WAZIRI LUKUVI AAGIZA MASHAMBA 24 KILOSA KUPELEKEWA ILANI YA KUFUTWA


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na uongozi wa wilaya ya Kilosa pamoja na Watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wakati wa muendelezo wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi mkoani Morogoro.
Baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (hayupo pichani) alipokwenda wilayani Kilosa wakati wa muendelezo wa ziara yake kutatua migogoro ya ardhi mkoani Morogoro.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale wakati wa muendelezo wa ziara yake mkoani humo kutatua migogoro ya ardhi. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi.
Baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (hayupo pichani) alipokwenda wilayani Kilosa wakati wa muendelezo wa ziara yake kutatua migogoro ya ardhi  mkoani Morogoro.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
 
 
Na Munir Shemweta, WANMM KILOSA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameagiza mashamba 24 yaliyopo katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kupelekewa ilani ya kufutwa kutokana na kutoendelezwa na hivyo kukosa sifa ya kumilikiwa na wamiliki wake.

Lukuvi alitoa agizo hilo leo tarehe 8 Novemba 2019 wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro alipozungumza na uongozi wa wilaya ya Kilosa na watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya hiyo akiwa katika muendelezo wa ziara ya kutatua migogoro ya ardhi katika mkoa wa Morogoro.

Alisema, wilaya ya Kilosa haina kumbukumbu za mashamba jambo lilosababisha wizara yake kuamua kufanya upekeuzi maalum wa mashamba yote katika wilaya hiyo na kubaini mashamba 24 yasiyoendelezwa tofauti na mashamba 48 yaliyopendekezwa kufutwa awali.

Kufuatia agizo hilo la Lukuvi, sasa wilaya ya Kilosa itakuwa na mashamba 72 yanayotakiwa kufutwa baada ya mashamba 48 ya awali kupendekezwa kufutwa kutokana na kutoendelezwa.
‘’Maafisa Ardhi  wa Wilaya ya Kilosa mfanye upekuzi wa mashama yote yasiyoendelezwa bila upendeleo wala kumuangalia mtu usoni na wala msitishwe na mtu yoyote kwa cheo chake au utajiri wakati wa kufanya kazi hiyo’’ alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi alisema, lengo la serikali kufuta mashamba yasiyoendelezwa ni kuwafikiria wananchi wanyonge wasiokuwa na ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na kubainisha kuwa mashamba yatakatayofutwa yatagawiwa kwa wananchi na mengine yatatumika kama ardhi ya akiba itakayotumika kwa shughuli za uwekezaji.

Aidha, Lukuvi amekemea tabia ya baadhi ya wananchi wa wilaya ya Kilosa kuuza ama kukodisha mashamba wanayopatiwa na serikali na kusisitiza kuwa katika kukomesha tabia hiyo Wizara yake inaangalia namna ya kugawa mashamba yaliyofutwa  kwa vikundi na kwa wale watakaopatiwa hawataruhusiwa kuuza na kuwataka Maafisa Ardhi kutofanya uhamisho wa shamba kwa yule aliyepatiwa .

‘’ Mkuu wa Wilaya komesha tabia ya udalali wa mashamba unaofanywa na baadhi ya wananchi wa Kilosa na yale mashamba yanayogawiwa kwa wananchi yatumike kwa shughuli zilizokusudiwa’’ alisema Lukuvi.

Vile vile, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza wafugaji wote wanaomiliki maeneo yenye hati kuweka uzio katika maeneo yao ili kuepuka mifugo yao kwenda maeneo ya wakulima na kusisitiza kufanyika ufugaji wa kisasa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ameomba kufanyika ukaguzi wa ardhi za vijiji kwa kuwa baadhi yake watu wamejimilikisha, wameuza na mengine kufanyika mgawanyo usio sahihi. Kwa mujibu wa Mgoyi halmashauri ya wilaya ya kilosa imeshindwa kufanya uhakiki kutokana na kutokuwa na fedha jambo alilolieleza kuwa limechangia migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo na kusisitiza kuwa tegemeo la wilaya yake kwa sasa ni mashamba yaliyofutwa pekee.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema vijijji viwili vilivyosajiliwa katika maeneo ya hifadhi wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro vitaendelea kubaki katika maeneo hayo kufuatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia vijiji 920 vilivyokuwa katika maeneo ya hifadhi kuendelea kubaki maeneo hayo.

Lukuvi amevitaja vijiji vya Mjambaa kilichoko katika shamba la Mbugani Estates lenye ukubwa wa ekari 1600 na kile cha Mambegwa kuwa vitaendelea kutambuliwa na kuagiza  halmashauri ya wilaya ya Kilosa kwenda kuvipima na kuanisha shughuli za kilimo na makazi katika vijiji hivyo

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post