WAANDISHI WA HABARI WAPATA AJALI YA GARI KWENYE MSAFARA WA WAZIRI WA MADINI

George Binagi-GB Pazzo, BMG
Msafara wa Waziri wa Madini, Doto Biteko umepata ajali kwa kuhusisha gari lililokuwa limewabeba waandishi wa habari kukosa mwelekeo na kugonga kingo za barabara katika eneo la Murugunga, Kata ya Murusagamba, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera.

Katika ajali hiyo, baadhi ya waandishi wamepata majeraha na kupatiwa huduma ya kwanza katika Kituo cha Afya Murusagamba na kisha kupelekwa mkoani Geita kwa uchunguzi zaidi.

Ajali hiyo imetokea mapema leo Julai 03, 2020 kwa kuhusisha gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye nambari za usajili STL 3132 mali ya Wizara ya Madini huku Waandishia wa Habari waliokuwemo wakiwa ni Nazareth Ndekia (TBC), Emmanuel Ibrahim (Clouds), Victor Bariety  (Chanel Ten) pamoja na Salma Mrisho (Star TV).

"Vumbi limesababisha dereva ashindwe kutambua pale kuna kona . Amejitahidi kulimudu gari vinginevyo lingepinduka. Tunamshukuru Mungu tumetoka salama" amesema Emmanuel Ibrahim.

Kufuatia ajali hiyo, Waziri Biteko aliyekuwa ametembelea mgodi wa madini ya viwandani Manganizi (Manganese) Magamba ametoa pole na kuwaombea afya njema waandishi hao pamoja na dereva wao.

Akiwa katika mgodi wa Manganizi Magamba, Biteko amewaagiza Mafisa Madini katika mikoa yote nchini hadi kufikia Julai 15, 2020 wawe wamefanya sensa ya madini ya viwandani yanayosubiri vibali kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi ili vibali hivyo vishughulikiwe.

Awali msimamizi wa mgodi wa Manganizi Magamba, Sarah Lusambagula amesema soko kubwa la madini ya Manganizi yanayotumika kwenye utengenezaji wa bidhaa za chuma liko nje ya nchi hivyo ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kusaidia upatikanaji wa kibali cha kuuza shehena ya madini ghafi aliyonayo kwani ikikaa muda mrefu inapoteza ubora.

Chanzo - BMG

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post