HALMASHAURI NCHINI ZASHAURIWA KUANZISHA MACHINJIO ZA KISASA

 

 Abdallah Chamzimu  (aliyevaa kofia)mkuu wa Idara ya Mifugo Shinyanga na Edga Mamboi Afisa Nyama kutoka Bodi ya Nyama Tanzania.
Abdallah Chamzimu  (aliyevaa kofia)mkuu wa Idara ya Mifugo Shinyanga na Edga Mamboi Afisa Nyama kutoka Bodi ya Nyama Tanzania,akitoa ufafanuzi wa jambo .

HALMASHAURI NCHINI ZASHAURIWA KUANZISHA MACHINJIO ZA KISASA 

Na.Vero Ignatus

Halmashauri Nchini zimeshauriwa kuanzisha   machinjio za kisasa (viwanda vya nyama) ili kuzalisha nyama bora salama ikiwa ni sehemu ya kuongeza mapato ya Halmashauri husika haswa katika kipindi hiki ambacho Tanzania ipo katika uchumi wa kati wa viwanda.

Hayo yamesemwa na Ndugu. Edgar Mamboi (Afisa Nyama) kutoka Bodi ya Nyama Tanzania alipotembelea kiwanda cha nyama cha Halmashauri ya manispaa ya shinyanga (Shinyanga Municipal Abattoir) na kufanya ukaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Nyama Na. 10 ya Mwaka 2006 na kanuni zake, sambamba na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusiana na uzalishaji wa nyama bora na salama ili kukidhi soko la ndani na nje ya Tanzania.

Ndugu. Mamboi amesema kuwa kutokana na taifa kuwepo kwenye uchumi wa kati wa viwanda ni vyema Halmashauri zote nchini kuchangamkia fursa hiyo kwa kuanzisha machinjio za kisasa zitakazozalisha nyama na bidhaa zake kwa kuzingatia viwango vya ubora . 

Aidha, Bodi ya Nyama Tanzania itaendelea kutoa elimu kwa wadau kuhusiana na uzalishaji wa mifugo unaokidhi viwango, uzalishaji wa nyama Bora na salama, elimu ya biashara ya nyama ikiwemo uuzaji wa nyama katika mazingira yanayokidhi matakwa ya Sheria, sanjari na usalama wa afya ya mlaji.

Kwa upande wake mkuu wa Idara ya Mifugo Halmashauri ya Manispaa Shinyanga Ndg. Abdallah Chamzimu amesema kukamilika kwa kiwanda hicho itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uchinjaji holela wa mifugo, lakini pia amewataka wachinjaji waliokuwa wanachinja mifugo machinjio ya nguzo nane na kwenye makaro mbalimbali kutii makubaliano waliyokubaliana kupitia vikao walivyokaa na hatimaye kuchinjia mifugo yao kwenye kiwanda hicho.

Aidha, uwezo wa kiwanda hicho ni kuchinja ng'ombe 600, mbuzi na kondoo 1,500 kwa siku na amesema  kiwanda hicho kimekamilika kwa asilimia tisini na tano bado mambo madogo madogo ikiwemo uwekaji wa mfumo wa baridi wa kuhifadhia nyama na mfumo wa maji taka ambao unatarajiwa kukamilishwa hivi karibuni.

Pamoja na hayo, kukamilika kwa kiwanda hicho kutaongeza wigo wa ajira nchini. Aidha, kiwanda hicho kinatarajia kuhudumia mikoa yote ya kanda ya ziwa na maeneo mengine nchini na kuhudumia soko la nje ya nchi.

Mwisho.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post