KULINDANA KWENYE VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA KIKWAZO KWA USALAMA WA MTOTO


Askari Polisi walio katika mapambano ya kutokomeza Vitendo vya ukatili kwa Wanawake na Watoto wakionesha bango lenye ujumbe huo.
Baadhi ya watoto wakionesha majeraha waliyopata kutokana na  kufanyiwa vitendo vya ukatili na ndugu zao wa karibu.


Kulindana kwenye vitendo vya ukatili wa kijinsia, kikwazo kwa Usalama wa Mtoto
 Na Abby Nkungu, Singida        

TABIA ya baadhi ya wazazi na walezi kumalizia katika ngazi ya familia kesi mbalimbali za ukatili wa kijinsia badala ya kuzifikisha kwenye vyombo vya sheria, imetajwa kuwa ni moja ya kikwazo kikuu katika kutokomeza vitendo hivyo na kuimarisha suala la Usalama na Ulinzi wa mtoto mkoani Singida.


Vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia ni pamoja na ubakaji, ulawiti, vipigo na mimba za utotoni.
 

Uchunguzi umebaini kuwa kutokana na baadhi ya makabila mkoani hapa kuoana kindugu, wengi wao hupenda kusuluhisha na kumaliza kifamilia kesi za ukatili wa kijinsia, zikiwemo zile za makosa ya jinai, bila kuzipeleka kwenye vyombo vya sheria kwa lengo la kulinda heshima ya undugu wao.

Ofisa Miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la SPRF linalojishughulisha na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia mkoani Singida, Mwedinuu Beleko alisema kuwa hali hiyo inajidhihirisha kwenye takwimu zilizokusanywa na Shirika hilo kutoka Kata tano za mradi huo Wilayani Ikungi ambazo ni Puma, Kituntu, Dung'unyi, Mungaa na Siuyu.

Mwedinuu alisema takwimu hizo zinaonesha kuwa katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Februari mwaka huu, jumla ya matukio 56 ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike, wakiwemo walio chini ya miaka minane (8), yaliripotiwa kutokea kwenye eneo la mradi. 

Hata hivyo, alieleza kuwa licha ya matukio hayo kuwa ni makosa ya jinai, matatu tu kati yake ndiyo yaliyofikishwa Mahakamani, 12 yalimalizwa kwa suluhu  katika ngazi ya familia huku mengine yakiishia Serikali za vitongoji, vijiji, Kata na  Vituo vidogo vya  Polisi.

Wadau wanasema kuwa hii imekuwa changamoto kubwa katika utekelezaji wa dhana nzima ya usalama na ulinzi wa mtoto kutokana na jamii kuendeleza matukio ya ukatili wa kijinsia huku kukiwa hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa dhidi ya wakosaji.

"Hebu fikiria, hao wanaowaingilia kimwili watoto wa kike na wa kiume; hata walio chini ya miaka mitano, kisha mzazi au mlezi anapewa kifuta machozi cha mbuzi, ng'ombe au fedha kidogo na suala linaishia hapo. Je, unadhani tunaweza kukomesha vitendo hivi?" alihoji Bernard Maira mkazi wa Wilaya hiyo na kuongeza kuwa hiyo imekuwa ikichochea zaidi vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Maofisa Watendaji, Jackline Samwel wa Kata ya Kituntu na Bakari Seif wa Siuyu walisema kuwa kutokana  na wakazi wa maeneo hayo kuoana kindugu ni vigumu kuchukua hatua za kisheria kwani wao hukubaliana kumaliza kesi kifamilia na iwapo watalazimishwa kwenda mahakamani kutoa ushahidi, huwa hawatoi ushirikiano wa kutosha.

"Huku kuna wazee wanaoheshimika katika kila ukoo na wanaoana ndugu kwa ndugu; hivyo mmoja akitoa kauli kuwa kesi iishe basi wanachinja mbuzi na kunywa supu. Aliyefanyiwa ukatili, hata kama kabakwa na kupewa mimba hafanyi chochote wala hawezi kuwa tayari kwenda kutoa ushahidi Mahakamani kwa hofu ya kutengwa au kulaaniwa na jamii ya ukoo wake" alieleza Bakari.
Akitoa taarifa wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Duniani mwishoni mwa mwaka jana, Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Singida, Inspekta Iddah John Ringo alisema moja ya changamoto inayowakabili ni kukosa ushirikiano kutoka kwa mashahidi kwenye kesi zinapofikishwa mahakamani na baadhi ya ndugu kufanya makubaliano ya kificho kwa lengo la kuondoa kinyemela shitaka lililofikishwa polisi.
Takwimu rasmi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi mkoa wa Singida zinaonesha kuwa jumla ya matukio ya ukatili wa kingono 390 yalitokea katika kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka jana, yakiwemo matukio ya ubakaji 140, kulawiti 160 na mimba kwa wanafunzi matukio 40. MWISHO

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post