amesema ubunifu wa Dkt John Pima umesaidia Jiji la Arusha kupata tuzo mbalimbali  lakini pia kuliingizia mapato mengi kutokana na ubunifu wa vyanzo vya mapato.


Amesema moja ya maelekezo ya CCM ni kushirikisha wananchi katika shughuli zote zinazowahusu na hilo amelifanya kwa vitendo kwenye zoezi la uwekaji anwani za makazi kwa  kuwashirikisha wadau mbalimbali  ili kuondoa malalamiko miongoni mwa wananchi.


DC Mtanda ambaye pia alikuwa akizungumza wakati wa kufungua mafunzo kwa wenyeviti na watendaji wa mtaa yenye lengo la utekelezaji wa kazi ya anwani za makazi jijini humo amesema kuwashirikisha wadau katika zoezi hilo ni jambo jema ili kuepuka upotoshaji unaoweza kujitokeza kwa watu wasiopenda maendeleo.


"Kwa dhati kabisa ya Moyo wangu nakupongeza Mkurugenzi kwa kazi nzuri unayoifanya, katika zoezi hili mmefanya vizuri sana kuwashirikisha wadau ili  waelewe umuhimu wa zoezi la makazi maana yake nini, watendaji naombeni msimuangushe Mkurugenzi, ni vyema mkafanya kazi kwa umoja na mshikamano ili iweze kukamilika kwa wakati, naamini kwa uchapaji huu Arusha itakuwa ya kwanza kumaliza zoezi hili tena bila dosari," Amesema.


Mtanda amewataka watendaji kufuata maelekezo waliyopewa kuhusiana na namna ya utekelezaji wa zoezi hilo na kwamba kufanya kwao kazi vizuri ndio sifa ya jiji la Arusha kuendelea kupata fursa mbalimbali.

DC Mtanda pia Dkt.John Pima kuhakikisha stahiki za  wasimamizi wa zoezi hilo zinalipwa kwa wakati na hata kama zitachelewa wapewe taarifa mapema ili waweze kufanya kazi vizuri na pia waweze kuhojiwa na kuwajibishwa endapo watafanya vibaya katika zoezi hilo.


"Tunataka nyinyi watendaji na watumishi wa serikali muwe kiunganishi kizuri baina ya serikali na wananchi kwani mkitekeleza vizuri kazi zenu wananchi wataipenda serikali hii na tutakuwa tunafaidika sote,"alisema.


Awali Mkurugenzi wa Jiji hilo Dkt Pima alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa matayarisho ya zoezi hilo yamekamilika na kuanzia kesho (leo Februari 15,2022), timu ya vijana kwa kushirikiana na watendaji wa Kata tano ndani ya Jiji la Arusha watapita mitaani kuanza kazi kubainisha majina ya mitaa na kwamba zoezi zima la uwekaji wa namba linatarajiwa kumalizika ndani ya wiki mbili.


Wakati huo huo Dkt Pima amewataka vijana walioteuliwa kwenye zoezi la kubandika anwani za makazi katika kata tano za Kaloleni, Themi, Elerai, Mjini Kati na Sekei katika  jiji la Arusha kufanya kazi hiyo kwa makini.


Dkt Pima ametoa wito huo wakati akifunga mafunzo juu ya maelekezo ya namna ya kubandika anwani za makazi kwa vijana maalum walioteuliwa na jiji hilo ambao miongoni mwao wamekuwa wakifanyakazi za kujitolea na wengine wapo kwenye mafunzo ya vitendo katika Halmashauri ya Jiji hilo. mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa madiwani ndani ya Jiji hilo

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post