RC Arusha awataka wazazi kumuunga mkono Rais

Rc John Mongela 

 

Na Mwandishi wetu,

Arusha.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela ameridhishwa na ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya jiji hilo na kutoa rai kwa wazazi kuwapeleka watoto wao shule kwani mazingira yameboreshwa.


Mkuu wa Mkoa ametoa rai hiyo leo alipotembelea shule ya sekondari ya Arusha Day pamoja na shule ya msingi ya Muriet huku akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Said Mtanda, Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Arusha Dkt John Pima, Mstahiki Meya wa jiji hilo Maximilian Iraghe pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya Abraham Joseph.


Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa amewaasa viongozi pamoja na wananchi wa mkoa wa Arusha kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuhakikisha kuwa wanafunzi nchini wanasoma katika mazingira mazuri ikiwa nia pamoja kuupatia mkoa huo zaidi ya shilingi bilioni nane kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.


“Sasa kutokana na jitihada za Rais wetu za kutoa fedha hizo, nitoe rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wote wenye sifa za kuanza shule waandikishwe, kwa maana ya watoto wote wenye umri wa miaka minne waanzishwe darasa la awali, wenye umri wa miaka saba nao waandikishwe darasa la kwanza lakini pia wale wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza waripoti shuleni” Alisema Mkuu wa Mkoa.


Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Arusha Mhe. Said Mtanda amemwambia mkuu huyo wa mkoa kuwa wamepokea maelekezo hayo na wapo tayari kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mhe. Rais ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora wakati wote.


Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt John Pima amesema Mhe. Rais amelipatia jiji hilo kiasi cha shilingi bilioni 2.1 ambayo wamezitumia katika ujenzi wa vyumba 105 vya madarasa, madawati 5250, pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo 44 na kuongeza kuwa kutokana na ujenzi huo idadi ya wanafuzi kujiunga na elimu ya awali, darasa na kwanza na kidato cha kwanza imeongezeka.


Naye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Mhe. Maximilian Iraghe amemuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi watahakikisha kuwa wanafunzi wote wenye sifa za kusoma wanaandikishwa shuleni mapema iwezekavyo.


Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Muriet Dominic Gado amemwambia mkuu wa mkoa kuwa zoezi la kupokea wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza linaendelea vizuri na kwamba wanafunzi wa darasa la kwanza 558 kati ya 661 wamesharipoti shule leo na kwa darasa la awali wanafunzi 201 kati ya 251 nao wamesharipoti shuleni hii leo.


Naye mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Arusha Day Judith Mollel amemshukuru Rais kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia kuanzia majengo, viti na meza na kumuahidi kusoma kwa bidii ili kuja kulitumikia Taifa baadaye.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post