MATAPELI ARDHI PANGANI KIBAHA, ‘MAHAWARA’ ZAO WANAOWATETEA WAKESHA WAKIPIGIANA SIMU NA KWA WAGANGA, WENGINE WATOROKA

*Wananchi wasema wameuziwa ardhi na viongozi, lakini wanatishwa waseme wamevamia ili viongozi wasishtakiwe kwa utapeli wa kuuza eneo la Serikali Mitamba huku wakijua sio lao
*Baadhi ya viongozi wa kisiasa na Serikali wamiliki maeneo makubwa ya ardhi kwa kutumia majina ya jamaa zao
*Ardhi ya CCM pia yauzwa kiholela bila kibali cha Bodi ya Wadhamini, wahusika waachwa, wanaosema ukweli wasumbuliwa na kutishwa

HUKU taarifa zikionyesha Kata ya Pangani iliyoko Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani ndiyo inayoongoza kwa utapeli wa ardhi, imebainika kuwa baadhi ya matapeli wameanza kukimbia baada ya kuwepo tetesi za kuanza utekelezaji wa agizo la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi la kuunda Tume ya kuchunguza vitendo hivyo.

Baadhi ya wanaodaiwa kutapeli watu kwa kuwauzia maeneo ambayo sio yao, wamekuwa wakidaiwa kukesha wakiwasiliana na ‘mahawara’ zao wanaowakingia kifua, baadhi yao wanakesha kwa waganga kutafuta dawa za kutochukuliwa hatua na kuna taarifa wengine wameanza kukimbia.

Hivi karibuni Waziri William Lukuvi akiwa Kata ya Pangani alizungumzia vitendo vya kitapeli katika ardhi, aliwaomba wananchi watoe ushirikiano wakati atakapounda Tume ya kufuatilia vitendo hivyo.

“Nitaunda Tume kuchunguza kwa kina suala la matapeli, ninachoomba kwa wananchi toeni ushirikiano pindi wanapopita katika maeneo yenu, mseme ukweli mliingiaje hapa Mitamba. Tunataka kukomesha vitendo hivi. Nitaunda Tume ambayo wajumbe wake watatoka mbali, sio hapa Pwani,” alisema Waziri Lukuvi na kushangiliwa na wananchi.
Kuna taarifa kuwa wakati wowote Tume hiyo itaanza kazi. Vitendo vya utapeli wa ardhi ni vya hali ya juu katika Kata Pangani, hili linathibitishwa na Mjumbe wa Kamati ya siasa wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kibaha, Zamda Komba akiwa katika ziara Mtaa wa Vikawe Shule Kata Pangani, kufuatia migogoro isiyoisha ya ardhi, ambapo alisema Kata ya Pangani ndiyo inayoongoza kwa vitendo vya kitapeli katika ardhi ukilinganisha na kata zote Halmashauri ya Mji Kibaha.

Taarifa zinaonyesha baadhi ya viongozi wa vyama tofauti vya siasa na Serikali ndio wahusika wakubwa wa utapeli wa ardhi, huku wengine wakiuza ardhi na kujipatia mamilioni ya fedha kwa matumizi binafsi badala ya maendeleo ya jamii.

Kata ya Pangani haina huduma bora na rasmi ya maji safi na salama wala kituo bora cha afya, kituo cha polisi, soko wala kiwanja cha mpira au huduma nyingine za jamii, lakini baadhi ya viongozi wanafanya utapeli kwa kuvamia ardhi kuuza na kujipatia mamilioni ya fedha. Baadhi ya viongozi wana kesi katika mahakama mbalimbali wakituhumiwa kutapeli ardhi hata za watu.

Kwa mfano mwaka 2012 kuna eneo katika Kata Pangani liliuzwa Sh87milioni, kwa muwekezaji ili achimbe mchanga, fedha waligawana viongozi ambao hadi sasa baadhi yao bado viongozi na wanadaiwa kuendelea kuvamia maeneo ya kuuza, huku wakiwa hawachukuliwi hatua zozote.

Baadhi ya waathirika wa kuuziwa ardhi bila kufuata kanuni ni Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho baadhi ya maeneo yake katika matawi ya Mkombozi na Kidimu yameuzwa kiholela kwa nyakati tofauti huku waliohusika wakiachwa na hata kutetewa.

Kwa mujibu wa Kanuni za Mali za CCM, hakuna mwenye mamlaka ya kuuza ardhi ya CCM pasipo kibali kutoka Bodi ya Wadhamini Taifa, lakini baadhi ya ardhi ya CCM katika maeneo ya Mtaa wa Mkombozi, na Kidimu Kata Pangani imeuzwa bila kupata kibali cha Bodi ya Wadhamini, huku waliohusika kuuza wakiachwa, kitendo kinachozua maswali.

Wale wanaotaka ardhi ya CCM irudishwe mikononi mwa CCM badala ya kuungwa mkono ili ardhi ya CCM irudishwe kwa ustawi wa CCM, wameanza kupangiwa njama chafu, wanasemwa vibaya kuwa wanajifanya wajuaji na wasomi, wanatishwa na kusumbuliwa, kitendo ambacho kimesababisha baadhi ya wanachama kuanza michakato ya kuomba msaada ngazi mbalimbali ikiwamo CCM Taifa ili ardhi ya CCM iliyouzwa kiholela Mitaa ya Mkombozi, Kidimu na kwingineko irudishwe CCM kwa ajili ya ustawi wa chama.

(Picha zote kwa hisani ya wizara ya ardhi).
Tunaunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na migogoro ya ardhi Tanzania.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post