WAZIRI SIMBACHAWENE ASEMA MAJAMBAZI YAMENYAMAZISHWA KIMYAKIMYA NCHINI, MSAKO WABAKAJI

 

 _Na Felix Mwagara, Moha,Kibakwe.

 WAZIRI0 wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema Jeshi la Polisi limewanyamazisha majambazi kimyakimya katika maeneo mbalimbali nchini baada ya hivi karibuni walipotaka kuijaribu Serikali.

Amesema operesheni ya kwanza ya kupambana na majambazi hao imefanikiwa kwa ufanisi mkubwa na sasa operesheni ya awamu ya pili tayari imeanza kwa watu wote wanaofikiri kufanya ujambazi ndiyo njia sahihi ya kujipatia kipato.

Akizungumzia na mamia ya wananchi wa Kata ya Lufu, jimboni kwake Kibakwe, Wilayani Mpwapwa, leo, Waziri Simbachawene amesema hivi karibuni uhalifu ulitokea na kuonekana kama unaongezeka kwa kasi na baadhi ya matukio ya ujambazi yalisikika katika baadhi ya miji ikiwemo Dar es Salaam, Arusha na Mwanza wakidhani kuwa Serikali imelegea hivyo wakawa wanaijaribu.


 “Wapo watu wengine wanafikiri uhalifu utawasaidia, kwa wale ambao wanavichwa vigumu wanaendelea kuichezea Serikali kwa kutokutaka kuacha uhalifu, kuacha ujambazi wa kutumia silaha, wanaopenda kubaka, wanaopenda kunyang’anya, wanaotumia pikipiki kupora, sisi tumeyaweka makosa hayo kama makosa makubwa, tukikukamata tunamalizana naye kimyakimya, wewe utajua kimyakimya tunamalizana kinamna gani,” alisema Simbachawene.


 Waziri Simbachawene amewataka Watanzania kufanya kazi halali kwa kuwa fursa zipo nyingi nchini kuliko kufanya uhalifu ambao utawaletea matatizo makubwa na kamwe hawawezi kufanikiwa kwa kufanya shughuli isiyo halali.

“Nawaomba Watanzania, na leo nazungumzia hapa Lufu, Jimbo la Kibakwe, Wilaya ya Mpwapwa, nataka kauli hii ifike nchi nzima, kwamba uhalifu sio dili, serikali ipo makini, tutadili na wahalifu wote mpaka tone la mwisho, acheni kufanya uhalifu, ukiwa mtu wa kupanga mambo yako utafanikiwa tu, lakini uhalifu hauwezi kukusaidia, na hata ukikusaidia leo, ni shimo la kutumbukia baadaye na utaishia huko ndani,” alisema Simbachawene.


Aidha, Simbachawene aliwapa wananchi hao, ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo amewataka wananchi wa jimbo lake waendelee kufanya kazi, na pia Serikali inaendelea kuwaeletea maendeleo ikiwemo umeme wa REA-Mradi wa Umeme Vijijini, muda wowote unafika katika baadhi ya vijiji vichache kikiwemo Kijiji cha Lufu ambacho kumefanyika mkutano huo wa hadhara.

“Lazima mfanye kazi, niwaambie ukweli tu, njia pekee ya kutoka katika maisha haya ni kufanya kazi, tujishughulishe kwa kazi mbalimbali, tuendelee na kilimo, tushirikiane kufanya kazi mbalimbali, tuwe wabunifu, tusikae tu na kuanza kuwasema watu, hatutaendelea, sasa Lufu hakuna tena shida ya barabara, tulime mazao mbalimbali na kwakuwa barabara ni nzuri tutaweza kuyasafirisha mazaao kwenda kuuza Mpwapwa au Dodoma,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa Wananchi wanapaswa kushirikiana na Serikali katika kudhibiti uhalifu kwa njia ya ulinzi shirikishi ambapo kila mwananchi anapaswa kutoa taarifa za uhalifu katika eneo lake ili kuweza kudhibiti uhalifu katika maeneo tunayoishi.

Awali Diwani wa Kata ya Lufu, Gilbert Msigala alimshukuru Waziri huyo kwa kulisaidia jimbo hilo na wananchi kuendelea kuwa na imani naye kutokana na mabadiliko makubwa yaliyopatikana katika Kata yake na Jimbo la Kibakwe kwa ujumla na pia aliwaonya wananchi wa Kata yake wasijishughulishe na uhalifu na pia akalipongeza Jeshi la Polisi kwa kufanya kazi nzuri katika Wilaya ya Mpwapwa.


“ Mheshimiwa Waziri ambaye pia ni Mbunge wetu, hali ya ulinzi na usalama ndani ya Kata yetu ipo shwari na pia tunashirikiana na kamati za ulinzi ndani ya Kata yetu, Jeshi la Polisi linatoa msaada mzuri ambao vibaka mbalimbali wamesambaratishwa, pia Mheshimiwa Waziri wananchi wa Lufu wanafuraha sana kwa ujio wa umeme, hakika Lufu itafunguka baada ya kupata umeme huu, tunakushukuru sana kwa kuwa na moyo huo, nasi tupo nawe siku zote,” alisema Msigala.

Waziri Simbachawene pia aliwataka wananchi wa Jimbo lake, na Watanzania wote nchini, kuendelea kujiandikisha kwa ajilli ya kupata Vitambulisho vya Taifa, na kwa wale ambao walishajiandikisha na wakapewa namba, muda wowote watapewa vitambulisho vyao kwa kuwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaendelea kutoa vitambulisho hivyo kwa kila wilaya kwa nchi nzima.This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post