Waziri Katambi akague miradi ya maendeleo Shinyanga

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini na Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu,kazi,vijana na ajira Paschal Patrobas Katambi ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inatekelezwa katika jimbo la Shinyanga mjini.


Akiwa ameambatana na kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga mjini pamoja na viongozi wa serikali,Katambi ametembelea miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na miundombinu ya barabara katika kata ya  Kolandoto,Ibadakuli,Chamaguha,Ndembezi,Ngokolo, Kambarage, Shinyanga mjini, Kitangili, Ibinzamata na Kizumbi.


Katika kata hizo Mheshimiwa Katambi ametembelea na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya sekondari  Kolandoto, Uzogore  sekondari iliyopo kata ya Ibadakuli, Chamaguha sekondari, shule ya sekondari Mazinge iliyopo kata ya Ndembezi, Ngokolo sekondari, shule ya sekondari Town iliyopo kata ya Mjini Shinyanga, Mwasele sekondari iliyopo kata ya Kambarage, Busulwa sekondari iliyopo kata ya Kitangili, Ibinzamata sekondari pamoja na Kizumbi sekondari.


Katambi pia amekagua miundombinu ya barabara ujenzi wa madaraja ikiwemo daraja la mto chemu linalounganisha kijiji cha Uzogore na mtaa wa Bugwandege pamoja na daraja la mto soka linalounganisha Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na wilaya ya Kishapu ambapo madaraja hayo yapo katika kata ya Ibadakuli.

Mheshimiwa Katambi ameridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo ambapo amewapongeza viongozi waliosimamia shughuli ya ujenzi huo hasa ujenzi wa vyumba vya madarasa ambayo madarasa yote aliyokagua yamekamilika na kwamba vyumba hivyo vitafanyakazi kama ilivyokusudiwa.


“Kwa sehemu kubwa kwenye jimbo letu tumefanikiwa sana kwenye eneo la madarasa nipongeze sana jitihada za  madiwani ambao ni wawakirishi wa wananchi lakini pia watendaji wetu wa serikali yupo mkurugenzi  na  mkuu wa wilaya sisi tunapokwenda kutafuta  fedha zinapokuja kwenye maeneo yetu ya utawala maana yake tunatarajia kwamba mkuu wa wilaya na timu yake ya mkurugenzi pamoja na watendaji watafanyakazi ya kuhakikisha kile kilichokusudiwa kunafanyiwa kazi madiwani watasimamia kwahiyo nikupongeze mstahiki meya, mkurugenzi, mkuu wa wilaya pamoja na mkuu wa mkoa kwa kweli kazi kubwa ambayo imefanyika tunaridhika nayo na chama tunawashukuru sana kwa kutusimamia”.


Kwa upande wao walimu wakuu wa shule hizo wameishukuru serikali na kwamba wamesema mwaka kesho hakutakuwa tena na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi.


Aidha walimu hao wamezitaja baadhi ya  changamoto walizokutana nazo katika shughuli ya ujenzi huo wa vyumba vya madarasa ikiwemo mahitaji ya vifaa vya ujenzi kuongezeka, uhaba wa maji, baadhi ya bidhaa kupanda bei  hali iliyopelekea baadhi ya vitu kutofanyika kama vile kuweka vigae kwa baadhi ya shule.


Wakizungumza kwa yakati tofauti baadhi ya wananchi wa jimbo la Shinyanga mjini wameipongeza serikalikwa kuwaletea miradi hiyo ambayo wameeleza itasaidia kuharakisha maendeleo na wameahidi kuunga mkono jitihada hizo.


Ziara hiyo ya Katambi ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika jimbo lake ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa kupitia fedha za ruzuku ya UVIKO-19  zilizotolewa na rais SAMIA SULUHU HASSAN.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post