WIZARA YA MAJI YATEKELEZA AHADI YA RAIS MAGUFULI MBALIZI

 Na Mohamed Saif, Mbeya

 

KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWASA) kwa kutekeleza kwa haraka agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kuwafikishia huduma ya majisafi wananchi wa mji mdogo wa Mbalizi Wilayani Mbeya. 

 

Ametoa pongezi hizo Agosti 6, 2020 alipotembelea mradi wa Maji wa Shongo-Mbalizi ikiwa ni ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais Magufuli ya kuwaondolea kero ya ukosefu wa majisafi wananchi wa mji mdogo wa Mbalizi aliyotoa Aprili 27, 2019 kwa Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa.

 

Mhandisi Sanga alisema amefurahishwa kuona ahadi ya Rais Magufuli kwa wananchi wa Mbalizi imetekelezwa na tayari mradi unafanya kazi na wananchi wameanza kunufaika.

 

“Mtakumbuka maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli aliyoyatoa alipopita hapa Mbalizi, alituagiza sisi Wizara kupitia Mbeya UWASA kuhakikisha tunawafikishia wananchi wake hapa huduma ya majisafi na alisisitiza mradi utekelezwe haraka nami ninafarijika kuona tayari wameanza kunufaika,” alisema Mhandisi Sanga.

 

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo wa bilioni 3.3, Mkurugenzi Mtendaji wa Mbeya UWASA, Mhandisi Ndele Mengo alisema ulianza kujengwa Julai 1, 2019 na hadi hivi sasa umefikia asilimia 98 na huku idadi ya wananchi waliounganishwa na huduma ikiwa ni 108 na vituo 10 vya kuchotea maji.

 

Mhandisi Ndele alisema uwezo wa mradi ni kuzalisha kiasi cha lita milioni 8.5 hadi 10 kwa siku na kwamba maji yanayotumika kwa sasa ni chini ya lita milioni nne kwa siku kutokana na maunganisho yaliyokwishafanyika.

 

Kufuatia taarifa hiyo ya Mhandisi Mengo, Katibu Mkuu Sanga aliielekeza Mbeya UWASA kuhakikisha inaunganisha wateja wengi zaidi huku akisema kiasi cha wananchi waliounganishwa hakiridhishi ikilinganishwa na ukubwa wa mradi na hivyo alisisitiza kasi iongezeke ya kuwaunganisha wananchi.

 

“Dhamira ya Rais Magufuli ni kuona wananchi wake wanafikishiwa huduma ya majisafi; sasa kwa idadi mliyonieleza hawa mliyowaunganisha ni wachache sana, hakikisheni mnatanua wigo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi kama anavyoelekeza Mheshimiwa Rais,” alielekeza Mhandisi Sanga.

 

Aidha, wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wa Mbalizi walieleza kufurahishwa kwao na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwaondolea kero mbalimbali zilizokuwa zikiwasumbua kwa muda mrefu ikiwemo ya ukosefu wa huduma ya majisafi.

 

Akizungumza mbele ya Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Usahandeshi katika Mji Mdogo wa Mbalizi, Joster Mwalingo alimshukuru Rais Magufuli kwa maelekezo yake kwa Wizara ya Maji ya kuhakikisha wananchi wa Mbalizi wanapata maji na pia aliipongeza Wizara ya Maji kwa utekelezaji wa haraka wa maelekezo hayo.

 

Mwalingo alisema tangu kitongoji hicho kianzishwe hakikuwahi kuwa na huduma ya majisafi na kwamba wakuwahi kufikiria itafika siku nao watapata huduma kwa haraka kama ilivyotokea lakini kwa maelekezo ya Rais Magufuli na jitihada za Wizara kupitia Mbeya UWASA ndoto yao imetimia.

 

“Tunamshukuru sana Rais wetu, hakika anasema na kutenda na pia tunawapongeza nyinyi watendaji wa Wizara mkiongozwa na Waziri Mbarawa kwa kuyapokea maelekezo na kuyafanyia kazi kwa kasi na sasa hivi maji tunapata,” alipongeza

 

Mhandisi Sanga yupo Mkoani Mbeya kwa ziara ya siku tatu ya kukagua ujenzi wa miradi ya maji ambapo mbali na mradi huo wa Shongo Wilayani Mbeya, atatembelea miradi ya maji ya Busokelo na Bulongwe ya Wilayani Rungwe pamoja na Chitete na Ndalambo ya Wilayani Momba Mkoani Songwe.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Mbeya, Mhandisi Ndele Mengo wakati wa ziara yake kwenye tenki la maji la mradi wa Shongo Mbalizi, Wilayani Mbeya.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akielekeza jambo wakati wa ziara yake kwenye mradi wa maji wa Shongo Mbalizi, Wilayani Mbeya.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akikagua chanzo cha maji cha mradi wa Shongo Mbalizi, Wilayani Mbeya wakati wa zira yake ya kukagua hatua ya ujenzi wa mradi huo

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Maji Mbeya (Mbeya UWASA), Edna Mwaigomole akimwongoza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (nyuma yake) alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli la ujenzi wa mradi wa maji wa Shongo Mbalizi, Wilayani Mbeya.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post