Ukatili wa kijinsia waelezwa kupungua kwa kasi Shinyanga

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mkuu wa Dawati la Jinsia Wanawake na Watoto Polisi Wilaya ya Shinyanga  Brighton Rutajama amesema hali ya ukatili wa kijinsia imepungua kutoka matukio 229 Mwaka 2020 hadi matukio 188 Disemba Mwaka huu 2021.


Rutajama  ambaye ni mkaguzi msaidizi wa Polisi amesema Dawati la jinsia la Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau wengine limekuwa na jitihada kubwa za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa namna mbalimbali ikiwemo kuelimisha jamii kupitia vyombo vya habari,mikutano ya hadhara lakini pia kwenye mikusanyiko mbalimbali ya Watu kueleza kuhusu  madhara ya ukatili wa kijinsia.


Amesema kwa kushirikiana na Wadau wengine wa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia imesaidia kupunguza ukubwa wa tatizo la ukatili wa kijinsia,huku akitoa rai kwa Wananchi kuchukua hatua za haraka kuripoti taarifa za matukio ya ukatili,ili kufikia malengo ya serikali ya kutokomeza vitendo hivyo.


“Kwa jamii ya Shinyanga tupaze sauti unapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia au kuona mtu akifanya vitendo hivyo basi chukua hatua kwa kuripoti tukio katika madawati ya polisi ya kijinsia vilevile unaweza kutua taarifa ya tukio katika ofisi za ustawi wa jamii, serikali za mitaa, vituo vya afya, vituo vya msaada wa kisheria vilivyopo hapa nchini ili kupata huduma kwa wakati msaidie muathirika kuripoti tukio lake ndipo tunaweza kutokomeza vitendo hivi”.


Afisa huyo wa Jeshi la Polisi amesema matukio ya kubakwa Watoto yanaongoza kutokana na mazingira hatarishi yanayowazunguka ikiwemo majumba ya starehe,nyumba za kulala wageni.


“Shinyanga inabadilika kwa kasi sana ukiangalia kuna nyumba za starehe hawaendi tu watu wazima peke yao wakati mwingine hata watoto au wanafunzi wanaenda maeneo hayo kwahiyo nitoe rai kwa wazazi watusaidie wasiruhusu watoto wadogo  kwenda kwenye nyumba za starehe kwa sababu ndiyo vyanzo vya matukio hayo vinavyoanzia huko”.


Dawati la Jinsia Wanawake na Watoto Jeshi la Polisi Wilaya ya Shinyanga, limeendelea kuelimisha Jamii kuhusu ukatili wa kijinsia kupitia kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya Watu pamoja na kutumia vyombo vya habari ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, ambayo kilele chake ni Disemba 10.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post