Hatua zisipochukuliwa, watoto 7000 kubakwa mwakani: Dkt Rose Reuben, Wadau watakiwa kuchukua hatua

Dkt Rose Reuben, Mkurugeni Mtendaji TAMWA

  

Na Seif Mangwangi, Arusha

KUFUATIA kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake nchini chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA), kimesema endapo hatua za haraka za kukomesha matukio hayo hazijafanywa, kuna uwezekano wa watoto  7000 kubakwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.


Katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye mtandao wa taasisi hiyo, Tamwa imesema pia endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, watoto 12,000 watakuwa  wamefanyiwa ukatili katika kipindi cha mwaka mmoja ujao jambo ambalo ni hatari na linatakiwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.


Taarifa za jeshi la Polisi kupitia taarifa yake iliyochapishwa kwenye tovuti ya Taifa ya takwimu inaeleza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2020 jumla ya makosa 11,001 yaliripotiwa ikilinganishwa na makosa 12,223 kwa mwaka 2019, ikiwa ni  upungufu wa makosa 1,222 sawa na asilimia 10.0.


“Makosa yenye ongezeko kubwa la idadi ni Kunajisi (23), Kutupa watoto (5) na Usafirishaji haramu binadamu (1). Aidha, makosa yaliyopungua sana kiidadi ni Kubaka (574), Mauaji (394) na Kulawiti (278),”ilisema taarifa hiyo.


Katika taarifa yake TAMWA imesema takwimu hizo mpya zinaogofya na kutoa wito kwa wadau, Serikali, wazazi na walezi kukubaliana na kutamka kuwa ubakaji nchini kwa hivi sasa ni janga.


“Tamwa tunaona ni wakati sahihi sasa, kwa wadau wa masuala ya ukatili wa kijinsia, kukaa pamoja na kupanga mikakati mipya na madhubuti zaidi ya kumaliza au kupunguza matukio haya kwani sheria na sera nzuri zipo lakini ukatili huo bado unaendelea katika jamii yetu,”imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Dkt Rose Reuben Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA.


Dkt Rose amesema “ni muhimu kwa taifa, sasa kuendelea kubuni njia mbadala na mpya za kukabiliana na janga hili. Tunaliita janga kwa sababu, watoto 3524 kubakwa si lelemama, bali ni tatizo kubwa katika jamii yetu ambalo linaharibu kabisa mustakabali wa maisha ya kizazi kijacho”.


Amesema Tamwa inaipongeza mahakama kwa kutoa hukumu na kufuatilia kwa ukaribu kesi za ubakaji, na kwamba  ipo mifano ya waliohukumiwa kwa kufanya matukio ya ubakaji sanjari na kutoa pongezi kwa madawati ya jinsia kwa kusimamia upelelezi na kutoa ushauri kuhusu matukio au kesi za ubakaji na ukatili mwingine. 

 

Dkt Rose alisema pamoja na jitihada zote hizo bado matukio ya ukatili wa kijinsia yanaendelea kuongezeka kila kukicha na kuhoji tatizo liko wapi na kudai ni muhimu kwa taifa, sasa kuendelea kubuni njia mbadala na mpya za kukabiliana na janga hili.

 

“Tunaliita janga kwa sababu, watoto 3524 kubakwa si lelemama, bali ni tatizo kubwa katika jamii yetu ambalo linaharibu kabisa mustakabali wa maisha ya kizazi kijacho,”amesema.

 

 Amesema mbali ya ukatili wa kijinsia kwa watoto kinamama wanaendelea kupokea vipigo, kubakwa, kupewa lugha dhalilishi katika jamii yao hali inayowafanya kuwa kundi linaloomboleza na wakati mwingine kuichukia jinsia yao. 

 

"Ukatili huu, una madhara ya muda mfupi, muda mrefu, kiuchumi, kimwili na kisaikolojia kwa wanawake na wasichana na watoto wote kwa ujumla, kwani inawazuia kushiriki kikamilifu na kwa usawa katika jamii yao," Amesema Dk Rose Reuben. 

 

"Hakuna namna nyepesi ya kuelezea madhara haya ya ukatili wa kijinsia, tumewahi kuona, pengine tumesikia lakini bado jamii nzima haijajua madhara yake kwa kina labda kwa sababu, matukio haya hayatokei kwa wingi mara moja. Lakini tungewapata waathirika hawa na kuwakusanya pamoja, basi Tanzania ingelia," Dkt Reuben.

 

"Ubakaji huu wa watoto ni janga. Serikali itambue kuwa hili ni janga kwa sababu madhara yake yanaweza yasionekana kwa sasa lakini yataonekana baadaye wakati ambapo kizazi hiki cha sasa kitakapokuwa kimeshika usukani" amesema Dkt Reuben.

 

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wanawake(UN-Women)zinaonyesha kuwa ukatili wa wanawake aghalabu hufanywa na mwenza, mume wa zamani au wa sasa. Inaelezwa kuwa wanawake zaidi ya milioni 640 wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea waliwahi kufanyiwa ukatili na wenza.

 

Ukatili huu unatajwa kusababisha msongo wa mawazo, kihoro, mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa ikiwamo UKIMWI na wakati mwingine waathirika kujiua. Takwimu hizo kadhalika zinaeleza kuwa, zaidi ya wanawake 87,000 duniani waliuawa na nusu yao, (50,000) waliuawa na mwenza au mwanafamilia. Zaidi ya thuluthi, waliuawa kwa makusudi na mwenza/mume wa sasa au wa zamani. 

 

Dkt Rose anasema TAMWA imeona zaidi kuwa unyanyasaji huu kwa hapa Tanzania umeendelea kujikita pia katika mashindano ya ulimbwende, vyuo vikuu, vyombo vya habari ikiwemo  mitandaoni pamoja na mahala pa kazi na kusema kuwa yote hayo yasipofanyiwa kazi, basi tutakuwa na dunia isiyo salama kwa kundi hili.

 

"Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha wazi kuwa anasimamia vyema haki za wanawake na watoto, tumemuona na kumsikia akipinga lugha dhalilishi kwa wanawake na udunishwaji wa kundi hilo katika nafasi za siasa na uongozi. Kongole Rais wetu," Amesema Dkt Rose Reuben

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post