Picha : WADAU WA MAJI MKOA WA TABORA WATEMBELEA CHANZO CHA MRADI WA MAJI YA ZIWA VICTORIA


Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Wadau wa Maji mkoa wa Tabora wamefanya ziara kwenye chanzo cha mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria cha Ihelele wilayani Misungwi mkoani Mwanza ili kujionea na kujifunza namna Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira katika mji wa Kahama na Shinyanga( Kahama Shinyanga Water Supply and Sanitation Authority(KASHWASA) inavyozalisha na kusambaza maji katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Wadau hao wa maji wakiwemo viongozi wa serikali ya mkoa na wilaya,madiwani,viongozi wa vyama vya siasa na dini na wananchi wa Tabora wametembelea chanzo cha mradi wa maji ya ziwa Victoria Jumanne Januari 14,2020.

Wakiwa Ihelele wadau wa maji wameshuhudia jinsi maji yanavyotolewa katika Ziwa Victoria,yanavyotibiwa, yanavyochujwa na kusukumwa kwenda kwenye Tenki kubwa la maji lenye ujazo wa lita Milioni 35 za maji lililopo kwenye mlima Mabale wenye urefu wa mita 400 ambapo pia wametembelea tenki hilo.

Akitoa taarifa ya Mradi huo,Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Joshua Mgeyekwa alisema lengo la kuanzishwa kwa mradi huo mwaka 2009 ukigharimu shilingi Bilioni 251 za mapato ya ndani ya nchi ilikuwa ni kutatua changamoto ya maji katika mji wa Shinyanga na Kahama na sasa wanaendelea kusambaza maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Tabora.

Alisema hivi sasa wanahudumia wateja saba ambao ni Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga Mjini (SHUWASA), Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga Mjini (KUWASA),Ngudu,Kishapu,Maganzo,Mgodi wa Mwadui na kusambaza maji katika kamati 64 maji Misungwi na Kwimba na kamati za wateja wadogo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Kahama Mji na Msalala.

Mhandisi Mgeyekwa alisema hivi sasa wanaendelea na ujenzi wa mradi wa Maji katika Mkoa wa Tabora ambao hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya Bilioni 600 na tayari maji yamefika katika tenki la maji Ushirika Nzega lenye ujazo wa lita  milioni 2.5,Kilichobaki ni kuyaweka katika mfumo wa usambazaji.

Alisema miradi inayoendelea kujengwa itafikisha uzalishaji maji hadi lita milioni 64 ifikapo Juni,2025.
"KASHWASA haipati ruzuku kutoka serikalini lakini serikali inawekeza kwenye miradi mikubwa ya maji",alisema.

“Mapato yetu kwa mwezi ni shilingi Bilioni 1.1 ambapo asilimia 60 inakwenda kwenye gharama za umeme na dawa,asilimia 40 inayobaki inakwenda kwenye mishahara ya watumishi wetu na mambo mengine”,alisema Mhandisi Mgeyekwa.

Alisema kutokana na hali hiyo sasa KASHWASA inajitegemea kwa asilimia 100 kwa upande wa gharama za umeme na madawa ya kutibu maji na mishahara ya watumishi hivyo inapata ruzuku kutoka serikalini asilimia 20 tu.

“Changamoto iliyopo ni wateja kutotumia maji. Uwezo wa mtambo wetu ni kuzalisha lita milioni 80 kwa siku lakini kwa mahitahi ya sasa tunazalisha lita milioni 43 tu kwa siku.Tunahitaji wateja wengi zaidi ili watumie maji tunayozalisha”,aliongeza Mhandisi Mgeyekwa.

Akizungumza katika ziara hiyo, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Tabora , Rukia Manduta alisema wamepokea kwa furaha mradi wa maji ya Ziwa Victoria akibainisha kuwa watakuwa wateja wazuri wa KASHWASA.

Manduta alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Tabora kuwa walipaji wazuri wa Ankara za maji,kuwa walinzi wa miundo mbinu ya maji ili kuepuka upotevu wa maji.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Igunga,John Mwaipopo aliipongeza serikali kwa kutekeleza mradi wa maji ya Ziwa Victoria na kuwataka wananchi kuyalinda na kuyatunza maji hayo pindi yatakapofika mkoani Tabora ili kuondokana na changamoto ya maji ambayo imekuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira katika mji wa Kahama na Shinyanga (Kahama Shinyanga Water Supply and Sanitation Authority( KASHWASA) Mhandisi Joshua Mgeyekwa akiwakaribisha wadau wa maji kutoka mkoa wa Tabora walipotembelea chanzo cha mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria cha Ihelele wilayani Misungwi mkoani Mwanza Januari 14,2020. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Joshua Mgeyekwa akiwaelezea wadau wa maji kutoka Tabora kuhusu Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria unaosimamiwa na KASHWASA.
Wadau wa maji kutoka mkoa wa Tabora wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Joshua Mgeyekwa wakati akitoa taarifa ya Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post