APC YAPATA VIONGOZI WAPYA 2020/2025, GWANDU ACHAGULIWA KWA KISHINDO, WAJUMBE WAMPITISHA ZULFA KUWA KATIBU MKUU

Viongozi wapya waliochaguliwa kuiongoza APC kwa miaka mitano ijayo, kutoka kushoto waliosimama nyuma David Frank(Mjumbe), Pamela Mollel (Mjumbe), Filbert Rweyemamu (Naibu Katibu Mkuu), waliokaa kutoka kushoto ni Cynthia Mwilolezi (Mwekahazina), Mussa Juma (Makamu Mwenyekiti), Claud Gwandu (Mwenyekiti) na Zulfa Mfinanga (Katibu Mkuu Mtendaji)
Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wapya waliochaguliwa
Na Mwandishi Wetu, Arusha

CHAMA cha waandishi wa habari Mkoa wa Arusha (APC), imepata viongozi wapya baada ya waliokuwa wakikiongoza chama hicho kumaliza muda waio wa miaka mitano tangu walipoingia madarakani mwaka 2015.


Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na kamati ya watu wawili iliyochaguliwa miongoni mwa waandishi wa habari ikiongozwa na Mwanaidi Mkwizu (Mwenyekiti wa kamati na Nerbert Mramba pamoja na wafanyakazi wa sekretarieti ya APC Claud Gwandu alichaguliwa kwa mara nyingine kuwa Mwenyekiti wa Klabu hiyo.

Mussa Juma aliyekuwa akichuana na Jane Edward katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti aliibuka kidedea kwa kura 35 na kumshinda Jane Edward ambaye katika uongozi uliokuwa unamaliza muda wake alikuwa mjumbe wa kamati ya utendaji.

Nafasi ya Katibu Mkuu Mtendaji ilinyakuliwa na mwandishi Zulfa Mfinanga aliyemshinda katibu anayemaliza muda wake Mustafa Leu aliyeambulia kura 16 za wajumbe 44 waliopiga kura katika uchaguzi huo.

Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu ililazimika kupigiwa kura upya baada ya aliyekuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo Allan Issack kukosa kura za kumwezesha kuwa naibu katibu mkuu baada ya kupata kura 17 kadi ya kura 44 za wajumbe wote.

Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi aliwahoji wajumbe kuhusiana na nafasi hiyo na wajumbe kukubaliana waliokuwa tayari kuwania nafasi hiyo kujitokeza ambapo wajumbe watatu kati yao walijitokeza akiwemo Allan Issack, Filbert Rweyemamu na Anjelina Karani.

Baada ya wajumbe hao kujitokeza, Filbert Rweyemamu aliibuka kidedea dhidi ya wagombea wenzake na hivyo kutangazwa kuwa mshindi kwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu, huku wajumbe wawili Allan Issack na Anjelina Karani wakiangukia pua kwa kupata kura chache.

Nafasi ya Mwekahazina ilinyakuliwa na mgombea pekee katika nafasi hiyo Cynthia Mwilolezi huku nafasi ya wajumbe wawili wa kamati ya utendaji wa kuchaguliwa ikichukuliwa na Pamela Mollel pamoja na David Frank.

uchaguzi huo ulikuwa wa kihistoria baada ya matukio yote kuonyeshwa moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii huku kura zikihesabiwa kwa uwazi jambo ambalo limepongezwa na wadau mbalimbali.

Awali akitoa hotuba yake ya kumaliza muda wa uongozi, Mwenyekiti aliyekuwa akimaliza muda wake Claud Gwandu aliwataka wajumbe kuchagua viongozi kwa uzoefu na ambao watakuwa na mapenzi mema kwa maendeleo ya APC ikiwemo kushirikiana katika kuwapatia waandishi wa habari maendeleo.

mara baada ya kuchaguliwa uongozi mpya ukiongozwa na Mwenyekiti Claud Gwandu uliahidi mambo mengi kwa wanachama katika kipindi cha uongozi wa miaka mitano ikiwemo kuwaunganisha wanachama na kuwa kitu kimoja.
 

  

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post