Waomba serikali kudhibiti biashara ya ngono

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga


Uongozi wa serikali ya mtaa wa Jomu Kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga umeiomba serikali ya Wilaya kuchukua hatua ya kudhibiti biashara ya kuuza  miili inayofanywa na baadhi ya wanawake.


Akizungumza mwenyekiti wa mtaa huo Peter Mashala amesema pamoja na jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanyika lakini hazijaleta mafanikio kwasababu biashara hiyo imeendelea kufanyika.


Bwana Peter ameiomba serikali pamoja na wadau wengine  kushirikiana na jamii ya mtaa huo kutatua changamoto hiyo ambayo isipotatuliwa mapema huenda ikachangia kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili.


“Hawa madada poa wanaojiuza ni kazi ngumu sana tumejaribu kutatua hili tatizo tunawakamata hadi tunawapeleka kituo cha polisi lakini unapowapeleka kituo cha polisi siku mbili tatu unawaona wako mtaani wamerudi walewale maana hilo tatizo bado ni endelevu na mpaka sasa hivi sijagundua kinachotokea”


Aidha mwenyekiti huyo ametaja changamoto nyingine inayoukabili mtaa huo kuwa ni kuwepo kwa wimbi la vijana wanaojihusisha wa tabia za udokozi wa mali za watu.


“Kunavijana wanatembea kwenye makundi ya watu kuanzia saba (7) wanaweza kufanya tukio lolote hasa kwenye maduka wakimuona kijana wanamuweza wanaingia kwenye hilo duka na kuanza kufanya vurugu huku wanachukua vitu mbalimbali niwaomba wananchi  wanapoona tukio kama hilo wanapaswa kunipigia simu mimi nitajua jinsi ya kufanya ilikusudi hao vijana wawekwe chini ya ulinzi”  


Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa mtaa huo wamesema vibaka na wanawake wanaouza miili yao ni changamoto inayohitaji jitihada za pamoja kuidhibiti.


Wananchi hao wametaja baadhi ya madhara  yanayoweza kujitokeza katika changamoto ya  wanawake wanaouza miili ambapo wamesema athari ya moja kwa moja ni kuenea kwa magonjwa ikiwemo Virus Vya Ukimwi (VVU).

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post