Waziri wa Madini Doto Biteko akishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya kampuni ya MMG GOLD LIMITED ya kulipa Shilingi Milioni 36 ndani ya siku 60. Kushoto ni  Mkurugenzi wa mgodi huo Yury Chernomorchenko akitia saini makubaliano hayo Mkoani Mara.


***************

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameuagiza uongozi wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya Dhahabu MMG GOLD LIMITED unaomilikiwa kwa ubia kati ya Kampuni ya MMG na Polygon kulipa deni la kiasi cha shilingi milioni 36 zinazodaiwa na kijiji kwa mujibu wa mkataba wa uwekezaji.

Agizo hilo amelitoa, Julai 19, 2021 wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua shughuli za uchimbaji katika mgodi wa MMG GOLD LTD katika kijiji cha  Seka kata ya Nyamlandililila wilaya ya Musoma Vijijini , Mkoani Mara.

Akizungumza na Mkurugenzi wa mgodi  huo Yury Chernomorchenko, Waziri Biteko ametoa miezi miwili deni hilo liwe limelipwa na kampuni hiyo. 

Biteko amesema kuwa, kampuni hiyo ilikuwa inadaiwa zaidi ya shilingi milioni 60 toka mwaka 2018 na Serikali ya kijiji kama ushuru, deni lililoachwa na menejimenti iliyopita ya MMG ambapo walilipa fedha kiasi na hadi sasa deni linalodaiwa ni shilingi milioni 36 na kijiji kwa mujibu wa mkataba wa uwekezaji.

“Niwaombe Serikali za mitaa, Vijiji na Halmashauri, makubaliano yoyote wanayoingia na migodi ili yaweze kuwa na nguvu ya Kisheria kwa msimamizi wa migodi ni lazima wayasajili makubaliano hayo kwenye ofisi ya madini.” amesisitiza Biteko

“Tunataka tuone haya manufaa ya mgodi huu yaweze kuonekana kwenye maisha ya kawaida ya wananchi kwenye miundombinu ya barabara, miundombinu ya elimu na afya”

Pia, amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara Nyaisara Mgaya  kuhakikisha anasimamia malipo hayo yanafanyika ndani ya muda hu ona endapo hayataliwa asimamishe shughuli zote katika mgodi mpaka deni litakapolipwa.

Akiwa kwenye mgodi wa uchimbaji Dhahabu wa Cata Mining Waziri Biteko ameagiza uongozi wa mgodi huo kuzingatia Sheria na Kanuni  za madini zilizopo hapa nchini hususan wanapofanya ununuzi wa bidhaa mbalimbali na wanapotafuta kampuni za kufanyanazo kazi kwenye mgodi.

Msipozingatia sheria za madini mtapigwa faini ya shilingi milioni 50 jambo  ambalo Serikali ya awamu ya Sita haipendi, tunataka kuwalea  ili mkue zaidi siyo kuwarudisha nyuma,” amesema Waziri Biteko.

Akijibu swali la waziri kuhusu ajira kwa wazawa, Mkurugenzi wa Mgodi huo Johann Christoffel amesema hadi sasa wana watumishi 470 ambao ni wazawa jambo ambalo limepongezwa na Waziri Biteko.

Hata hivyo amewashauri wanapoajiri wazawa watoe kipaumbele kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka mgodi wa Cata ili kuweka mazingira mazuri ya kiuhusiano na jamii.

Waziri Biteko amefanya ziara ya siku moja Mkoani Mara na kutembelea migodi miwili ya MMG Gold Limited na Cata Mining. Mkoa wa Mara umebarikiwa kuwa na aina nyingi za Madini ambayo ni dhahabu, shaba, Silver, chuma, chokaa, soapstone na madini ya ujenzi. Kati ya hayo madini yanayopatikana kwa wingi zaidi ni madini ya dhahabu.