WIZARA YA MAJI YAWEKA KAMBI JIMBONI KWA ALIYEKUWA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele wakati wa ziara kwenye mradi wa maji wa Nyahiti
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akielekeza jambo wakati wa ziara yake kwenye mradi wa maji wa Nyahiti, Wilayani Misungwi
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (wa pili kulia) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Anthony Sanga (kulia) wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga (wa pili kudhoto) akieleza jambo wakati wa ziara yao wilayani Misungwi.
UONGOZI wa Wizara ya Maji ukiongozwa na Naibu Waziri, Jumaa Aweso na Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga umeweka kambi Wilayani Misungwi kwa lengo la kupata ufumbuzi wa miradi ya maji inayotekelezwa kwa kusuasua wilayani humo. 

Uamuzi huo umefikiwa wakati wa ziara ya viongozi hao Desema 3, 2019 ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa Wilayani Misungwi ambapo walionyesha kutoridhishwa na hali ya utekelezaji wake. 

Akizungumza juu ya uamuzi huo wa kuweka kambi wilayani humo, Jumaa Aweso alisema hali aliyoishuhudia ya utekelezaji wa miradi ya maji unakwenda kinyume na dhamira ya Rais John Pombe Magufuli ya kuhakikisha wananchi wanaondokana na kero hiyo haraka iwezekanavyo. 

Wakati wa ziara hiyo, Aweso na Naibu Katibu Mkuu Sanga walikuta ujenzi wa mradi wa Ihelele na Mbarika unaotekelezwa na Mkandarasi Shanxi Construction Engineering Corporation ya China ukiwa umesimama kwa madai ya kuchelewa kufika kwa mabomba ya chuma (steel pipes) kutoka kwa mtoa huduma kiwanda cha Tanzania Steel Pipe (TSP) jambo ambalo liliwalazimu kuitisha kikao cha dharura kitakachohusisha wadau wanaohusika na ujenzi wa mradi. 

"Hili suala halikubaliki, Serikali imetoa fedha lakini hakuna kinachoendelea, ninaagiza kesho nikutane na TSP, Mkandarasi na Msimamizi wa mradi KASHWASA ili tupate ufumbuzi wa pamoja," alisisitiza Naibu Waziri Aweso. 

Aweso alisisitiza kuwa hatoondoka Wilayani humo hadi hapo utatuzi wa bomba hizo utakapopatikana ikiwa ni pamoja na TSP kuthibitisha lini watakamilisha na kuleta mabomba hayo. 

"Nimeelezwa kwamba TSP bado inadai kiasi cha fedha ili kukamilisha mabomba, niwathibitishie wananchi wa Misungwi Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametupatia fedha sasa tunataka kiwanda kituthibitishie lini kitakamilisha mabomba haya ya mradi," alisema Aweso. 

Mbali na hilo, Aweso alimuagiza Mkandarasi kuhakikisha ifikapo Machi, 2020 mradi uwe umekamilika na wananchi wanapata huduma

Kwa upande wake Mhandisi Sanga alisisitiza kuwa fedha za kutekeza miradi ya maji Wilayani Misungwi ilikwishatengwa na alisisitiza Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi kama alivyoelekezwa. 

Mhandisi Sanga alishukuru jitihada za Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na kero ya maji ambapo alisema fedha imekuwa ikitoka kwa wakati na hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha miradi. 

"Namshukuru sana Mhe. Rais kwani hajawahi kuchelewa kutupatia fedha ya kukamilisha miradi na amekuwa mstari wa mbele kufuatilia na kila anapoahidi hajaacha kutekeleza," alisema Mhandisi Sanga. 

Mradi wa Maji Ihelele utanufaisha zaidi ya wananchi 81,000 kutoka vijiji vya Nyang'omango, Isesa, Igenge na Mbarika.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post