Uchunguzi uliofanywa na kituo cha televisheni nchini Kenya
umefichua ni jinsi gani sera dhaifu zilivyoruhusu viwango vya hali ya juu vya
unga wa ugali wenye sumu kuvu - aflatoxin kuuzwa nchini humo jambo
lililosababisha watu wengi kuhoji juu ya viwango vya usalama wa chakula nchini
humo.
Uchunguzi uliofanywa na televisheni ya kibinafsi NTV ulifanya
vipimo vya unga wa Ugali wa mahindi na mtama za nembo aina 12 za bidhaa hizo za
nafaka.
Nembo tatu zilibainika kuwa na viwango vya hali ya juu vya
sumukuvu kuliko kiwango kinachopendekezwa cha sehemu 10 kwa bilioni, huku saba
zikiwa bado zikiwa na viwango vya hali ya juu vya sumukuvu (aflatoxin).
Aflatoxin, ambayo hutengenezwa na fangasi katika mazao ya
kilimo na inaweza kusababisha saratani.
Wiki moja tu iliyopita Mamlaka ya Kenya ya viwango (kebs)
ilinyang'anya makampuni ya utengezaji wa Siagi ya karanga inayotumiwa zaidi
kupakwa kwenye mikate kutokana na hofu kuwa ilikuwa na sumu kuvu. Pia ilionya
Umma dhidi ya kutumia kama chakula cha unga wa ugali kutoka makampuni matano ya
unga wa mahindi.
Madaktari na wataalamu wa chakula waliohojiwa katika taarifa
ya uchunguzi ya runinga walisema kuwa baadhi ya watu walikufa kutokana na ulaji
wa unga huo unaodaiwa kuwa na sumukuvu.
Madaktari pia walihusisha visa vya saratani za ini na mfuko
wa uzazi na ulaji wa ugali wenye sumu kavu.
Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, ambaye pia alihojiwa na
uchunguzi wa runinga, alithibitisha kuwepo kwa sumu ya sumukuvu katika vyakula
nchini humo .
Alisema kuwa wana wasiwasi kuwa wanyama wanaofugwa nyumbani ,
kama vile ng'ombe, pia wanakula vyakula vyenye sumu jambo ambalo pia hushiriki kuisambaza
kwa walaji.
Bwana Kiunjuri alilaumu biashara ya kikanda kuwa sababu ya
kuwepo kwa chakula chenye sumu.
"Huwezi kusema kuwa utapambana nayo ndani ya mipaka ya
Kenya. Tunabadilisha ," alisema.
Mahitaji ya hali ya juu ya chakula kikuu unga wa mahindi
yamekuwa yakiilazimisha serikali kubuni sababu ya kuagiza mahindi kutoka nje ya
nchi.
Mwaka 2009, Mkurugenzi Mkuu wa Kebs Kioko Mangeli alifichua
kuwa Wakenya wamekuwa wakila ugali wenye sumu tangu mwaka 2008, huku serikali
ikiwa na uelewa fika wa hilo.
"Nina uhakika wa zaidi ya 100% kwamba inawaathiri watu
na kwamba katika kipindi cha miaka 10 hadi 15 tutakuwa pia na visa vingi vya
saratani kutokana na mahindi ," Bwana Mangeli aliiambia kamati ya bunge la
Kenya.

Kutokana na hayo Wakenya wameingia katika mtandao wa habari
wa kijamjii wa Twitter kupitia hashtag #WhiteAlert huku wakiitaka serikali
iwakamate maafisa wanaohusika na kuhakikisha viwango vya usalama wa chakula
nchini humo.
Hali ikoje kwa Tanzani
juu ya Sumukuvu katika nafaka?

Tanzania ikiwa ina matumizi ya nafaka kwa kiwango kikubwa
Afrika mashariki, vyakula ambavyo vinaweza kuambukizwa sumu kuvu ni kama vile
mahindi na unga wake, karanga na mazao yanayotokana na karanga, muhogo.
Sumu kuvu inatokana na fangasi ambayo inayoota kwenye mbegu
za nafaka, hutokea pale ambapo nafaka ikiwa imetunzwa vibaya.
Sumu hiyo mara nyingi husababisha kansa ya ini na inaweza
kusababisha vifo vya watu kwa pamoja na kama watu wakila chakula hicho kwa
pamoja basi wote wanaweza kuathirika.
Sumu kuvu (fangasi) unaoota kwenye mbegu za nafaka na jamii
ya kunde, mazao ya mizizi na karanga.
Mtaalamu wa masuala ya Afya na mwandishi kutoka nchini Tanzania
Syriacus Buguzi anasema kuwa Sumu kuvu ni tatizo kubwa nchini Tanzania, utafiti
uliofanyika mwaka 2012 uliangazia taifa zima na kuonyesha jinsi sumu hiyo
inaweza kuathiri chakula kwa kiwango kikubwa.
Mwaka 2016, kesi 65 ziliripotiwa katika maeneo ya Chemba na
Kondoa mkoani Dodoma na watu 19 walifariki dunia kutokana na ugonjwa
unaojulikana kitaalamu kama 'Aflatoxicosis' unaosababishwa na sumu kuvu kwenye
nafaka iliyoharibika.
Buguzi anasema mara nyingi athari hii inapowatokea watu, ni
ngumu kugundua chanzo cha tatizo lililowapata kutokana na uelewa kuwa mdogo
bado.
