NI HAKI YA MWANAHABARI KUPEWA HABARI NA TAASISI ZOTE ZA UMMA NA SIO HISANI- MWAKYEMBE

Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imezitaka ofisi za Umma kutoa taarifa kwa wanahabari kwa kuwa siyo hisani na siyo hiyari, bali ni takwa la kisheria kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18 (d).
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na uongozi wa Arusha Press Club kuhusu namna bora ya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Habari, leo Jijini Dodoma

Kauli hiyo imetolewa na Waziri mwenye dhamana ya tasnia ya Habari Dkt. Harrison Mwakyembe alipokutana na ujumbe wa viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Arusha (APC), kupitia mradi unaouendesha wa Alternative Media leo jijini Dodoma.

“Serikali haina ugomvi na vyombo vya habari, bila vyombo vya habari hatutaweza kuwahabarisha wananachi masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu” amesema Dkt. Mwakyembe.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi (kushoto) akizungumza katika kikao cha Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na uongozi wa Arusha Press Club kuhusu namna bora ya kutekeleza majukumu yao ya kutoa habari sahihi kwa wananchi leo Jijini Dodoma.
Aidha, amewakumbusha wanahabari kuwa kazi wanayofanya ni muhimu sana ambapo nchi zilizoendelea bado wanatumia vyombo vyao vya habari ikiwemo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ambalo lina miaka zaidi ya 90 na linatangaza habari zake kwa lugha zaidi ya 40 ili kuwafikia wananchi wake na dunia kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari kutoka mkoa wa Arusha Bw. Claud Gwandu amemshukuru Waziri Dkt. Mwakyembe kwa mapokezi, majadiliano yenye tija kwa uwazi na ukweli na kumpongeza kwa kazi nzuri anayofanya katika sekta anazozisimamia.
Mwenyekiti wa Arusha Press Club Bw. Claud Gwandu akizungumza jambo wakati wa kikao na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) ambapo walijadiliana masuala mbalimbali yanaohusu tasnia ya habari leo Jijini Dodoma

“Tunamshukuru Waziri kwa kutupa nafasi ili tuweze kushirikiana katika kuimarisha tasnia ya habari iwe bora kwa mustakabali wa nchi yetu” amesema Gwandu.

Amesema APC kupitia mradi wa Alternative Media imefanya utafiti na kupata maoni ya wanahabari na wadau nchini ambao kwa pamoja wanaiomba Serikali ibadilishe sheria  na kanuni mbalimbali  ambazo zimekuwa vikwazo vikubwa katika tasnia ya habari nchini ikiwemo  kanuni namba 4 ya maudhui mtandaoni inayotaka kila anayeanzisha chombo cha habari mtandaoni (online media), kulipa kiasi cha Tsh1100,000 fedha ambazo ni nyingi kulingana na uwezo wa wanahabari nchini.
Aidha, Mwenyekiti huyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya kwa kutekeleza miradi mingi kwa manufaa ya Watanzania na kusisitiza kwa mwenye macho haambiwi tazama.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akipokea kipeperushi cha majukumu ya uongozi wa Arusha Press Club mara baada ya kumaliza kikao na uongozi huo kuhusu namna bora ya kutekeleza majukumu yao ya kihabari leo Jijini Dodoma.

awali akiwasilisha maoni ya wanahabari kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria na kanuni mbalimbali Wakili James Marenga alimweleza Waziri kuwa katika utafiti uliofanywa  na Arusha Press Club umeweza kubaini mambo mengi ambayo yamekuwa kikwazo kwa wanahabari lakini kwa kuanzia wamebainisha mambo machache ambayo ni pamoja na kuiomba Serikali kufanyia marekebisho baadhi ya sheria kama ifuatavyo; 

Sheria ya usalama wa Taifa ya mwaka 1970 sura ya 47 inatakaza mwandishi wa habari kuchapisha taarifa yoyote ambayo ni SIRI lakini haijafafanua taarifa hizo ni zipi. Serikali  inashauriwa kubainisha taarifa hizi ili kuondoa mgogoro usiokuwa wa lazima. Lakini pia kutamka Waziri wa Usalama ni yupi tofauti na sasa.

  • Sheria ya haki na kinga ya Bunge ya mwaka 1988 kifungu cha 27 hakijataja waandishi wa habari kama sehemu ya haki yao kikatiba kuhudhuria bunge na badala yake wamekuwa wakiingia kwa upendeleo.  Serikali inashauriwa kulishauri bunge kubadilisha kifungu hiki na kutaja waandishi wa habari kama ni haki yao kuhudhuria bunge na kuchukua habari.

  • Sheria ya magereza ya mwaka 1967, kifungu cha 91(20) kimekataza afisa yoyote wa magereza kutoa taarifa bila idhini ya Kamishna Mkuu wa Magereza. Serikali inashauriwa kuruhusu afisa yoyote wa kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Wilaya kutoa taarifa kwa waandishi wa habari muda na wakati wowote wanapohitaji taarifa.

  • Sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016 kifungu cha 5(4), haijalazimisha kutolewa kwa taarifa zaidi ya kusema ni haki ya kila mtu kutoa au kupokea taarifa. Serikali inashauriwa kuweka msisitizo katika kifungu hiki kuwa ni haki ya mwandishi kupata taarifa bila kikwazo chochote.

  •  Kanuni ya adhabu (Penal code) kifungu cha 75-76, hakijaweka ulinzi wa waandishi wa habari wawapo katika mikutano isiyokuwa halali na badala yake inatoa ruhusa kwa afisa wa Serikali kupokonya vifaa vya kazi kwa mwandishi atakayekuwa katika eneo hilo.  Serikali inashauriwa kutunga sheria inayompatia ulinzi mwandishi wa habari endapo atakuwa akifanyakazi katika mazingira ya namna hiyo na kuondoa adhabu iliyotajwa kwa kuwa yeye yupo kazini.

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post