Sheria ya Fidia ya Uharibifu Wa Wanyamapori Kupitiwa Upya

Serikali ya Tanzania ipo katika hatua ya kupitia upya sheria ya fidia ya uharibifu unaofanywa na wanyamapori  ili kuendana na wakati na gharama halisi  ya mazao yanayoharibiwa na wanyama hao ili  kupunguza malalamiko ya wananchi juu ya kutokupewa  fidia stahiki inayoendana na uharibifu hao.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ,Profesa Adolf  Mkenda wakati akizungumza katika mkutano wa wadau wa uhifadhi na maliasili uliondaliwa na Jumuiko la Maliasili nchini Tanzania (TRN) ,ambapo amesema kuwa sheria hiyo ya mwaka 1974  inafanyiwa mapitio na kufanyiwa marekebisho ili wananchi waweze kupata haki pale uharibifu unapotokea.

Profesa Mkenda asema kuwa marekebisho yatakayofanyika yataweza kupunguza malalamiko yaliyokua yakitolewa na wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi lakini pia wizara hiyo imekua ikigawa mizinga ya nyuki kama njia mojawapo ya kukabiliana na uharibifu wa wanyamapori hususan tembo.

Aidha amesema kuwa katika kukabiliana na uwindaji wa kitoweo baada ya kufanikiwa kutokomeza uwindaji haramu wa tembo kwa sasa wizara inakamilisha mchakato wa kuwa na sehemu za kuuza nyama pori katika maeneo yanayozunguka hifadhi ili kuepuka uwindaji wa kitoweo katika maeneo ya uhifadhi.

Mbunge wa Babati Vijijini Jitu Soni  amesema kuwa kurekebishwa kwa sheria ya fidia kutawafuta wananchi machozi hasa wanaoishi mbali kidogo na hifadhi tofauti na wale walioko karibu na pia itasaidia kuhamasisha uhifadhi endelevu miongoni mwa wananchi.

Mkurugenzi wa Jumuiko la Maliasili nchini Tanzania Zacharia Faustine  amesema kuwa mchakato wa kulipa fidia umekua ukichukua muda mrefu na kiasi wanacholipwa hakiendani na hasara jambo ambalo linaweza kushusha hamasa wa wananchi kushiriki katika uhifadhi hivyo serikali imefanya vyema kupitia sheria hiyo.

Mmoja wa wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi za taifa,Asha Salim  amesema kuwa marekebisho sheria ya fidia imekua sio rafiki kwa wananchi hivyo inapaswa kuangaliwa upya kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post