Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Yakiwa Kukomesha Michezo Michafu Katika Huduma Ndogo Za Fedha

Na. Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kusimamia Sekta Ndogo ya Fedha kikamilifu ili kukomesha michezo michafu inayofanywa na  baadhi ya watoa huduma ndogo za fedha nchini na kusababisha  upotevu wa mali za wananchi.

Ametoa maagizo hayo, wakati akizindua Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha, uliowakutanisha wadau mbalimbali zikiwemo Wizara, Idara, Taasisi na watoa huduma za fedha.

 Alisema kuwa kuna taasisi za huduma ndogo za fedha ambazo zinatoa mikopo kwa masharti magumu ikiwa ni pamoja na viwango vikubwa vya riba na  tozo ambazo huanzia asilimia 3 mpaka asilimia 20 kwa mwezi ambayo ni sawa na asilimia 36 mpaka 240 kwa mwaka na pia kukosekana kwa uwazi na masharti ya mikataba ya mikopo.

 ‘’Naiagiza Benki Kuu ya Tanzania ifuatilie kwa makini mwenendo wa utoaji wa huduma ndogo za fedha kupitia mitandao (Digital Microfinance Services) na pia elimu kwa umma ya huduma hiyo ya fedha iwe endelevu na itolewe nchi nzima”, alieleza Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango alisema kuwa kwa muda mrefu takribani wananchi milioni 15.4 sawa na asilimia 55.3 ya nguvu kazi ya Taifa walikua wanatumia huduma ndogo za fedha bila kuwepo kwa Sheria ya kutambua na kulinda haki zao.

Aidha alisema kutokuwepo kwa sheria inayosimamia huduma hizo za kifedha kulisababisha kukosekana kwa uwazi wa masharti ya mikataba ya mikopo kwa kutopatikana kwa takwimu sahihi za uendeshaji za watoa huduma hizo

Dkt. Mpango  alisema kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali ilitunga Sheria ya huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake zilizotungwa mwaka 2019, ambazo lengo lake ni kuhakikisha watumiaji wa huduma hizo wanalindwa kikamilifu.

‘’Sheria hii inatambua madaraja manne ya taasisi zinazotoa huduma za fedha ambapo Daraja la Kwanza ni zile zinazopokea amana, daraja la pili ni taasisi zisizopokea amana, daraja la tatu linahusu vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na daraja la nne ni vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha”, aliongeza Dkt. Mpango.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa BoT tawi la Kanda ya Kati, Bw. Richard Wambali, ambaye alimwakilisha Gavana wa Benki hiyo Prof. Florens Luoga, amewataka watoa huduma ndogo za fedha kuisoma na kuielewa sheria na kanuni zake ili wazitekeleze kwa ufanisi.

Pia amewataka wadau hao kutumia muda wa miezi 12 iliyotolewa na Sheria kuweka mifumo na taratibu za biashara kuendana na matakwa ya Sheria na Kanuni ili ifikapo Oktoba 31, 2020, muda mbao umeainishwa kisheria kuwa ni mwisho wa kutekeleza masharti hayo wawe wamepata leseni hizo kutoka BoT au kwa mamlaka zilizokasimishwa majukumu hayo.

Aidha amewataka kuzingatia mazingira na fursa mbalimbali zinazotokana na uwepo wa Sheria na Kanuni kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wananchi ambao hawajafikiwa na sekta rasmi ya fedha.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa kuendeleza Sekta ya Fedha (FSDT), Bi. Irene Mlola, alisema kuwa Mfuko huo utaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuwa anaamini nafasi ya  huduma za kifedha katika kumkomboa mwananchi kwenye hali ya uchumi na kumsaidia kimaendeleo katika kupunguza umasikini.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post