Wanafunzi Arusha wakimbilia masokoni baada ya shule kufungwa kwa Corona

 

Soko la Kilombero kama linavyoonekana kwa nje 

Na Mwandishi Wetu, Arusha

TANGU kulipoibuka kwa janga la ugonjwa wa Corona nchini na kupelekea kufungwa kwa shule za Sekondari na msingi nchini, idadi kubwa ya wanafunzi wamekimbilia katika masoko nchini wakifanya biashara.

Kundi kubwa la wanafunzi wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 10 hadi 15 wamekusanyika katika masoko ya Kilombero na Soko Kuu jijini hapa wakifanya biashara ya kuuza mifuko ya kubebea bidhaa mbalimbali za sokoni.

Mbali ya kuuza mifuko vijana wengine wamekuwa wakitafuta ujira kwa kuelekeza maegesho ya magari ya wateja wanaofika sokoni hapo kwaajili ya kupata mahitaji ambapo baada ya mteja kufanya manunuzi humpatia kijana aliyemwelekeza kiasi ambacho atapendezwa nacho.

Aidha vijana hao pia wamekuwa wakitumika kama vibega wa kubebea wateja wanaofika sokoni kwaajili ya kupata mahitaji ya nyumbani, na kulipwa ujira wa kati ya Tsh500 hadi 2000 kwa kazi hiyo.

Akizungumza na APC BLOG, mmoja wa vijana hao aliyejitambulisha kwa jina la Edward Saitabau anayesoma darasa la sita shule ya msingi Olmuringaringa anasema ameamua kufanya kazi hiyo baada ya shule kufungwa na nyumbani kwao maisha ni magumu.

“Nyumbani maisha ni magumu, baba hana kazi na mama pia, kwa hiyo nimeamua kuja sokoni kutafuta pesa baada ya shule kufungwa ili nipate pesa kidogo ya kujikimu, baada ya shule kufunguliwa lakini pia pesa nitakayoipata napeleka chakula kidogo nyumbani,”amesema.

Amesema Serikali kuamua kufunga shule ni fursa kwake kama kijana kwa kuwa anapata nafasi ya kujitafutia fedha ambazo zitamsaidia pindi shule zitakapofunguliwa kununulia mahitaji ya shule kama daftari, viatu na sare za shule.

 

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post