Virusi vya corona: Watu 497 wapya waambukizwa Kenya

Kenya inalenga kufikia upimaji wa corona kwa watu zaidi ya 3,000 kila siku

Wizara ya Afya nchini Kenya imetangaza ongezeko la watu 497 wapya wenye virusi vya corona.

Idadi hiyo ni ya juu zaidi ya maambukizi kuwahi kushuhudiwa kwa siku tangu ugonjwa huo ulipogunduliwa nchini humo.

Kufikia sasa Kenya ina jumla ya watu 10,791 walioambukizwa virusi vya corona.

Katika taarifa kwa wanahabari siku ya Jumanne kuhusu mwenendo wa hali ya ugonjwa wa Covid-19 nchini Kenya, Katibu mkuu katika Wizara ya Afya Mercy Mwangangi pia alitangaza kuwa watu watano zaidi wamefariki kutokana na ugonjwa huo katika kipindi cha saa 24, na kufikisha 202 idadi ya vifo vy corona.

Wakati huohuo, wafanyakazi wa Hospitali ya kujifungua kina mama ya Pumwani mjini Nairobi wamegoma baada ya wahudumu 41 wa hospitali hiyo kupatikana na virusi vya corona.

Kaimu Mkukuruenzi wa Afya Patrick Amoth, amethibitisha idadi ya waliopata maambukizi katika hospitali hiyo na kuongeza kwamba madaktari waliosalia watapimwa.

Alisema kwamba walioambukizwa 41 ni kati ya 290 waliopimwa huku wahudumu wengine 100 zaidi wakiwa wanasubiri kufanyiwa vipimo.

Wafanyakazi waliosalia kutoa huduma katika hospitali hiyo sasa wameonesha wasiwasi wao baada ya kugundulika kwa maambukizi zaidi ya virusi vya corona huku wengine wakisema kwamba wamelazimishwa kusalia kazini licha ya tukio hilo.

"Tuna tatizo kubwa katika hospitali ya kujifungua ya Pumwani ambapo ninafanyakazi. Serikali ilianza kupima wafanyakazi ugonjwa wa Covid-19 na idadi ya wanaopata maambukizi inazidi kuongezeka," amesema mmoja wa wafanyakazi ambaye hakutaka kutambuliwa kwa hofu ya kuadhibiwa.

Sasa wafanyakazi wanaishi kwa hofu kwa sababu ya kukosa kujua ukubwa wa maambukizi katika hospitali hiyo, na hilo pia linaweka kina mama wajawazito waliolazwa hospitalini humo kuwa katika hatari zaidi.Chanzo BBC

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post