TANAPA yatoa tozo mpya kuingia hifadhini, yashusha bei kuvutia watalii zaidi

NA GRACE MACHA, ARUSHA

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa nchini, (TANAPA), imefanya mabadiliko ya tozo kwa kupunguza viwango kwa baadhi ya bidhaa za utalii huku wakianza tozo mpya ya kuingia hifadhini zaidi ya mara moja, (multiple entry).

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano wa shirika hilo, Pascal Shelutete amewaeleza waandishi wa habari ofisini kwake leo julai 30, kuwa mabadiliko hayo ya  tozo yanaanza kutumika rasmi Agosti mosi mwaka huu mpaka juni 30, mwakani.


 Amesema tozo ya kuingia hifadhini zaidi ya mara moja itakuwa ya aina mbili tofauti ambapo kwa wageni wanaolala ndani ya hifadhi watapewa kibali cha saa 24  huku wale wanaolala nje ya hifadhi wakipewa kibali cha saa 12.

"Tofauti iliyopo kati ya vibali hivyo viwili ni kuwa kibali cha saa 12 kitaisha inapofika saa 12 jioni bila kujali kilikatwa muda gani wa siku husika. Ndani ya saa 12 ya kibali mgeni anaweza kutoka na kurudi hifadhini bila kulipia tozo ya ziada," anasisitiza.

Amesema kuwa kibali za saa 24 kitadumu kwa kipindi cha saa 24 tangu kilipotolewa na ndani ya muda huo na mgeni anaweza kutoka na kurudi hifadhini bila kulipa tozo ya ziada.

"Uamuzi huu wa serikali unalenga kuinua utalii wa kiutamaduni kwenye maeneo ya wananchi yaliyo nje ya hifadhi za Taifa ambapo wageni hasa watalii walishindwa kuyatembelea kwa kuhofia kulipia tozo mara mbili," amesema Shelutete na kuongeza.

"Uamuzi huu unatarajiwa kuinua utalii wa kiutamaduni kwenye maeneo hayo pamoja na kuongeza kipato cha wananchi katika maeneo hayo na hivyo kufaidika na uwepo wa hifadhi katika maeneo wanayoishi,".


Kamishna Msaidizi Mwandamizi huyo wa Mawasiliano amesema katika jitihada za kuvutia watalii kutembelea hifadhi, serikali imepunguza tozo kwa utalii wa kutembea (Canopy walk way ) kwenye ziwa Manyara kutoka dola za Marekani 60 mpaka 10 kwa raia wa kigeni huku raia wa nchi za Afrika Mashariki tozo hiyo imepungua kutoka shilingi 15, 000 mpaka shilingi 10,000.

Shelutete alisema serikali imetangaza tozo za hifadhi mpya zilizoanzishwa mwaka 2019 za Burigi -Chato, Ibanda - Kyerwa na Rumanyika - Karagwe , Mto Ugala, Nyerere na Kigosi.

Alisema kwa ujumla mabadiliko ya tozo hizo yamelenga  kuongeza idadi ya wataliu, mapato pamojs na kuboresha huduma za utalii ndani ya hifadhi.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano wa
Shirika la Hifadhi za Taifa nchini, (TANAPA),  Pascal Shelutete leo akiongea na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya shirika hilo jijini Arusha.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post