Watumishi viwanja vya ndege watakuwa kuchukua tahadhari ya Corona

 WATUMISHI  WA MIPAKANI KUJILINDA NA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA CORONA :DKT:SICHALWE


Na WAMJW- Kilimanjaro 


Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amewaagiza Watumishi wote wa Afya katika Mamlaka za viwanja vya ndege kujilinda wenyewe kwa kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji safi tiririka. 


Dkt. Sichalwe ametoa agizo hilo leo wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utayari wa kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro na Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kaskazini KCMC. 


"Watumishi wote wachukue tahadhari za kujikinga dhidi ya ugonjwa huu kwa kuhakikisha kwamba wamevaa Barakoa, wana nawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka au kutumia vitakasa mikono na kupunguza misongamano ambayo haina umuhimu " amesema Dkt. Sichalwe. 


Aliendelea kusema kuwa, suala la kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona sio tu kwa Watumishi peke yao, bali na kwa wageni pia wanaotoka na kuingia nchini, huku akisisitiza kuwa pamoja na kuwachukua vipimo watu waendelee kuwasisitiza juu ya elimu ya kujikinga ikiwemo kuvaa barakoa. 


Amesema, sasa hivi wageni wameongezeka hasa Watalii wanaofika katika nchi ya Tanzania kupitia uwanja huu wa kimataifa wa Kilimanjaro, hivyo ni muhimu kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Corona. 


Aidha, amefurahishwa na kitendo cha Wasafiri kuanza kujaza taarifa kupitia njia ya mtandao na kufanya malipo kupitia njia ya mtandao jambo ambalo limesaidia kurahisisha zoezi zima la upimaji na kukamilika ndani ya muda mfupi.


"Nzuri zaidi ni kwamba Wasafiri hawa wameanza kujaza taarifa zao kwenye mtandao na kulipa kwenye mtandao ambayo hii imefupisha kabisa zoezi la upimaji kwa sababu ukishatambuliwa unaenda kuchukuliwa sampuli na ndani ya muda mfupi anakuwa ameshapata majibu yake" amesema Dkt. Aifello Sichalwe. 


Hata hivyo amewaagiza kuongeza vifaa vya utoaji huduma kama mtandao na computer katika uwanja huo hususan katika utoaji huduma za upimaji wa Corona ili kuokoa muda wakati wa kutoa kopi za vyeti vyao.


Pia Dkt. Sichalwe ametembelea Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kaskazini KCMC na kujionea hali ya utayari wao wa kuwahudumia wagonjwa wenye maambukizi ya Corona, huku kwa kiasi kikubwa akiridhishwa na hatua za utoaji huduma zinazochukuliwa na Watoa huduma katika Hospitali hiyo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona. 


Amesema kuwa, "Kwa kiasi kikubwa tumejiridhisha na utayari wao kwa upande wa upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba na hata uzalishaji wa gesi tiba ya oksijeni"


"Hawa wenzetu wana mtambo mkubwa wa kuzalisha hewa ya Oksjeniwenye uwezo wa kuzalisha mitungi ya hewa ya oksijeni zaidi ya 375 kwa siku, huku matumizi yao kwa sasa yakienda mpaka mitungi 200 mpaka 300 kwasababu hii ni Hospitali kubwa kwa siku " amesema. 


Mbali na hayo, Dkt. Sichalwe ametoa rai kwa Wataalamu wenye ubobezi katika Hospitali hiyo kufanya tathmini ili kubaini maeneo ambayo wagonjwa wengi hutokea ili kwenda kuwajengea uwezo Wataalamu wenzao ili waweze kuwahudumia wagonjwa huko huko jambo litalosaidia kupunguza mzigo wa wagonjwa katika Hospitali ya KCMC. 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post